Kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa imezidi kuinogesha Tanzania katika ulimwengu wa soka kiasi cha kuongeza ushindani miongoni mwa timu kubwa hapa nchini.

Hii ni kampuni ya michezo ya kubahatisha ambayo imepata kutoa udhamini kwa timu kadhaa hapa nchini, ambazo ni pamoja na Yanga, Simba, Mbao na Singida United.

Safari hii, miongoni mwa timu hizo kubwa zilizopata kuwa chini ya ufadhili wa SportPesa, Simba ndiyo yenye manufaa zaidi ikitarajia kucheza mchezo wa kimataifa na timu maarufu ya Sevilla.

Hivi karibuni uongozi wa SportPesa umethibitisha kwamba timu hiyo ya Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania itakuja kucheza na timu ya Simba SC ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania.

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Uwanja wa Taifa Mei 23, mwaka huu. Sevilla watakuja kuchuana na timu ya Simba SC huku rekodi yao Ulaya ikibainisha kuwa ndiyo timu yenye mataji mengi katika michuano ya Europa baada ya kutwaa taji hilo mara tano.

Michuano ya Europa ndiyo michuano ya pili kwa ukubwa barani Ulaya kwa upande wa klabu, baada ya michuano ya Klabu Bingwa (UEFA Champions League).

Timu ya Sevilla imetwaa mataji ya Europa mwaka 2006 na 2007. Vilevile mwaka 2014, 2015 na 2016, ilitwaa taji la Europa mara tatu mfululizo – maarufu kama ‘back to back’.

Ukiachana na michuano ya Europa, hata katika Ligi Kuu ya Hispania, maarufu kama Laliga, Sevilla wametwaa taji hilo la ligi hiyo miaka takriban 74 iliyopita, yaani msimu wa 1945/1946.

Vilevile rekodi zinawaonyesha mwaka 2006 walitwaa Kombe la UEFA Super Cup, pia wakishikilia mataji matano ya Spanish Cup katika kabati lao la makombe.

Katika Laliga msimu huu kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo walikuwa wakishikilia nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania.

Kuhusu mfumo wa uchezaji, Sevilla ni ‘waumini’ wa kucheza soka au kandanda la kupiga pasi nyingi kama timu zingine za Hispania zinavyocheza.

Kikosi cha Sevilla kinaundwa na wachezaji wengi mahiri, lakini Wissam Ben Yedder ndiye mchezaji tishio katika timu ya Sevilla baada ya kupachika magoli 17 katika msimu huu.

Wachezaji wengine tishio katika timu hiyo ni Pablo Sarabia, Andre Silva, Ever Banega na Munir El Haddadi.

Kwa upande mwingine, timu ya Simba imeonekana kuwapo katika kiwango cha kuridhisha kumudu kucheza na mabingwa hao wa zamani wa Europa, Sevilla, kutokana na kufanya vizuri katika michuano ya SportPesa iliyofanyika mwanzoni mwa mwaka huu na kufanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems, si mgeni wa mpira wa Ulaya. Kocha huyu ni mzaliwa wa Ubelgiji na kwa mantiki hiyo, wapenzi wa soka na mashabiki wa timu ya Simba SC wanatarajia kushuhudia soka lenye ushindani kati ya timu hizo.

Ukiachilia mbali Sevilla kuwa na nyota tishio kwa klabu nchini Hispania na Ulaya, Simba kwa sasa inatajwa kuwa na wachezaji wenye uwezo, wenye kuleta matumaini dimbani. Wachezaji kama Emmanuel Okwi na Juuko Murshid ambao wamekwisha kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika.

Wengine katika orodha ya wakali wa Simba ni Meddie Kagere na Clatos Chama. Ikumbukwe kwamba Sevilla si timu ya kwanza kuja kucheza nchini kwa udhamini wa SportPesa. Mwaka 2017 timu ya Everton iliwasili nchini kucheza na bingwa wa SportPesa kwa wakati huo, timu ya Gor Mahia kutoka nchini Kenya. Gor Mahia ilitwaa nafasi ya kucheza na Everton baada ya kuibuka kidedea katika michuano ya SportPesa iliyoshindanisha baadhi ya timu za Afrika Mashariki.

Please follow and like us:
Pin Share