Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Dodoma

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa jitihada inazofanya za kuishauri na kutoa maoni yanayoiwezesha Serikali kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kupitia Sekta ya Maliasili na Utalii.

Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo leo Jijini Dodoma kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Wizara ya Maliasili na Utalii akieleza kuwa Wizara anayoiongoza itaendelea kutekeleza majukumu kwa ufanisi na kuunga mkono kazi kubwa aliyoifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwenye Wizara hiyo kwa kuhakikisha lengo la kuongeza mapato na idadi ya watalii linafikiwa.

Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana ameongeza kuwa licha ya uwepo wa janga la UVIKO-19, Programu aliyoanzisha Rais Samia Suluhu Hassan ya Tanzania The Royal Tour imezidi kuitangaza vyema Tanzania na kuongeza idadi ya watalii na mapato na kwamba hiyo ni ishara kuwa Sekta ya utalii inaendelea kuimarika baada ya Janga la UVIKO -19.

“Ni ukweli usiopingika kuwa kupitia ushauri wa Kamati hii, Wizara imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa na hivyo kuleta tija katika maendeleo ya Taifa letu husuan kukuza uchumi na ustawi wa maisha ya Watanzania” Amesisitiza Mhe. Balozi Dkt.Chana.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb), Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka , Wakurugenzi wa Wizara na baadhi ya Wakuu wa Taasisi , Wizara ya Maliasili na Utalii imewasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Chuo cha Viwanda wa Misitu (FITI) na taarifa ya utekelezaji ya miaka 4 ya Mradi wa Kuongeza Mnyororo wa Thamani ya Mazao ya Misitu (FORVAC).

By Jamhuri