Nguvu ya umma imeshinda vita dhidi ya ghiliba na hujuma za Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.

Naam, Nyalandu kwa kujipa moyo, amediriki kuunda nukuu yake inayosema, “Watu ambao wanaandika habari ambazo zinasononesha mioyo ya watu na kuaminisha watu kuwa habari hizo ni za kweli, mikono yao ione aibu kushika kalamu iliyojaa wino na kuandika uongo”.

Akaendelea kusema, “Watu hao mahali pao ni katika ziwa la moto, lenye moto mkali”.

Tungeshangaa kama Nyalandu na kundi lake wangeshindwa kubuni maneno ya kisanii ya aina hii. Kwake yeye, yote yanayoandikwa juu yake ni uongo na ghiliba! Hii ndiyo aina ya Waziri tuliye naye.

Tunawashukuru na kuwapongeza mno wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliosimama kidete kumbana Nyalandu kutokana na uongozi wake wa visasi na uliojaa maslahi binafsi ya sifa.

Wabunge na viongozi waandamizi kama Mbunge wa Ngara, Deogratias Ntukamazina, hawakusita kumwambia Nyalandu wazi kwamba kwa kuwaondoa wakurugenzi wale kisiasa, alikuwa kavunja sheria.

Mbunge wa Viti Maalum, Mama Zakia Meghji, ambaye ndiye waziri pekee wa Maliasili na Utalii aliyedumu kwa miaka tisa katika wizara hiyo, alimkanya juu ya mpango wake wa kufungua Mpaka wa Bologonja ambao Mwalimu Nyerere aliufunga mwaka 1977 kutokana na maslahi mapana ya kiuchumi na kimazingira kwa nchi yetu.

Magdalena Sakaya akahoji mbinu za ‘uuzaji’ Hifadhi za Taifa kwa kampuni ya African Parks Network (APN), na mambo mengine mengi. Yote haya na mengine ya uongezaji muda wa uwindaji kutoka miezi minane hadi tisa, Nyalandu aliyathibitisha. Kumbukumbu za Bunge zinaonesha hivyo.

Anapozomoka na kudai kwamba wanaomwandika wanaandika uongo, anajua fika kabisa kuwa anachosema si kweli. Hakuna habari iliyondikwa juu yake ambayo inapaswa kumsononesha. Kinachomuuma ni kuona kila anachojaribu kukifanya kwa hila, Mungu anakuwa upande wa wapenda nchi yao!

Sehemu ya tahariri yetu ya kwanza kabisa tuliyoichapisha Desemba 6, 2012, ilisema hivi, “Kwa kuwa hili ndilo toleo la kwanza, tunapenda kuweka bayana baadhi ya shabaha zetu kuu. JAMHURI ni gazeti huru lisilofungamana na chama chochote cha siasa wala mwanasiasa awaye yeyote. Halifungamani na mfanyabiashara yeyote. Ni gazeti linalosimama katika ukweli na haki.

JAMHURI halitamwonea mtu au kikundi cha watu kwa kuripoti habari zisizokuwa na ukweli. Litakuwa mstari wa mbele kusifu pale panapostahili sifa, na kukosoa pale ambako kunastahili kukosolewa… Kwa wale wanaostahili kupongezwa, hatutasita kuwapongeza.”

Haya tuliyasema tukiwa hatujui kama kuna siku Nyalandu atakuwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Wala hatukujua tutakuwa na kiongozi wa wizara mwenye maono hafifu anayeweza kudiriki kufungua mpaka wa Bologonja kwa sababu ya maslahi yake na rafiki zake.

Hatukujua kama kutakuwa na kiongozi katika Wizara hii mwenye ndoto ya ‘kuuza’ Hifadhi kwa ushirika wake na viongozi wenzake wanaojitahidi kujifanya waadilifu mbele ya umma, lakini ni hatari kwa mustakabali wa Taifa letu.

Sasa upo mpango mahsusi uliokwishaiva wa Nyalandu na maswahiba wake kutufikisha mahakamani kutufunga midomo ili tusiendelee kuwasema kwa matendo yao hatari. Tunasema kama kazi hii hatutaifanikisha sisi, kizazi kijacho kitaimaliza ngwe itakayokuwa imesalia.

Nyalandu aache tumtendee haki. Tuna wajibu wa kuwasema wote wenye vimelea vya kuliangamiza Taifa letu kiuchumi.

1061 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!