Mgana msindaiAwali ya yote nawapongeza Wahifadhi wote wanaoendelea kuhakikisha wanyamapori wanaendelea kuishi kwa utulivu baada ya ujangili kupungua kidogo.

Nawashukuru Wahifadhi, Polisi na Mahakama kwa hatua kali walizochukua hivi karibuni huko Mbeya, Mpanda na nakadhalika kwa kuyatupa majangili jela kwa miaka mingi bila kujali sehemu walikotoka. Hongera sana.

Nitoe masikitiko makubwa kwa Faru na mtoto wake kuuawa kikatili ndani ya Hifadhi ya Serengeti. Hii ni hifadhi ambayo Faru wake wanalindwa saa 24.

Lengo hasa leo nikuandika juu ya pori dogo la Mgori, lenye wanyamapori wengi sana, ndege, wadudu, misitu – mimea ya miti mbalimbali ikiwemo Mninga. Pia kuna chemchem nzuri za maji.

Msitu ambao sasa hivi Serikali isipoingilia utakwisha hivyo kupunguza maeneo mazuri yenye rasilimali nyingi mkoani Singida.

Msitu wa Mgori upo Wilaya ya Singida Vijijini, lakini ni pori kama halina mwenyewe maana halitengewi bajeti na Halmashauri ya wilaya wala halipati ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Hili ni pori lenye wanyama wote wenye sifa za kitalii kama vile Tembo, Simba, Chui, Pundamilia, Swala Digidigi, Tandela, Ngiri, Sungura Mwitu na Ndege wa aina nyingi. Kuna vijito na chemchem zisizokauka.

Awali maji ya chemchem hizo yalikuwa yanatumiwa wakazi wa Wilaya ya Ikungi na Chemba Mkoa wa Dodoma na Hanang mkoani Manyara.

Pori hili dogo linazungukwa na kuingiliwa na vijiji vya Kohoma, Ngimu, Landa, Unyampanda, Mughunga, Dua Muganga na Mukulu kilichopo mpakani Wilaya ya Chemba.

Mgori ni pori la asili ambalo liko chini ya   Halmashauri ya Singida Vijijini, Jimbo la Singida Kaskazini chini ya ubunge wa Lazaro Nyalandu aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii mpaka 2015.

Hata hivyo, bila kuzungaka, niseme wazi majangili wa Tembo, Chui na Simba wenyeji huingia kwa wingi wakitumia pinde, mishale na mapanga huku wakisaidiwa na mbwa.

Majangili huingia na magari na kuna wakati wanatumia bunduki kuwinda wanyama wengi kwa matumizi yao na kuna wakati wanawauzia watu wa mjini Singida, Kateshi na kadhalika.

Manjangili ambao huvamia humo pia hukata miti bila woga na huenda kuuza maeneo niliyoyataja hapo juu na zaida. Na wa viumbe wa porini, lakini sasa hivi wakulima na wafugaji wameishavamia.

Wavamizi hawaoni shida ya kuvamia maana hakuna askari wa wanyamapori, maofisa misitu wanaoishi   ndani ya pori hili wala kufanya doria. Maofisa maliasili wilaya na mkoa wao kazi yao ni kutoa vibali vya kuwinda tu wala si leseni halali.

Ujangili

Kuna ujangili wa hali ya juu sana ndani ya pori hili. Ujangili wa kitoweo kiasi kufanya viongozi wa vijiji vyote vinavyolizunguka pia kuwa na mgogoro wa mipaka kati ya Wilaya za Singida vijijini (Mkoa wa Singida) na Wilaya Chemba Mkoa wa Dodoma.

Viongozi husika wa vijiji, kata, tarafa na wilaya mpaka leo hii hawajakutana kupitia tatizo hili hatimaye mapendekezo yapelekwe kwenye vikao vya mikoa husika Dodoma na Singida vitoe uamuzi au waite wataalamu wa mpaka watakaoonesha mpaka umepita wapi ili ufumbuzi upatikane.

Wakulima na wafugaji

Kutokana na Pori la Mgori kutokuwa na ulinzi wowote, wananchi wafugaji na wakulima wamevamia pori hilo kwa ajili ya kilimo na ufugaji na baadhi yao kutoka vijiji vyote vinavyolizunguka wameamua kuanzisha makazi ya kudumu.

Pia miundombinu ya kijamii kama zahanati nakadhalika zimejengwa ndani ya pori hilo.

Mpaka

Kuna mgogoro kati ya mpaka na pori. Cha ajabu ni kwamba tangu wachaguliwe kuwa wabunge na madiwani, kila mmoja anashughulika na kata yake tu bila kuitisha mikutano ya ujirani mwema wazungumzie tatizo la mpaka na shughuli zingine za maendeleo.

Mbunge wa Singida Kaskazini

Pamoja na kwamba pori la Mgori lipo chini ya Halmashauri ya Singida Vijijini, bado ni pori ambalo halijapanda hadhi kuwa pori la akiba. Lakini, kwa uwezo aliokuwa nao Nyalandu angeweza kutekeleza jukumu hili alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Angeweza pia kutatua mgogoro wa mpaka kati ya wananchi wanaoishi kwenye vijiji hivi. Wananchi hawa hugombea ardhi na kila upande anasema hilo eneo liko wilayani kwake Singida Vijijini na Chemba hasa wa vijiji vya Mukulu wao wanadai pori lipo Chemba.

Wabunge na Madiwani

Wabunge wa maeneo haya (Chemba na Singida) Kaskazini hawajawahi kukutana kujadili tatizo hili. Ninachofahamu ni kwamba hutembelea, napo ni kwa uchache sana. Kuna mambo mengi wangevuna huko na kuweka mikakati ya kujiongezea mapato yao kutokana na asali na nta ambavyo vingefaidisha nchi kwa mapato.

Wananchi wa maeneo haya wamepata hasara kwani asali wanaitumia tu kama dawa ingawa ingeweza kuwa zao la biashara.  Baada ya kulitunza na wanyamapori kuongezeka, wananchi wangekuwa na ‘outa’ maalumu kwa ajili ya afya zao. Kikosi cha kuzuia ujangili kilichoko Manyoni hakifanyi lolote.

Nimeambiwa tu kwamba kwa sasa vikao mbalimbali vinaandaa kulifanya eneo hili kuwa na utawala yaani Wildlife Management Area (WMA).

 

Mgana Msindai, kitaaluma ni Mhifadhi kabla ya kuingia kwenye siasa. Anapatikana kupitia namba 0768 444777; 0789 444777; 0714 811831 na 0622 811831.

2379 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!