Waziri Dk. Mwigulu epuka kodi za kero

Na Deodatus Balile, Dodoma

Wiki iliyopita nilikuwa katika Ukumbi wa Bunge. Nilimsikiliza kwa umakini mkubwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, wakati anawasilisha bajeti ya wizara yake. Dk. Mwigulu alieleza kuhusu maeneo mengi hasa kilimo kwa ufasaha mkubwa hadi nami nikavutiwa kuwekeza katika kilimo. Mipango ya serikali aliyoitaja kwenye bajeti ya mwaka huu ikienda sambamba na upatikanaji wa fedha, maana mipango ni kitu kimoja na fedha ni kitu kingine, basi nchi yetu itajinasua kwenye wimbi la umaskini.

Sitanii, leo sitazungumzia mipango hiyo. Nazungumzia maeneo mawili ambayo wabunge wasipoyaangalia vizuri na kuyakataa, tutakuwa na mgogoro mkubwa kati ya serikali na wananchi si muda mrefu. Waziri alitangaza kuanzisha kodi ya ving’amuzi ambayo ni kati ya Sh 1,000 na Sh 3,000. Kodi hii haikufafanuliwa ni vigezo vipi vitatumika.

Hakufafanua kama itatozwa kwa mwezi, kwa wiki au kwa mwaka. Kumekuwapo kilio cha muda mrefu cha wamiliki wa visimbuzi (ving’amuzi) wakitaka wananchi wavilipie. Nadhani hapa tumekwenda kasi mno pasipo ulazima. Hawa wenye visimbuzi walipaswa kubanana na wazalishaji wa maudhui ndio walipie gharama za kurusha matangazo.

Vituo vya runinga vinarusha matangazo ya biashara katika vipindi vyake. Faida inayopatikana, kamwe hawamrudishii mwananchi ambaye ndiye anazalisha fedha hizo kwa kununua bidhaa mbalimbali wanazozitangaza. 

Nafahamu wamiliki wa ving’amuzi watakuwa wamefurahi, lakini ikiwa hivyo ndivyo, basi hata wachapaji wa magazeti wataomba serikali iweke kodi ya namna hiyo kwa wananchi wote kulipia gharama za kuchapa magazeti. Hii si sahihi kuwatoza wananchi wote fedha za kuendesha biashara za watu binafsi.

Jambo jingine linalopaswa kuangaliwa kwa kina, vyombo vya habari ndicho chombo pekee cha kuelimisha wananchi wetu. Kwa mtu anayetafuta utajiri hawezi kuwekeza kwenye vyombo vya habari. Huku ni huduma kwa jamii. Kuwatoza wananchi gharama ya kumiliki TV, si sahihi. Tukianza kupata hamu hii, baadaye tutahamia kwenye simu za mkononi, redio na magazeti kila mwananchi atatozwa kodi ya kuwapo au kumiliki bidhaa hizi za elimu kwa umma.

Sitanii, ukiacha hili la kodi ya TV ambalo halijakaa sawa, nimeona ufafanuzi wa Dk. Mwigulu juu ya Watanzania wote wenye umri wa miaka 18 kulipishwa kodi, ila sijamwelewa. Siku ya Jumanne bungeni, Dk. Mwigulu alisema hivi: “Mheshimiwa Spika, kila Mtanzania mwenye umri wa zaidi ya miaka 18 na mwenye kipato anatakiwa kulipa kodi. Ili kutimiza azima hiyo, serikali inakusudia kutoa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN) kwa kila Mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 au zaidi.

“Kwa kuwa usajili wa namba za utambulisho wa Taifa (NIDA) unamtaka kila mwananchi mwenye umri wa miaka 18 au zaidi kujisajili NIDA, napendekeza kuwa wale wote wenye NIDA kwa sasa (wanaofikia milioni 19 nchi nzima) wapatiwe namba za TIN na itumike kwenye miamala yote inayofanyika katika ununuzi na mauzo yote yanayofanyika ndani ya nchi. Kila mwenye namba ya mlipakodi atapata makadirio yake kwa njia ya simu na kulipa kodi husika kwa njia ya mtandao.”

