Wanyama albino wazua gumzo

*Pundamilia, nyati, twiga albino waonekana Tarangire, Katavi

*Wananchi wafurahi, wadhani ni kivutio kipya cha utalii

*Wataalamu wapinga, wadai kuna tatizo kubwa na la hatari

MARA

Na Anthony Mayunga

Nyati mweupe ameonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kuwa kivutio kwa wengi, wakidhani kuwa ni aina mpya ya wanyama inayopatikana eneo hilo pekee.

JAMHURI linafahamu kuwa wanyama kama twiga na pundamilia wenye rangi tofauti na ile ya asili wamewahi kuonekana katika maeneo mengine nchini, ikiwamo Hifadhi ya Taifa ya Katavi na kutangazwa kama kivutio.

Hata hivyo dhana kwamba mnyama kuwa na rangi tofauti na ile ya asili ni kivutio cha utalii, inapingwa na wataalamu wa wanyamapori wakisema huo ni ualbino.

Sababu za ualbino kwa wanyama

Uvamizi wa shoroba (corridor au mapito ya wanyama kutoka eneo moja hadi jingine) unatajwa kuchangia baadhi ya wanyamapori kuzaliwa na ualbino huku tembo wakizaliwa bila kuwa na meno.

Tafiti za awali zinadai kwamba hali hiyo huchangiwa na wanyama husika kulazimika kupandana ‘ndugu’ wa familia moja kinyume cha mfumo wa maisha yao.

Hifadhi ya Tarangire ilipoanzishwa mwaka 1970 kulikuwa na shoroba tisa za mapito ya wanyamapori kutoka eneo moja kwenda jingine ambazo kwa sasa zimevamiwa na kusalia chini ya tatu tu.

“Shoroba nyingine zote za Tarangire zimevamiwa na watu kwa ajili ya makazi, taasisi za umma zimejenga ofisi, vituo vya afya, shule na huduma nyingine,” anasema mdau mmoja wa utalii na wanyamapori.

Ofisa kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Revocatus Meney, anasema athari za kuzibwa shoroba zinaongezeka ukubwa na kusababisha kuzaliana kaka na dada.

“Wale wanyama dhaifu ndio hupata ualbino huku tembo wakizaliwa bila meno. Tembo huishi kifamilia, hawatakiwi kupandana wao kwa kwao.

“Hawa inapofika kipindi cha uzazi, harufu husambaa kilometa 20 kwa kuwa wana uwezo wa kunusa umbali huo, hivyo madume huifuatilia; yakifika hupigana na anayeshinda ndiye humpanda jike.

“Lakini sasa shoroba zimevamiwa, madume yanashindwa kutoka maeneo yao kufuata majike na badala yake wanaingiliana kifamilia, matokeo yake wanazaliwa wanyama wasiokuwa na meno na albino ambao wameonekana Tarangire na Mwiba,” amesema.

Amesema hilo ni tatizo la muda mrefu na halipaswi kuachwa liendelee kwa kuwa athari zinazidi kuwa kubwa kiuhifadhi huku tembo wakubwa wenye meno makubwa wanazidi kupungua na kupoteza sifa tuliyonayo kimataifa.

“Hata kwa binadamu haiwezekani kaka na dada kuoana kwa kuwa kitaalamu kunaweza kutengeneza tatizo jingine ndani ya ukoo. Kuzibwa kwa shoroba kunawafanya wanyama wakose mtawanyiko kutoka hifadhi moja kwenda nyingine na kupata wachumba wa kuoana nao,” amesema Meney.

Mkurugenzi wa TAWIRI wa Serengeti, Dk. Emmanuel Masenga, anaunga mkono kauli ya Meney, akisema matokeo ya muda mrefu ya uvamizi wa shoroba yanaanza kuonekana.

“Zamani tembo wa Serengeti walikuwa wakienda mpaka Tarangire. Leo haiwezekani na tunaanza kuziona athari zake,” amesema Dk. Meney.

