Mkoa wa Tanga umebarikiwa kuwa na aina mbalimbali za madini

Wafanya biashara waaswa kuzingatia Sheria za Madini

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

Wito umetolewa kwa Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini mkoani Tanga kutokana na uwepo wa aina mbalimbali za rasilimali madini mkoani humo.

Wito huo umetolewa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tanga Winnifrida Mrema hivi karibuni wakati akizungumza na Wanahabari Ofisini kwake jijini Tanga ambapo amesema, Mkoa huo umebarikiwa kuwa na aina mbalimbali za madini yakiwemo Madini ya metali kama vile madini ya Dhahabu, Chuma na Shaba, Madini ya Viwandani kama Kinywe, Bauxite, Chuma, Jasi, Chokaa, Ulanga, Dolomite, Feldspar, na Chumvi, na MadinI Ujenzi.

Aidha, Mrema amesema mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa yenye utajiri mkubwa wa madini ya vito hapa nchini ambapo ametaja aina mbalimbali ya vito vinavyopatikan mkoani humo ikiwa ni pamoja na Garnets za aina mbalimbali, Rubi, Tourmaline za aina mbalimbali, Sapphire, na Zircon na Tangastone.

Pia, Mrema amesema madini mengine yaliyopo mkoani humo ni pamoja na Madini Tembo (Heavy mineral sand), Bauxite, Chumvi, Ulanga (Mica), na Quartz

Vilevile, Mrema amesema mkoa huo umejaliwa kuwa na viwanda vikubwa vinne vinavyotumia madini mbalimbali kwa ajili ya kuzalisha wa saruji na chokaa. Viwanda hivyo ni pamoja Tanga Cement, Maweni na Kilimanjaro vinavyozalisha saruji, pamoja na kiwanda cha chokaa cha Neelkanth.

Pamoja na mambo mengine, Mrema amesema, kwa kuwa Dunia inauhitaji mkubwa wa madini mkakati hivyo ametoa wito kwa wawekezaji wakubwa na wadogo kutoka ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika madini mkakati ya Kinywe na Madini Tembo ili kujipatia faida na kunufaisha mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Mrema amewasisitiza Wamiliki wa Leseni za Uchimbaji wa Madini na wafanya biashara wa madini kuzingatia Sheria na Kanuni za Madini hususan kwa wafanya biashara ya madini ya dhahabu na vito kufanya biashara zao kupitia masoko ya madini.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Uthaminishaji wa Madini ya Vito Visetasi Kiding’a amesema, mpaka sasa mkoa wa Tanga bado hauna wawekezaji wa kutosha kulinganisha na fursa za shughuli za madini zilizopo mkoani humo ambapo ametoa wito kwa wawekezaji kujitokeza kwa ajili ya kuomba leseni za uchimbaji na ufanyaji biashara ya madini mkoani humo.

By Jamhuri