Nimefurahi kusikia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, anataka kutumbua jipu hili, lakini lazima nikiri kuwa jipu hili ni gumu kutumbulika kwa sababu linahusisha watu wengi kupitia urasimu wa utoaji vibali na suala la msingi kabisa la rushwa. 

Tanzania tumefika mahali ambako nadhani ni vema tukasema hata usalama wetu wa ndani tumeuweka rehani kwa wageni waliojazana.

Nimeona niwe muwazi kusema kuwa jipu hili kamwe haliwezi kutumbuka hadi pale tutakapoamua kumshirikisha mwenye madaraka ya juu kabisa ambaye amejitanabahisha kuwa yeye na rushwa ni alfa na omega, amejitanabahisha kuwa yeye na haki ni ndugu mmoja na kwamba haki inauma lakini inamaana katika jamii iliyoongoka.

Tanzania ni Taifa ambalo nalijua kwa uzuri wake wa kuwa kisiwa cha amani kwa muda mrefu, ni nchi ambayo naijua kwa uzalendo ambao ulitukuka katika awamu ya kwanza, ni Taifa ambalo kuna wakati miaka ya 1970 tulifika kiwango cha kuitwa ni nchi ya pili kiusalama baada ya Israel, sifa hiyo sasa haipo tena.

Nina hakika waziri wakati akitoa maagizo hayo ni kitu ambacho alikuwa anakijua vizuri juu ya tatizo la ajira kwa kuruhusu kila mwenye kuweza kuja nchini na aje afanye kazi au aajiriwe na mtu yeyote bila kuzingatia suala la usalama, kuna maana nyingi za kiusalama ambazo naweza kuwa namaanisha lakini ni vizuri nikajaribu kuzidondoa chache ili tujue tuko salama ama vipi.

Tuanze na tatizo la ajira, nchi yetu ina vijana wengi ambao kwa sasa hawana ajira na maisha yao yamekuwa ya kutangatanga kila siku kutafuta riziki yao, vijana hawa ni wahitimu wa fani mbalimbali katika masomo yao na bahati mbaya hawana ajira.

Vijana hawa siku watakaposema yatosha baada ya kusubiri mpango kazi wa kuzifungua fursa za ajira waliyosubiri kwa muda mrefu yatakayotokea ni kama yale ya Afrika Kusini, kuamua kuingia barabarani na kuwamaliza wale wote wanaoamini wanafanya kazi ambazo wao walipaswa kuzifanya, watafanya hivyo bila kufuata sheria ya ukaguzi wa nyaraka kihalali na hapo kiusalama tutakuwa tulishindwa kudhibiti hali hiyo kabla ya kutokea, hivyo kimsingi tutakuwa hatuna maono ya mbali kujua nini kitatokea katika siku za usoni.

Kuna suala la ajira ya mtaji ambayo pia ipo katika suala la ugeni wa nchi hii, kuna wageni wanaokuja wakiwa na mitaji mikubwa na kufanya biashara ambazo vijana wetu wangeweza kuzifanya, lakini kutokana na uwezo wao mdogo kifedha na mtaji, wanajikuta wao ni waajiriwa kwa maana ya vibarua na kunyanyaswa kama vile nchi hii si sehemu ya hisa yao, haya yamejidhihirisha wazi katika mahoteli, viwanda, kilimo na kadhalika.

Zipo ajira ambazo Watanzania wanajiuliza; hivi kazi hizo ni muhimu kiasi gani hata waletwe wageni kuzifanya kama hakuna kitu kinachofichwa katika kazi hizo ikiwamo kukwepa kodi, kudhulumu haki za Watanzania, kuiba maliasili zetu na mengineyo?

Idadi kubwa ya Wakenya wanaofanya kazi wanazoweza vijana wetu inatisha, wamefikia mahali wanatudharau kwa kujidharaulisha, idadi ya Wachina haisemeki na kama haitadhibitiwa baada ya muda mfupi ujao tunaweza lingana idadi na wageni, sisi Watanzania tutakuwa wageni wa nani?

Hivi sasa Wachina wanawanyanyasa sana Watanzania, wamefikia mahali wanawapiga na kuwatemea mate Watanzania, kisa mtaji au urafiki wa Nyerere na Mao? Hii ni nchi huru au bado tunatawaliwa kwa mtaji wa mtu? Hawa Wachina wanafanya kazi zote zinazoweza kufanywa na Watanzania lakini rushwa ndiyo iliyotufikisha hapa.

Naamini jambo lililotangazwa halitakuwa kuwafanya Watanzania wachache wenye dhamana kuneemeka mbele ya Mheshimiwa Magufuli, hii ni kero kubwa na iliyopitiliza, vijana wetu hawana ajira tunamleta mwekezaji pamoja na watu aliowaajiri kutoka kwake, Tanzania imegeuka kichwa cha mwenda wazimu, Tanzania imegeuka shamba la bibi watu wanafanya watakavyo, haiwezekani.

Nawashauri wenye mamlaka mtuondolee wote wanaofanya umachinga wa kazi na biashara bubu, tunaojua wanatucheka, wanatudharau, wanatutukana, wanatunyanyasa na tunaendelea kuwa watumwa ndani ya ardhi yetu.

Huko kwao haturuhusiwi kwenda, huko kwao haturusiwi kufanya biashara, huko kwao haturuhusiwi kuwekeza ajira, huko kwao hatuna sauti, huko kwao tunapigwa, huko kwao tunafukuzwa, huko kwao hata kutembea tunapangiwa, kwetu ni uhuru wa manyani, sisi twende wapi sasa.

Sasa hivi wamefikia mahali wanajihusisha na masuala ya siasa, sitashangaa hata kidogo kusikia siku moja tuna diwani au mbunge Mkenya, Mrundi, Mnyarwanda, Mchina, Msouth Afrika, Myemen, Mturuki, Mwingereza, Mrusi na yeyote. Tayari baadhi wana nyadhifa serikalini kila siku tunasikia katika vyombo vya habari, usalama wetu uko wapi.

Wanaohusika wakishindwa kwa sababu ya mlungula basi tutakuomba mdau wa kweli, kweli kabisa tuliokuchagua na ukachagulika na wachaguaji wakikuamini uanze kuwatumbua viongozi wako kuanzia uhamiaji hadi wanakochakata vikatolewa vibali vya kucheza na nchi yetu.

Tumechoka na hili ni jipu nafuu ya bandari na TRA.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.

1461 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!