Niliposikia kauli hii moyo wangu ulipiga paaaaaa! Nilijiuliza Mhe. Mwigulu anaifahamu Tanzania au anaiangalia kupitia kwenye taarifa ya habari? Nikajiuliza kama amepata kufika Nanjilinji, Kikakati, Nkunya, Kibirizi, Kojani au maeneo ya ndani kabisa vijijini ambapo tajiri mkubwa anamiliki baiskeli! Nikajiuliza kama waziri hakuamka akafananisha maisha ya Dar es Salaam na Namanyere. Huko vijijini bado watu wanabadilishana nyama na ndizi kali (enyama yenkundi).

Lakini pia nikapata tabu kidogo. Kwamba anasema mwananchi ataletewa makadirio kwenye simu yake na kulipa kodi kupitia simu yake. Lohooooo! Hivi iko wapi nafasi ya kujadiliana kati ya mtoza kodi na mlipa kodi? Lakini kama kigezo kitakuwa ni kupitia ununuzi anaoufanya, kuna udhibiti gani umewekwa kutambua kuwa kipato alichokitumia kufanya ununuzi Mwalimu wa Shule ya Msingi Nanjilinji, kimetokana na mapato ambayo tayari yamelipa kodi ya mapato (PAYE), kodi ya kuendeleza ujuzi (SDL) na kodi nyinginezo?

Hapa kuna hatari ya wafanyakazi kukadiriwa kodi katika fedha ambazo tayari wamezilipia kodi. Nafahamu nchi kama Marekani zinatumia mfumo huu wa kila mwananchi wake kukadiriwa kodi na kufanya marejesho kila mwaka. Lakini alichosahau Mhe. Mwigulu ni kuwa Wamarekani wana mifumo. Mwananchi anapofanya marejesho (annual returns), mifumo inasoma na kubaini pato lipi limetokana na ajira ambalo tayari limelipiwa kodi.

Wakati anafafanua sintofahamu hii, akajikoroga zaidi kwa kusema: “Kuhusu kodi haitozwi kwa kila mtu, anatozwa mwenye kipato, kwa hiyo mtu mwenye kipato ndiye atakayetozwa kodi si mtu mwenye kitambulisho cha taifa. Kitambulisho cha taifa ni utambuzi, lakini kodi anatozwa yule mwenye kipato, watu wasipate hofu, sisi tunarahisisha,” amesema Dk. Mwigulu.

Sitanii, hapa kwetu kama tumekaa miaka sita bila wafanyabiashara wenye angalau mfumo unaoeleweka ikashindikana kurejeshewa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT receivable), hivi unatarajia kwa mwananchi wa kawaida kijijini atakayekadiriwa Sh 300,000 kwa mwaka itakuwaje? Naiona nia ya kupanua wigo wa walipa kodi, lakini hatuwezi kwenda hivyo. Mfumo huu unaopendekezwa ni zaidi ya kodi ya kichwa.

Miaka ya 1980 wanaume wengi walikuwa wanalala porini kwa sababu ya kodi ya baiskeli ya Sh 250. Kodi ya kichwa ilikuwa Sh 4,000, lakini Basil Mramba aliifuta mwaka 2005 baada ya kushuhudia mateso iliyowapa Watanzania katika nchi yao huru. Mfumo huu anaoupendekeza Waziri Mwigulu unakwenda kujaza magereza au kufilisi wananchi. Bila kumng’unya maneno, kodi hii itakuwa chanzo kizuri kwa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuchukiwa na wananchi. Mimi nashauri tusijaribu kuonja sumu. Mfumo huu wa kodi unaopendekezwa usitishwe, tutafute vyanzo vingine kama nchi.