Mabingwa wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika huingiza kwenye akaunti zaidi ya dola milioni 1.5. Si fedha chache, na ni chanzo cha mtaji wa timu nyingi zinazobeba taji hilo.

Klabu kama TP Mazembe inawalipa mshahara wachezaji kutoka mataifa mengi ya Afrika kwa sababu ya matumizi mazuri ya fedha za ubingwa wa Afrika na hata zile fedha za ushindi wa pili pamoja na zile ambazo klabu zinapata kwa kuweza kufikia hatua za mwishoni za michuano.

 Yanga na Azam FC wanazo changamoto nyingi njiani kabla hawajaanza kutia kibindoni fedha zitolewazo na CAF kwa mabingwa wa Ligi ya Mabingwa pamoja na wale wa Kombe la Shirikisho.

Changamoto ya awali kabisa ambayo timu zetu zitatakiwa kupambana nayo ni ile ya upatikanaji wa wachezaji wa kimataifa ambao watakuja kuimarisha timu.

Unakumbuka miaka michache nyuma, TP Mazembe iliwekeza kwenye utafutaji wa wachezaji bora, ambao wanalingana viwango na wale wa timu kubwa za Afrika Kaskazini na Magharibi. TP Mazembe ikifungwa na Raja Casablanca magoli 2-1 kule Morocco, inakuja kuifunga timu hiyo magoli 3-1 pale DRC.

 Wale wanaopinga wingi wa wachezaji wa kigeni kwenye timu zetu za ligi kuu watazame mbali zaidi ya kuutetea ukosefu wa ushindani tulionao kwenye soka letu.

Hakuna njia tunayoweza kuibuni, ambayo itatupatia mafanikio sawa na yale ya klabu kubwa barani Afrika, tumeshaweka misingi ambayo inaweza kutumika kama mifano hai ya maendeleo ya soka.

Miaka michache nyuma, Yanga ilifungwa na Al Ahly kwa penalti kule Misri, tofauti ya kiuchezaji haikuwa kubwa kati ya timu hizo mbili. Yanga ilihitaji wachezaji wachache wenye viwango vya wale wa Al Ahly na Waarabu wangefungasha virago ndani ya ardhi yao.

Yanga pia ilishafanya vibaya katika michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kufungwa na Etoile du Sahel kule Tunisia, Yanga ilihitaji akili za wachezaji wachache wa kigeni wenye maarifa kama ya wale Watunisia.

Azam FC na yenyewe ina kila sababu ya kuwatafuta wachezaji bora wa kigeni, udhaifu wa wachezaji wa Tanzania wanaochezea timu hii uko dhahiri kabisa. Azam FC inao wachezaji wengi wazalendo ambao pamoja na kupata huduma bora za kimaisha, bado hawana uwezo wa kuifikisha mbali kimataifa.

Alipoondoka Kipre Tcheche, walitakiwa kuwasaka kina Kipre wengi zaidi, kwani wataleta shauku ya vijana wazalendo kutaka kufika mbali. Naamini kocha wa sasa ni mzoefu, hivyo anaifahamu fika ile tofauti iliyopo kati ya wachezaji wazalendo na wale wa kigeni.

Wachezaji wa kigeni wenye vitu vingi vya ziada kulinganisha na hawa wa kwetu, watakuja kutuonyesha umuhimu wao, wakati klabu zetu zitakapoanza kupokea fedha ndefu kutoka makao makuu ya CAF, baada ya kumaliza michuano mikubwa tukiwa katika nafasi za juu.

Hispania ya Xavi Hernandez ndiyo ilikuja kubeba makombe makubwa kuanzia ngazi ya klabu mpaka ile ya timu ya taifa. Kaka zao hawakuwa na mafanikio mengi ya kuweza kujivunia.

Wachezaji wa kigeni kutoka kila kona ya dunia wamechangia katika kuongeza ubora wa vituo vya kulea vipaji vya Hispania. Timu moja ina nyota kadhaa kutoka Brazil, ina mafundi kutoka Argentina, ina wachezaji wenye nguvu kutoka Afrika Magharibi, matokeo yake makocha wazalendo wakajikuta wakilazimika kuongeza ufanisi wa kazi na wakatengeneza kizazi cha ushindi.

Bila ya uwepo wa wachezaji wa kigeni, pengine La Masia isingekuwa na mafanikio ya kuzalisha wachezaji wa bei kubwa.  Hakuna taifa ambalo linaweza kujitegemea kwenye soka likiwa limesimama lenyewe pasipo muingiliano wa tamaduni za uchezaji.

Wajerumani walijaa kiburi cha Kijerumani lakini taratibu wakaanza kuwapatia nafasi vijana kutoka mataifa mengine. Leo hii wachezaji wenye asili ya Uturuki kama Mesut Ozil, Shkodran Mustafi na Sami Khedira ni sehemu ya kikosi cha kwanza cha timu ya Taifa ya Ujerumani.

Tunawahitaji wachezaji wengi wenye umri mdogo kutoka mataifa kama Nigeria, Cameroon, Guinea, Ivory Coast, DRC na Senegal ili waje kuongeza ushindani wa namba kwenye klabu zetu. Ushindani ambao unaweza kabisa kuboresha hata ufanisi wa vituo vya kulea vipaji.

Ligi Kuu ya Afrika Kusini imefaidika kwa miaka mingi kupitia ushindani wa wachezaji wa mataifa mengi ya Afrika. Ni lazima tupite njia zile zile walizopita wenzetu wakiwa katika safari ya utafutaji wa maendeleo ya kweli ya soka.

 Yanga au Azam FC hawatataka kurudi nyuma kama ikitokea wakaanza kulipwa fedha baada ya kutwaa ubingwa wa Afrika au baada ya kumaliza wakiwa kwenye nafasi nne za juu.

By Jamhuri