Huu ni usemi wa Kingoni unaotahadharisha wanadamu duniani. Una maana ya kuwa “Watu ni hatari”. Kwa lugha ya Kingoni neno ‘likoko’ ni mnyama au mdudu wa kuhatarisha sana na anaweza kumdhuru mtu wakati wowote ule. 

Basi kwa usemi huo kuwa “Wandu makoko” tunakumbushwa daima kuwa watu ni viumbe hatari hapa duniani. Pengine kwa Kingoni tunasema “Wandu tilandine manjwili nambo kumtima tiwi ta makoko” yaani watu (binadamu) tumefanana kwa nywele zetu (maumbile ya nje), lakini mioyoni mwetu tuko kama wanyama au wadudu wabaya (tuko tofauti sana kati ya mtu na mtu). 

Hivyo usione ajabu, swahiba wako akakugeuka na kukudhuru – utashangaa lakini ndiyo ukweli wenyewe duniani. Hata enzi za Warumi tunasikia Kaisari akiwa vitani alipigwa mkuki na swahiba wake Brutus na alipogeuka kutaka kumuona ni shujaa gani huyo aliyemfikia hata kumchoma kwa mkuki ule wa kifo, akaona eti au kumbe aliyemtenda vile ni yule swahiba wake wa karibu sana – Brutus. Hapo kwa mshangao mkubwa Kaisari akalia kwa sauti alisema “Et tu Brutus” (kwa Kilatini) akimaanisha hata wewe Brutus! Basi hapo ndipo chanzo au asili ya kutokea usemi ule wa “umdhaniaye ndiye, siye” na yule usiyemfikiria huwa ndiye. 

Kwa utangulizi huu, mimi bado ninaamini kuwa hii “Stalemate” au mkwamo wa kisiasa uliotokea Zanzibar, utatatuliwa tu na WazanzibarI wenyewe. Kamwe hauwezi kutatuliwa kwa nguvu au watu wa nje ya nasaba ya Uzanzibari. Kwa nini nasema hayo?

Niliwahi kuandika makala yenye kichwa cha habari, “Siasa za Zanzibar za aina yake” katika gazeti hili la JAMHURI Desemba, 2015. Nikapokea meseji kadha kuhusu maoni na mawazo yangu yale. Moja ya meseji zile nainukuu hapa inasomeka hivi, “Mzee Mbenna, call “a spade, a spade”. Lowassa angekuwa madarakani leo Visiwani biashara ingekuwa imekwisha. Pasipo haki hakuna amani. Ndicho kitu kinachotengenezwa hapo visiwani. Tukishaanza kutiliana mashaka ya Ki-Afro na Kihizbu basi ghasia zinatengenezwa. Kuwa mkweli na muwazi. Nakushangaa leo unamsifia Lowassa kwa busara. Basi toa ushauri mtakatifu nini kifanyike visiwani. Wahenga walisema “Kiti kisicho chako, ukikalia kitakutesa” Ujumbe kutoka simu Na. +255 755 339 859 Desemba 9, 2015 saa 9.31 alasiri (3:31 pm). 

Hii meseji sina shaka imetoka kwa Mzanzibari, akinitaka niwe mkweli tena nitoe ushauri nini kifanyike kule visiwani kuondoa hii hali ya wasiwasi na mkwamo uliotokea kule Visiwani baada ya kufutwa matokeo ya ule Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015. Hii ndiyo moja ya changamoto za uandishi wa makala na kila itokeapo changamoto ni lazima ipokewe na itendewe kazi. Nimeipokea. 

Nikaanza kuangalia makala mbalimbali zinazoandikwa na waandishi waliobobea katika mambo ya Zanzibar. Wapo Wazanzibari wengi tu, wametoa maoni, mawazo na kuchimbua kihistoria kuonesha nini kimetokea kule hata kusababisha hali hii iliyofikiwa sasa. Kwa uchambuzi wangu mimi niliyeishi kwa muda fulani (miaka 3) nikifanya kazi katika Serikali ya SMZ wakati wa Rais wa Awamu ya Pili, Alhaji Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, napenda nitoe maoni yangu wazi hapa kama changamoto iliyotolewa kwenye meseji. 

Baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964, Serikali ya Mapinduzi iliyoundwa na Mzee Abeid Amani Karume ilikuwa na mchanganyiko – ilitia wana Mapinduzi ambao wengi wao hawakuwa na elimu ya kutosha na wasomi pia. Hii ililenga kuyalinda Mapinduzi yale matukufu na kuendeleza nchi kiuchumi kupitia wale wasomi. 

Ukiangalia Baraza lake la kwanza la Mawaziri tunaona aliwatia wasomi kama Sheikh Abdulla Kassim Hanga ambaye alimpa Umakamu wa Rais, na Uwaziri Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Abdulrahman Mohamed Babu, Mambo ya Nje na Biashara, Dk. Othman Sharif, Elimu na Utamaduni, Sheikh Saleh Sadala, Kilimo, Hasnu Makame, Fedha na Mipango, Mzee Aboud Jumbe, Afya na Ustawi wa Jamii, Sheikh Idris Abdul Wakil, Mawasiliano na Kazi. 

Hapo utaona namna Sheikh Karume alivyodhamiria kuendesha Serikali yake kwa kuenzi Mapinduzi na kwa kuleta maendeleo endelevu kupitia wasomi kadhaa. Tunasema ali-balance kati ya wasomi na wale wazee wa Mapinduzi. 

Mimi nilichokiona ni kuwa palitokea na hali ya wasiwasi kati ya wale wazee 14 waliopanga na kuongoza Mapinduzi (hawakuwa na elimu ya kutosha, lakini walikuwa na uzalendo kwa Uafrika wao katika nchi yao) na vijana wasomi akina Othman Sharif, Aboud Jumbe (Ualimu) (Makererian), Abdulrahman Babu na Kassim Hanga (Urusi), Hasnu Makame na Idris Abdul Wakili. Hivyo hali ya kutokuaminiana ilijitokeza tangu mwanzo wa Serikali ya Mapinduzi. Na kwa vile Baraza lote la Mapinduzi lilitawaliwa na hao wasiokuwa na elimu nzuri – akina Seif Bakari, Abdallah Natepe, Hamisi Hemedi, Hafidh Seleman, Hamisi Daruweshi, Saidi Ali Bavuani, Yusuf Himid, Saidi Washoto na kadhalika, basi wasomi hawakujiona kuwa wako salama. Hapo, mshikamano kisiasa (stability) kati ya Baraza na Serikali haukuwapo. Ndiyo sababu mpaka leo kule Zanzibar hakuna kuaminiana miongoni mwa wasomi na makabwela wakazi wa huko visiwani. 

Pili kuna hali ya kudharauliana sana kati ya Waunguja na Wapemba. Inasemekna huko nyuma baada ya Mapinduzi, waziri mmoja Mmkakunduchi aliwakejeli Wapemba kwa kusema akili za Mmakunduchi mmoja ni sawa na akili za Wapemba watano! Hilo Wapemba karibu wote wanalizungumzia. Hakuna maelewano kati ya Wamakunduchi na Wapemba. Basi kwa ujumla wa mambo kama hayo miongoni mwa Wazanzibari, yanafanya mshikamano kati ya Waunguja na Wapemba kuwa legelege. 

Kihistoria, wapo waandishi wa Zanzibar wanaweka wazi uhusiano uliopo kati ya Wapemba na Waunguja. Kwa uasilia, miingiliano, nasaba na kisiasa ni vitu vinavyochochea kukosekana kwa huo umoja kule visiwani. Kadhalika, hali hiyo inapunguza upendo miongoni mwa wazanzibar, na hiyo inaleta ile taswira ya Uunguja na Upemba. Upo ukweli usiopingika kuwa zipo tofauti zinazoonekana waziwazi kati ya Wapemba na Waunguja. Kuna lahaja tofauti baina ya wakazi wa Unguja na Pemba. Tamaduni zao ni tofauti. Desturi na ikhlaq za matambiko ya kijamii ni tofauti. Kisiasa inafahamika wazi Pemba ni ya Jumuiya ya Arab Association Party by subjects of Sultan (NZPSS) wakati Unguja ni haswa ya Waafrika wana African Association tu. 

