Wananchi na watumiaji wa bia wamelalamikia hatua ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupandisha bei ya bia kabla hata bajeti ya Serikali haijapitishwa.

Tangu Aprili 1, 2016 bei za bia zimepanda kutoka wastani wa Sh 2,300 na kufikia 2,500, huku uongozi wa TBL ukitumia kigezo cha kuongezeka gharama za uendeshaji kupandisha bei ya bia.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya TBL, zinaonyesha kuwa mpango wa kupandisha bei ya bia umelenga kuitishia Serikali isiongeze kodi kwenye bia katika bajeti ijayo.

“Hawa watu mwaka jana walifanikiwa kuitisha Serikali kuwa bia zikiongezewa kodi mauzo yatashuka kwani gharama itakwenda juu mno. Serikali haikuwaongezea kodi, lakini wao Julai 16 na Novemba 22, waliongeza bei ya bia zao.

“Tulishuhudia bei ya bia inaongezeka na kufikia Sh 2,300. Mwaka huu wanafanya mbinu kuishinikiza Serikali isiwaongezee kodi, tena wana mpango wa kuishawishi Serikali kuwa badala ya kuwatoza kodi kwa chupa kama inavyofanya sasa, ibadilishe iwape kiwango kama ni bilioni 80 au 200 kwa mwaka, basi walipe hizo kama ushuru,” kimesema chanzo chetu kutoka ndani ya TBL.

Chanzo hicho kimesema ikiwa Serikali itaingia mkenge na kukubaliana na mpango wa TBL, basi wajue bia zitauzwa kreti nyingi mno na Serikali itapata fedha kidogo.

“Kwa kawaida bia hazipaswi kuongezeka bei katikati ya mwaka au kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha maana gharama za uendeshaji zinakuwa zile zile, sasa najiuliza hawa jamaa leo (Ijumaa wiki iliyopita) wamekuwaje kutuongezea bei? Nimekunywa bia mbili hapa, natoa noti ya 5,000 naambiwa hakuna chenji, hii haikubaliki Mura,” Mwita Magambo aliliambia JAMHURI, akiwa katika baa za eneo la Banana Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Tangazo la TBL, bia za Safari, Kilimajaro, Castel Lager na Peroni sasa zimepanda bei na kuwa Sh 2,500 huku nyingine zikiuzwa kuanzia Sh 1,300 kama Eagle Lager.

 Uongozi wa juu wa TBL hata ulipotafutwa kuzungumzia hatua hii inayodaiwa kuwa ni mtego kwa Serikali hakuwa tayari kuzungumza na JAMHURI, zaidi ya wasaidizi wao kusema hawakuwa na nafasi ya kuzungumza.

JAMHURI halikupata fursa ya kuzungumza na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya watendaji wakuu kuwa kwenye vikao vya bajeti inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni mwezi huu.

Hata hivyo, Afisa mmoja kutoka Wizara ya Fedha, ameliambia JAMHURI kuwa mpango wa kulipishwa kodi kwa kukadiriwa ulioombwa na TBL umegonga mwamba na Serikali imeona bora iendelee na utaratibu wa kutoza kila chupa inayozalishwa.

“Kwani wasiwasi wao ni nini? Sisi hatuwatozi kwa chochote ambacho hawakuzalisha. Sasa tunasema wakizalisha kidogo, tutawatoza hicho hicho kidogo, wakizalisha kingi utozaji nao utakuwa mkubwa. Wasiwe na wasiwasi,” afisa huyo aliyesema si msemaji ameliambia JAMHURI.

 Hata hivyo, zipo taarifa za wazi kuwa ingawa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Bia Tanzania, Waziri Mkuu (mstaafu), David Msuya ametofautiana na Mkurugenzi Mkuu, Roberto Jarrin kwa kuonyesha kuwa mauzo yameshuka kwa asilimia 6.5, huku Jarrin akisema yameshuka kwa asilimia 4, bado TBL wamepata faida kubwa.

