Kuanguka kwa zama za ukoloni na ukoloni
mkongwe kumetoa nafasi kwa ukoloni
mamboleo na ubeberu kutamalaki Afrika.
Watoto wa Afrika hatuna budi kuona kwa
undani mifumo miwili hii inayotamalaki
inakatishwa na kufutwa.
Watoto wale (waliopita) wa Afrika waliona
athari na madhara ya ukoloni na ukoloni
mkongwe. Wakaung’oa. Leo Afrika iko huru.
Je, watoto hawa (sisi) wa Afrika wanaona
athari na madhara ya ukoloni mamboleo na
ubeberu unavyoyumbisha siasa, unavyoua
utamaduni na unavyodidimiza uchumi wa
Afrika?
Tukumbuke kikomo cha ubepari ni ubeberu.
Ubeberu ni ubepari uliokomaa na kuvuka
mipaka ya nchi yake na kuingia nchi
nyingine kwa madhumuni ya kuunyonya
uchumi wa nchi hizo. Nchi za Afrika ndizo

hasa zinazolengwa kwa sababu ya utajiri
wa rasilimali zake kedekede.
Ukoloni mamboleo ni mfumo wenye mbinu
mpya: za kisasa katika kunyonya mali za
nchi nyingine kupitia mikondo ya siasa,
utamaduni na hata mkondo wa haki za
binadamu. Mabeberu wanaweka mitaji yao
na kutaja vivutio vizuri vikiwamo misaada,
tiba, teknolojia n.k katika maendeleo ya
kiuchumi.
Kinachofanyika katika kulea mifumo hii ni
kuanzisha istilahi mpya za kisiasa na
kibiashara ( uchumi ) kama vile utandawazi,
ubinafsishaji, ufadhilishaji, uwekezaji n.k.
Mkazo mkubwa unawekwa katika kutumia
sayansi na teknolojia.
Istilahi hizi na nyinginezo katika maendeleo
ya kiuchumi, kisiasa au kitamaduni, hazina
budi kuonwa na kuangaliwa kwa umakini na
watoto wa Afrika, tunapopokea urafiki,
ufadhili au uhisani kutoka nje ya Bara letu la
Afrika.
Natambua dunia leo ni kama kifuu cha nazi.
Ni ndogo na imeenea kiganjani mwako.
Mambo haya hayakwepeki kuyasikia,
kuyaona wala kuyakabili. Nasisitiza tu

hadhari kubwa inahitajika katika kupokea na
kutekeleza misaada ya maendeleo ya
kiuchumi, kisiasa na kitamaduni.
Hivi leo unaweza kusema ‘Media’ ndiyo
inayoendesha dunia kupitia redio, runinga,
magazeti, mitandao ya kijamii, simu na
kadhalika ndani ya sekta ya Habari na
Mawasiliano. Mifumo na istilahi nilizotaja
zinapata umaarufu na ustawi mbele ya
mataifa, hata kuwezesha matumizi
ya‘Media’ kuwa kubwa kwa wanamataifa.
Baadhi ya viongozi, wanasiasa, wananchi
na hata wanasheria wanadhani
kutumia ‘Media’ kutoa madukuduku na
malalamiko ya taasisi zao au mawazo yao
ya migongano ndiyo njia bora ya kupata
suluhisho la matatizo yao. Badala ya
kutumia na kufuata taratibu za kisheria na
vyombo vyake vya mazungumzo
vilivyokubaliwa na kuwekwa katika jamii
husika.
Watoto wa mabara mengine wameona
mwanya huo na wanaotumia katika
kuendeleza ubeberu na ukoloni mamboleo,
kwa kutumia maneno matamu ya faraja
kusaidia kupata maendeleo Afrika.

Wakati watoto wa Afrika wanalumbana
kisiasa, kisheria na kimasilahi, watoto wa
mabara mengine wanaendelea kuchukua
mali za Afrika huku wakichochea
malumbano kisirisiri.
Watoto wa Afrika tuzinduke. Tuangalie
rasilimali zetu na tuone tulivyonavyo. Na vipi
tutahifadhi, tutatunza na tutatumia kwa
masilahi na faida yetu. Tuone na tuangalie
msemo huu: “Ni kweli chao ni chetu na
chetu ni chao au chetu ni chao na chao ni
chao?” Tafakari.

Mwisho

Please follow and like us:
Pin Share