Tangu hapo zamani enzi za usultani idadi kubwa ya Wapemba wanaishi kwao Pemba na wachache sana wamehamia Unguja kufanya makazi yao. Vivyo hivyo Waunguja hawafikirii kwenda kufanya makazi Pemba labda wahamishiwe huko kikazi na hili Waunguja wanaliona kama uhamisho wa adhabu kupelekwa Pemba. 

Hali hiyo ilikuwapo hata huku bara. Mchagga au Mhaya kuhamishiwa mikoa ile ya Kusini (Southern Province) enzi za ukoloni ilikuwa ni kiashiria cha adhabu. Nadhani wazee wengine wanakumbuka miaka ile ya 1960 na 1970, wapo maofisa walikuwa wanakacha uhamisho wa Kusini. Upo mwaka Mwalimu Julius Nyerere alimhamisha Mkuu mmoja wa Mkoa kutoka Tanga kwenda Lindi (huyu mkuu alikacha uhamisho ule) na hakwenda, ikamfanya Mwalimu amteue mtu mwingine kuwa Mkuu wa Mkoa  akampeleka Lindi na yule mswahili wa Tanga akafutwa cheo cha u-RC hapo hapo. 

Mimi najua Katibu mmoja wa CCM Mkoa alikacha kwenda Lindi, lakini aliona heri kupelekwa Pemba kuliko kwenda Kusini (jina ninalo). Basi hata kwa visiwani hali hiyo ipo hadi leo. 

Inaaminika Unguja na Pemba hadi leo wamekuwa marafiki wa mashaka. Hawaaminiani wala hawawezi kusafiri masafa mrefu wakiwa wamoja bila katikati ya safari yao kubaguana kila waoneshanapo visogo. Kwa mtazamo huo Pemba tangu enzi za ukoloni hawajaunga mkono ASP na hata leo hii hawaiungi mkono CCM. Hivyo wao hata ule wakati wa Tume ya Mabadiliko Pemba walitaka Serikali ya mkataba – hawaungi mkono maoni ya Unguja kuwa na Muungano tulionao sasa. 

Mpaka hapa niandikapo makala hii, Pemba hakuna Diwani wa CCM na wala Mbunge wa CCM ndiyo sababu kila utokeapo Uchaguzi Mkuu kura za urais kwa Pemba zinakuwa kidogo sana kwa CCM tunaita ‘kiduchu’! Kwa imani yao Wapemba wengi wanaona wanabambikizwa tu hili wazo la Muungano. Ingekuwa uamuzi wao kimapenzi na hiari basi wangeamua Pemba iwe kivyake na Unguja kivyake. Wanatamani utengano wa visiwa hivyo.  

Lakini mimi kwa ukweli kabisa naweza kusema kuanzia Serikali ya Awamu ya Pili kule Visiwani, Mzee Jumbe alinuia kuwa na “autonomy” kwa Visiwa vya Unguja na Pemba. Alipendelea wasomi waachane na yale mawazo ya wazee walioasisi yale Mapinduzi ya Unguja. Kwa fikra zangu alipendelea awe Rais kamili wa Visiwa vya Unguja na Pemba na siyo kwa Muungano kama ulivyoasisiwa na Sheikh Abeid Karume. Hivyo alianza kuwatumia wasomi wa Pemba kumjengea uhalali wa hiyo “autonomy” ya kule Visiwani. Kuanzia alipochukua madaraka Aprili 1972 alijaribu kutafuta njia za kupunguza uwezo na nguvu za waasisi wa Mapinduzi kule Visiwani. 

Ninakumbuka nilipopelekwa kuanzisha chombo cha JKU, Mzee Jumbe alikuwa muwazi kuwa kisiitwe JKT na akatoa jina la Jeshi la Kujenga Uchumi ndiyo (JKU). Hivyo mpaka leo chombo kile cha kulea vijana Visiwani kinaitwa Jeshi la Kujenga Uchumi na siyo la Kujenga Taifa. Ingawa yeye mwenyewe alipitia ukuruta JKT-Ruvu Operation Kazi ‘B’ Januari 1968.

 

>>ITAENDELEA

2151 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!