 “Kati ya bilioni 380 walizopata kabla ya kodi, walipaswa kupata faida kubwa zaidi, ila mikataba waliyoingia ya kulipa tozo zisizo na kichwa wala miguu ndizo zinatafuna fedha za TBL. Hata wakiongeza bei ya bia hadi mbinguni, kama hawajasitisha mikataba kama ya Baveman Services, kampuni haiwezi kuwa na mapato ya uhakika,” kilisema chanzo chetu.

 

 Utafiti uliofanywa na ActionAid

 Wiki iliyopita, tulikuletea sehemu ya utafiti uliofanywa na Shirika la ActionAid la Uingereza juu ya Kampuni ya SABmiller inayoimiliki TBL ukionyesha jinsi kampuni hiyo inavyochepusha mapato ya kampuni zilizoko Afrika na Asia, katika gazeti la leo, tunakuletea mwendelezo wa uchunguzi huo.

 

Nani anapata na nani anapoteza

 Kampuni zinazomilikiwa na SABmiller kutoka Afrika na Asia ni nyingi. Wakati huo huo baadhi ya kampuni zinamilikiwa na wazawa kwa mfano Kampuni ya Bia ya Ghana inamilikiwa na Mfuko wa Pensheni, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na Shirika la Bima kwa asilimia 11.

SABmiller inasema nje ya Afrika Kusini, kampuni zake zote zina wabia wenyeji na wenye hisa wachache zikiwamo Serikali, wakala wa Uwekezaji ambazo zinaelezwa na kukubaliwa na mfumo wa umiliki ununuzi na mikataba ya uendeshaji.

Lakini fedha inapotoka, Kiwanda cha Bia cha Accra au kampuni nyingine tanzu ya Afrika kwenda kwenye kampuni nyingine zenye pepo ya kodi ambako wanahisa hawana hisa, basi wanahisa hao hupoteza.

ActionAid inakisia kwamba malipo yanayokwenda katika nchi zenye pepo ya kodi huigharimu Ghana kati ya pauni 440,000 na  milioni 1.1 kwa mwaka ikiwa ni gawio lililopotea.

Hivi karibuni SABmiller imewanunua wanahisa wadogo ambao bila shaka wamekatishwa tamaa na faida inayopungua kutokana na malipo yanayofanywa na kampuni za nje ya nchi.

Kampuni ya huduma za fedha ya Ghana iitwayo Data Bank inasema wanahisa wenye hisa chache wanaweza kujisikia vibaya kutokana na malipo wanayopewa.

 

Bei linganishi zina umuhimu kwa Ghana?

Kodi ya Ghana ipatayo pauni milioni 284 inayotokana na kampuni 365 ambazo ni walipa kodi wakubwa na nyingi kati ya hizo ni kampuni za kimataifa.

Idara yake ya walipa kodi wakubwa na wafanyakazi 52 tu wanaofanyia kazi mashirika hayo 365 ambapo wachache mno hufanya ukaguzi wa kodi.

Tatizo la msingi la idara hii, haina uwezo wa kufuatilia mbinu zilizojadiliwa katika ripoti hii zinazotumika kuhamisha faida. Tatizo hili ni kubwa na lilibainishwa katika mkutano wa Jukwaa la Walipa kodi Afrika jijini Pretoria.

Ambako katika tamko lake lilisema: “kutoza kodi biashara ya kimataifa, hasa hasa bei linganishi linaendelea kuwa suala gumu.”

 Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Ghana (GRA), katika hili anasema: “Bei linganishi ni tatizo katika nchi zinazoendelea.”

Maafisa wengine waandamizi waliozungumza na ActionAid walikubaliana hili ni tatizo kubwa na mmoja akahoji kwanini nchi zinaendelea kuwekeza katika biashara isiyo na faida sehemu nyingine?

“Kampuni zinatengeneza hasara miaka mitano au 10, lakini bado zinaendelea kufanya uwekezaji. Swali ni je, nini kinazivutia? Ni jambo tunalolifahamu, lakini hatuna uwezo.”

