Wawili mbaroni kwa kutapeli kwa kutumia jina la Mo Dewji

Na Mwandishi Maalum

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na oparesheni, misako na doria zenye tija kuhakikisha usalama wa raia na mali zao.

Aidha kupitia misako na doria limepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kukamata watuhumiwa wa kughushi na utapeli, kupatikana silaha bila kibali na mali ya wizi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wawili wote wakazi wa Chapakazi katika Mji Mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya ambao ni Sarael Geshon (19) na Christian Erasto (21) kwa tuhuma za kughushi nyaraka mbalimbali na kutapeli watu kwa kutumia jina la “Mo Dewji Foundation”.

Watuhumiwa walikamatwa Oktoba 22, 2023 katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Altas iliyopo Mji Mdogo wa Mbalizi katika misako inayoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali.

Aidha, watuhumiwa walikutwa wakiwa na simu za mkononi Smart Phone 6, simu ndogo 3, line za simu za mtandao wa Vodacom 10, Tigo 2 na Airtel 3 zenye usajili wa majina tofauti wakizitumia kuibia watu mbalimbali kwa kutoa machapisho ya uongo kwamba wanatoa mikopo kupitia “mo dewjifoundation”.

Watuhumiwa wamekuwa wakighushi kwa njia ya kompyuta kitambulisho cha NIDA, Tin ya TRA, leseni ya biashara na usajili wa Brela kwa jina la mo dewji foundation na kisha kutapeli watu wakidai kutoa mikopo kwa riba nafuu. Watuhumiwa wamekiri kutekeleza matukio ya utapeli katika maeneo mbalimbali na kujipatia kipato isivyo halali.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mkazi wa Nsalala Mkoani Mbeya aitwaye Joshua William (19), kwa tuhuma ya kupatikana na mali ya wizi bajaji MC 548 TVS Kings rangi ya kijani. Mtuhumiwa alikamatwa Oktoba 22, 2023 huko eneo la Stendi ya mabasi ya Tunduma iliyopo Mji Mdogo wa Mbalizi akiwa katika harakati za kuisafirisha bajaji hiyo kwenda Mji Mdogo wa Tunduma Mkoa wa Songwe.

Mtuhumiwa amekiri kuhusika katika tukio la wizi wa bajaji lililotokea Oktoba 21, 2023 majira ya saa 3:00 usiku katika Kijiji cha Shigamba – Mbalizi ambapo mhanga Emanuel Obimsonge (38), mkazi wa Shigamba aliibiwa bajaji hiyo yenye thamani ya Tshs 9,100,000.

Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mzee wa miaka 80 mkazi wa Kijiji cha Madundasi Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya aitwaye Paschal Mwango kwa tuhuma za kupatikana na bunduki aina ya Gobole bila ya kuwa na kibali cha umiliki halali.

Mtuhumiwa alikamatwa Oktoba 20, 2023 huko Masenjele ndani ya hifadhi ya taifa ya Ruaha wakati Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa Jeshi la Uhifadhi – TANAPA likiwa katika misako na doria dhidi ya wawindaji haramu na majangiri wanaofanya uhalifu ndani ya hifadhi ya Taifa.

Katika upekuzi alikutwa na bunduki moja (gobole), risasi (golori) 35, unga wa baruti ukiwa kwenye mfuko wa plastiki, kisu 1, kiberiti 1 na fataki mbili za kulipulia bila kibali cha umiliki halali wa vitu hivyo. Mtuhumiwa amekuwa akifanya uhalifu kwa kuwinda na kuua wanyama pori ndani ya hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kusalimisha kwa hiari katika vituo vya Polisi, ofisi za serikali za mitaa na ofisi za watendaji wa Kata.

Muda wa kusalimisha silaha ni kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi 10:00 jioni. “Hujachelewa, salimisha silaha sasa katika kipindi cha msamaha” Pia katika muendelezo wa misako, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa sita kwa tuhuma za wizi wa mali zinazosafirishwa kwa magari.

Imetolewa na Benjamini Kuzaga ACP Kamanda wa Polisi,Mkoa wa Mbeya.