Na Mwandishi Wetu- Jeshi la Polisi

Maafisa Habari wa Jeshi la Polisi Nchini wametakiwa kutumia kalamu zao vizuri ili kuwaelimisha Wananchi mbinu mbalimbali za kubaini na kutanzua uhalifu hapa Nchini.

Hayo yamesemwa Agosti 21, 2023 Jijini Mwanza na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP )David Misime wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa Maafisa habari wa Jeshi hilo kutoka Makao Makuu ya Polisi na baadhi ya Mikoa ya Tanzania yenye lengo la kuwajengea uwezo katika kufanya kazi zao za kila siku.

Miseme alisema Maafisa hao wanapaswa kutambua umuhimu wao katika jamii na kutumia vyema kalamu zao kwa kutangaza kazi mbalimbali zinazofanywa na Jeshi hilo ambazo lengo lake ni kubaini na kuzuia uhalifu.
“Ushirikiano baina ya Wananchi na Polisi umeongezeka kupitia mradi wa Mkaguzi wa Kata hivyo ninyi ndio wenye jukumu la kuuhabarisha umma haya mazuri ambayo yanafanyika katika mikoa yenu” Alisema Misime.

Aliongeza kuwa katika mafunzo hayo Maafisa habari wa Jeshi la Polisi watapata muda wa kujifunza mambo mengi ikiwemo namna ya kuandika habari na makala, upigaji wa picha za kihabari, itifaki na ustarabu pamoja na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii katika kutangaza mafanikio mbalimbali ya kazi za Polisi na miradi ya Polisi jamii ukiwemo mradi wa Polisi Kata.

Kwa Upande wake Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Gidion Msuya alisema mafunzo hayo yamefanyika katika kipindi kizuri ambapo Jeshi hilo limejikita katika kufanya kazi Kidijitali na Maafisa hao ndio wenye jukumu kubwa la kuwafahamisha Wananachi mabadiliko na maendeleo ya utendaji wa Jeshi la Polisi.

Mafunzo hayo ambayo ni utekelezaji wa Mpango kazi wa Jeshi la Polisi yanafanyika kwa awamu ya pili yakiwa yamehusisha Maafisa Habari kutoka Makao Makuu ya Polisi, Mkoa wa Kigoma, Geita, Mwanza, Kagera, Katavi, Shinyanga, Tabora, Simiyu, Iringa, Mara na Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya.

Please follow and like us:
Pin Share