Utafiti mpya waanza kufanyika

Kuhusu kuonekana kwa nyati dume na jike wenye rangi nyeupe Tarangire, mtafiti mstaafu wa wanyamapori, Dk. Robert Fyumagwa, anasema:

“Huenda sababu zikawa hizo zilizosemwa awali au hata nyingine. Kuna utafiti unaendelea kwa sasa kujua undani wake, ngoja wamalize watakuja na taarifa halisi,” amesema.

Mmoja wa wahifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya Serengeti (jina tunalihifadhi), amesema zaidi ya asilimia 60 ya simba wanaishi na kuzaliana nje ya maeneo yaliyohifadhiwa kutokana na uvamizi wa shoroba.

“Katika mazingira kama hayo wanyama hao na wengine licha ya athari za uzazi wao kuharibiwa, lakini pia wanaendelea kupungua kwa kuwa wanauawa kwa urahisi hasa wanapokula mifugo na mazao ya wavamizi wa shoroba. Kwa hakika kunatakiwa kuchukuliwa hatua madhubuti kunusuru hali hii,” amesema.

Amesema uhamaji wa wanyama kutoka eneo moja hadi jingine husaidia kuhamisha vinasaba vinavyoleta ukuaji mzuri na endelevu, ikiwamo kuondoa kuzaliana ndugu kwa ndugu kunakosababisha kupatikana vinasaba hafifu na uwezekano wa kutoweka kabisa aina fulani ya wanyama.

“Wakati wanyama wakihama huku na kule kupitia hizo shoroba, mbali na kuzaliana, pia huwawezesha kutafuta madini maalumu yanayoimarisha afya yao,” amesema.

JAMHURI ina taarifa kuwa miongoni mwa shoroba zilizovamiwa kwa wingi ni ikolojia ya hifadhi za taifa za Tarangire na Manyara.

Shoroba nyingine ni ya Tarangire inayounganisha mapori ya Tarangire, Loikisale, Emboret, Mkungunero na Simanjiro ambako wanyama huzaliana.

Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI uliothibitishwa na Ofisa Maliasili wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Michael Gwandu, unaonyesha kuwa kaya zaidi ya 30 zinaishi ndani ya eneo la Ikolojia ya Tarangire na Manyara na kuathiri mzunguko wa kawaida wa wanyamapori.

“Uhakiki wa eneo hili umebainisha ukweli huu wa kusikitisha. Kaya zinaishi katika shoroba na kuzibwa kwake kuna athari nyingi. Mbali na hili la kuzaliana ndugu, kuna uwezekano wa kusababisha mlipuko wa magonjwa,” amesema Gwandu.

Ikolojia hii huwapa nafasi wanyama kuzunguka kati ya Tarangire, Manyara, Ngorongoro, mapori ya akiba ya Mkungunero na maeneo mengine yaliyohifadhiwa.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa TAWA Kanda ya Kaskazini, Peter Mbanyoko, anakiri kuwa kuzibwa kwa shoroba kuna athari kubwa na kunachochea ujangili.

Faida, athari za wanyama albino

Mtaalamu mmoja wa wanyamapori kutoka TANAPA anasema wanyama albino huwavutia watu mbalimbali kwenda kuwaangalia kutokana na tofauti iliyopo kati yao na wengine.

“Hawa huwa maarufu sana kwa kuwa kesi zao ni chache. Inadaiwa katika mamalia, kila watoto 10,000 inaweza kutokea kesi moja na inapotokea taarifa zake huenea haraka kama hii ya Tarangire,” amesema.

Hata hivyo utofauti huu husababisha kuuawa haraka kwa kuwa inakuwa rahisi kuwindwa na wanyama wala nyama kwani huonekana kwa urahisi huku wakiwa katika uwezekano wa kupata magonjwa kama kansa ya ngozi kwa urahisi.

Utalii huchangia zaidi ya asilimia 17 ya pato la taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni, kwa maana hiyo wadau wanaiomba serikali kuchukua hatua madhubuti kuzizibua shoroba zilizovamiwa ili kuwawezesha wanyama kuwa na mtawanyiko, vinginevyo umaarufu wa Tanzania kimataifa utatoweka.