Chini ya sharia ya Ghana, kampuni haiwezi kulipa mrahaba au tozo ya usimamizi kwa kampuni inayohusiana nayo nje ya nchi bila mkataba rasmi kati yake na kampuni mbili zinazopaswa kuwa zimesajiliwa na Baraza la Uwekezaji la Ghana (GIPC).

Benki Kuu ya Ghana haiwezi kuruhusu uhamishaji wa malipo bila vielelezo sahihi kutoka GIPC.

Mkataba unaeleza kiasi kinachoweza kulipwa na kinapaswa kubaki katika mipaka ya kisheria, tozo ya usimamizi kwa mfano haiwezi kuzidi asilimia tano ya mzunguko wa fedha za kampuni.

GIPC inaruhusu kampuni kuhamisha fedha, lakini afisa mmoja alituambia: “Mara nyingi hakuna malipo yanayofanyika.”

Yanapofanyika malipo, kuthibitisha kwamba bei linganishi ilikuwa sahihi inakuwa tatizo. Na afisa huyo anasema si kamba hawafahamu bali huwezi kueleza kwa usahihi kama ni bei linganishi au la.

Mmoja wa Wakurugenzi, kutoka Kampuni za Uhasibu anasema tozo zinazotozwa haziwezi GIPC imekwisha zipitisha.

 

Kuimarisha bei linganishi

 Kuna vizingiti kadhaa katika kutekeleza suala la kanuni la bei linganishi nchini Ghana.

Kwanza, kwa sasa Ghana ina sharia ya ukurasa mmoja juu ya bei linganishi inayotajwa na afisa mwenye jukumu la kusimamia kuwa ni la kijumlajumla na haina mwelekeo.

Ingawa sharia inawapa mamlaka GRA kurekebisha kiwango cha faida kinachopaswa kutozwa kodi iwapo kanuni ya bei linganishi katika biashara ya kimataifa ingefuata, inategemea utashi wa kamishna mkuu wa GRA kisheria.

Kwa uzoefu mdogo na kutokuwa na sheria yenye kuongoza kwa asili, maafisa hawatumii haki hii kwa usahihi.

Pili, wanakosa taarifa. Sehemu ambayo kuna malipo yanastahili kufanywa kwenye kampuni, inakuwapo uhamishaji wa faida. Hivyo watoza kodi wamefungwa mikono kwa kutokuwa na taarifa sahihi.

Nchi nyingi zilizoendelea hupambana na tatizo hili kwa kulazimisha uwapo wa kumbukumbu za kila malipo zikilinganisha na washindani wao wanatoza bei kiasi gani.

Kumbukumbu hizo huonyesha aina ya malipo, sababu za malipo, asili ya bei linganishi na jinsi gani hesabu ilivyopigwa kufikia bei hiyo.

Kanuni mpya za bei linganishi ambazo kwa sasa zinaanza kuandaliwa zikiwa na matakwa ya kutunza kumbukumbu katika sharia mpya zitasaidia, lakini hata hivyo mapato yatakumbana na kikwazo cha tatu, utaalamu mkubwa walionao kampuni za kimataifa katika masuala ya kodi ukilinganishwa na idara za kodi na wakaguzi wa nchi zinazoendelea.

GRA haina hata mtaalamu wa bei linganishi wala idara ya bei linganishi. 

Kundi la wataalamu wa maafisa wa kodi wa Ghana limekuwa nchini Uingereza, wakijifunza katika mitaala ya kodi ya taifa na ushuru, lakini Mamlaka ya Kodi Ghana inasema inahitaji utaalamu zaidi juu ya suala la kodi linganishi.

 

Je, unajua ni kiasi gani nchi za Afrika zinapoteza kwa SABmiller kuchepusha faida kwenda kwa kampuni zake tanzu? Usikose JAMHURI wiki ijayo.

2707 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!