Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia Mei 15 ,2024 taarifa ya hali ya Ukatili wa Watoto Mtandaoni (Disrupting Harm Report in Tanzania 2022) ya utafiti wa Serikali na UNICEF inaonesha katika nchi zote Duniani, watoto na vijana balehe wanaongoza kwa utumiaji wa simu za mkononi, kompyuta na runinga ambapo kwa Tanzania asilimia 67 ya watoto wa umri wa miaka 12 hadi 17 ni watumiaji wa simu na intaneti.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ameeleza hayo leo Aprili 18,2024 jijini Dodoma na kufafanua kuwa taarifa ya utafiti huo ilibainisha kuwa, kundi hilo hutumia zaidi simu za ndugu zao wa karibu wakiwemo wazazi, walezi, marafiki na ndugu wengine wanaowazunguka.

Amesema utafiti wa hali ya Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria nchini ya mwaka 2022 umebainisha kuwa, mifarakano na migogoro katika familia imesababisha malezi duni na uangalizi hafifu wa watoto hususan watoto wa kike iliyopelekea watoto hao kuanza ngono katika umri mdogo jambo ambalo limesababisha mimba za utotoni kuendelea kuwepo kwa kiwango kikubwa.

“Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 22 ya watoto wenye umri wa miaka 15 – 19 walipata ujauzito ikilinganishwa na asilimia 27 ya watoto wa umri huo kwa mwaka 2015/16,aidha kiwango cha mimba za utotoni vijijini ni kikubwa zaidi kwa 25% ikilinganishwa na mijini kwa 16%. Kiwango hicho kinapungua lakini bado ni kiwango kikubwa kwa watoto, ” amesema Dkt, Gwajima.

Pia amesema, taarifa hiyo inaeleza kuwa asilimia 4 ya watoto waliotumia mitandao walifanyiwa aina mojawapo ya ukatili mtandaoni ikiwemo kulazimishwa kujihusisha na vitendo vya kingono, kusambaza picha na video zenye maudhui ya kingono bila ridhaa yao, na kurubuniwa kujihusisha na shughuli za kingono kwa kuahidiwa fedha au zawadi zingine.

Aidha ukatili dhidi ya watoto na ukatili wa kijinsia katika familia umechangia kuongezeka kwa migogoro ya kifamilia hususan kati ya wenza au wanandoa jambo lenye athari kubwa katika malezi na ustawi wa watoto wa familia na jamii kwa ujumla.

Mfano, “Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wengi wamekimbia familia zao kutokana na migogoro ya wenza au wanandoa ambapo Taarifa ya utafiti inaonesha asilimia 27 ya wanawake wa umri wa miaka 15 hadi 49 walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili huku asilimia 12 ya wanawake wa umri huo walifanyiwa ukatili wa kingono, ” amesema.

Na kuongeza “Asilimia 13 ya wanawake waliowahi kuwa na mume au mtu mwenye mahusiano katika kipindi cha miezi 12 kabla ya utafiti huo walifanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili, kingono na kihisia. Unyanyasaji wa kimwili, kingono, au kihisia miongoni mwa wanawake walioolewa umepungua kutoka 50% mwaka 2015/16 hadi 39% mwaka 2022/23, ” amesema Dkt Gwajima.

Hata hivyo Wizara imeendelea kuratibu huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia kupitia Baraza la Usuluhishi wa Ndoa la Kamishna wa Ustawi wa Jamii lililopo Makao Makuu ya Wizara, Mabaraza ya Kata na Mabaraza ya Jumuiya.

Amebanisha kuwa, kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 jumla ya mashauri 14,600 yalishughulikiwa ambapo, yaliyohusu migogoro ya ndoa yalikuwa 5,306 (asilimia 36), yaliyohusu migogoro ya kifamilia na matunzo ya Watoto 5,944 (asilimian41), yaliyohusu matunzo ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa yalikuwa 3,350 (asilimia 23).

Aidha, mashauri 3,411 yalifikishwa kwa Maafisa Ustawi wa Jamii ambapo 1,642 yalipatiwa ufumbuzi na 443 yanaendelea kufanyiwa kazi huku mashauri 1,326 yalipewa rufaa kwenda kwenye vyombo mbalimbali vya usuluhishi ikiwemo mahakama (921) na mabaraza ya kata na jumuiya (405).

“Moja ya vikwazo katika kukabiliana na migogoro ya familia ni kukosekana kwa upendo, ustahimilivu na kutokuwa na hofu ya Mungu miongoni mwa wanafamilia, mifumo kandamizi inayoendelea katika Jamii inayochochewa na mila na desturi za baadhi ya makabila hapa nchini zimesababisha wanandoa hasa wanawake kukaa kimya bila kujadiliana na kumaliza tofauti zao jambo linaloweza kuwa na athari kubwa, ” amesema Dkt, Gwajima.

Na kuongeza ” Mara zote waathirika wakubwa huwa ni watoto Vikwazo vingine ni uelewa mdogo kuhusu malezi chanya na mawasiliano duni miongoni mwa wanafamilia pamoja na wazazi kutotimiza majukumu yao ya msingi ya malezi na changamoto hizi zimechochea mmomonyoko wa maadili miongoni mwa watoto na vitendo vyenye athari kwa watoto mathalani; kujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo vinavyosababisha ongezeko la maambukizi ya VVU kwa kundi la watoto na vijana balehe, ” amesema.

Katika kuimarisha uwezo wa wazazi au walezi kwenye malezi chanya ya watoto, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuelimisha wazazi au walezi na jamii kuhusu malezi bora ya watoto sambamba na kuhimiza wajibu wa wazazi au walezi katika malezi na matunzo ya watoto na familia mathalani;

katika kipindi cha Julai 2023 na Aprili 2024, Wizara na Wadau wake kupitia Mwongozo wa Taifa wa Wajibu wa Wazazi na Walezi Katika Malezi ya Watoto na Familia imeendelea kutoa elimu ya malezi chanya kwa jamii kupitia redio na runinga, mikutano ya wazi na makongamano yanayohusisha wananchi na mitandao ya kijamii.

Aidha, kupitia viongozi wa dini, elimu hiyo imeendelea kutolewa ambapo, jumla ya viongozi wa dini 191 walipatiwa mafunzo kuhusu malezi chanya ya watoto huku waumini 35,520 wakipata elimu hiyo kwa njia ya mihadhara na mahubiri katika nyumba za ibada.

Wito wangu kwa viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu ya malezi chanya ya watoto na familia na kusisitiza kuimarisha mahusiano katika ndoa ili kuendelea kutoa huduma bora za malezi ya watoto.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, Wizara inashauri Mikoa na Halmashauri kuandaa mijadala katika Jamii kwa kutumia wataalamu wa malezi chanya ya watoto na familia, kuhusisha viongozi wa Dini kwenye kutafuta ufumbuzi wa changamoto za familia na malezi duni ya watoto sambamba na mmomonyoko wa maadili tunaoushuhudia katika jamii.

By Jamhuri