Watu 13 wakamatwa Shinyanga kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya TANESCO

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limewakamata watu 13 wakituhumiwa kuhujumu na kuharibu miundo mbinu ya Shirika la Umeme (TANESCO ) na kulisababishia hasala zaidi ya shilingi milioni 10 kati yao wamo watumishi wawili na wachungaji wa dini wawili.

Kwa mjibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Shinyanga,ACP Janeth Magomi kwa waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita alisema wanatuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati mbalimbali wilayani Kahama.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Shinyanga ACP Janeth Magomi akionyesha vifaa vya Shirika la umeme Tanzania (TANESCO)  vilivyokamatwa kwenye oparesheni iliyofanywa kwa pamoja polisi na shirika hilo kwa wanaohujumu miundombinu na wateja waliounganishiwa umeme kinyume cha utaratibu kulia ni kaimu meneja wa Tanesco wa wilaya ya Kahama Mhandisi Tumaini Chonya , Picha na Patrick Mabula,

Kamanda Magomi amesema Tanesco kwa kushirikiana na njeshi la polisi lilifanya lilifanya oparesheni maalumu kwa lengo la kuwakamata watu wanaojihusisha na vitendo vya kuhujumu miundombinu ya umeme pamoja na waliojiunganishia bila utaratibu na kufanikiwa kuwakamata watu 13.

Amesema kati ya watuhumiwa hao wamo watumishi wawili wa Tanesco , Vishoka 4 , askofu wa kanisa la CAG na mchungaji mmoja pamoja na wateja 7 ambao walibainika kujiunganishia umeme kinyume cha utaratibu na wafanyakazi hao wasiokuwa waaminifu kwa kushirikiana na vishoka na kufanya wateja hao watumie umeme bila malipo yeyote.

Kamanda Magomi amesema katika oparesheni hiyo ilibainika watumishi hao wawili wasiokuwa waaminifu kwa kushirikiana na vishoka wanne walibainika kuhujumu miundombinu ya shirika kwa kuiba vifaa pamoja na kuwaunganishia wateja umeme bila kufaata taratibu na kwa maslahi binafsi.

Amesema katika hujuma hiyo jumla ya Transfoma 73 za umeme zilihujumiwa na kusasabisha uharibifu mkubwa kutokana na kuibiwa vifaa mbalimbali zikiwemo waya za kopa na kulitia hasala shirika zaidi ya shilingi milioni 10 pamoja na wateja hao waliounganishiwa umeme kinyume cha utaratibu na kutumia bule.

Kaimu meneja wa Tanesco wa Wilaya ya Kahama, Mhandisi Tumaini Chonya akifafanua kuhusu hujuma hiyo alisema wafanyakazi hao wasiokuwa waaminifu walikuwa wanaiba vifaa vya shirika na kwenda kuwaunganishia umeme watu kinyume cha utaratibu yakiwemo makanisa ya viongozi hao dini waliokamatwa na kutumia umeme bule siku zote.

Mhandisi Choya amesema hujuma iliyofanywa na watu hao ni kubwa kwa sababu wamelitia hasala shirika na kukwamisha jitihada za kupanua huduma kwa wateja hali iliyomfanya kutoa wito kwa wananchi wenye mapenzi mema kutoa taarifa kwa Tanesco na kwa jeshi la polisi kuhusu vitendo vya hujuma dhidi ya miundombinu ya shirika.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na TANESCO linatoa wito kwa mwananchi yeyote anayeju kuwa amaunganishiwa umeme kwa njia zisizo halali na kwamba anatumia umeme bure bila kulipia bili kujisalimisha kwa ofisi ya Tanesco kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa ikiwemo kukamatwa.