Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge wakati alipowasili kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Mwandege wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani kukagua ujenzi wa madarasa na kuzungumza na wananchi, Novemba 27, 2022. Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange na wa pili kushoto. Ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Shaaban Mlao. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Mwandege wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani kukagua ujenzi wa madarasa na kuzungumza na wananchi akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya mkoa wa Pwani, Nevemba 27, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari Mwandege wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya Mkoa wa Pwani, Novemba 27, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim  Majaliwa akipanda mti baada ya kukagua ujenzi wa madarasa ya Shule ya Sekondari Mwandege. Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya Mkoa wa Pwani, Novemba 27, 2022.  Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge.( Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri nchini kutumia fedha za makusanyo ya ndani katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo badala ya kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu pekee.

Amesema hayo leo (Jumapili, Novemba 27, 2022) wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa sita katika shule ya Sekondari ya Mwandege iliyopo Wilaya ya Mkuranga, Pwani.

Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mwantumu Mgonja kutenga kiasi cha shilingi milioni 120 kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la utawala katika shule hiyo ifikapo Januari 2023.

Akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba hivyo vya Madarasa, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga vizuri kuwahudumia watanzania ili kusaidia kuchochea shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

“Huu ni wakati wa kufanya kazi, nimeridhika na viwango vya ujenzi wa vyumba madarsa katika shule hii, endeleeni kusimamia viwango kwenye miradi mingine, twende na matakwa ya Rais wetu na kumsadia kutimiza  maono yake ya kuwahudumia watanzania”

Waziri Mkuu amesema kuwa mipango ya Rais Samia ni kuhakikisha kwamba Serikali inawafikia watanzania popote walipo hadi vitongojini kwa kupeleka huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo afya, maji, shule, umeme pamoja na mawasiliano.

Aidha,Majaliwa ametoa wito kwa wakulima wote nchini kutumia mvua hizi za mwanzo kuanza kujishughilisha na shughuli za kulima.  “Mvua za kwanza ndio mvua za kupandia, twende tukaanze kazi ya kilimo, tupande mazao yenye uwezo wa kuota kwa muda mfupi ili yaweze kuiva na kutusaidia kupata chakula”

Pia Mheshimiwa Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali kuzungumza na wakulima kutumia vizuri chakula kilichopo ili kiweze kuwasaidia kufika msimu ujao wa mavuno.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange amesema kuwa mkoa wa Pwani umepokea kiasi cha shilingi bilioni 6.8 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 341. “Wananchi wa Mkuranga niwahikishie kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria na anafanya kwa vitendo kutuondolea adha ya vyumba vya madarasa”

Naye Mbunge wa Mkuranga na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdala Ulega amemshukuru Rais Samia kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya ya Mkuranga na mkoa wa Pwani kwa ujumla.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa Afisa Elimu Idara ya Sekondari Benjamin Majoya amesema kuwa Wilaya ya Mkuranga imepokea fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa 132 ya kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 katika shule 26 za sekondari yenye thamani ya shilingi bilioni 2.64.

Amesema kuwa kukamilika kwa vyumba hivyo vya madarasa pamoja na vilivyopo kutawezesha  jumla ya wanafunzi 10,800 kupata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2023 wilayani Mkuranga.

Mheshimiwa Majaliwa leo Novemba 27, 2022 ameanza ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuongea na watumishi katika mkoa wa Pwani!

By Jamhuri