Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Chunya

Waziri wa Madini Anthony Mavunde apokea changamoto mbalimbali za wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu wilayani Chunya mkoani Mbeya katika machimbo ya Itumbi akiwa katika ziara maalum ya kikazi.

Waziri Mavunde akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Chunya Ndugu Mayeka Simon Mayeka alipokelewa na wachimbaji zaidi ya 200 ambao katika mkutano walitaja changamoto zao mbalimbali kama vile ukosefu wa mitaji , vifaa duni vya uchimbaji , ukosefu wa Nishati ya Umeme na kukosekana kwa Miundombinu salama.

Mapema baada ya kupokea changamoto hizo Mhe.Mavunde aliwatoa hofu wachimbaji kwa kuwaambia kuhusu mikakati mbalimbali iliyowekwa na Serikali katika kuwainua wachimbaji wadogo nchi nzima kwa kuwapatia mashine za uchorongaji, kuwaunganisha na Taasisi za fedha ili kupata mikopo yenye riba nafuu na mpango wa kufanya utafiti wa kina ili kupata taarifa sahihi za miamba na madini.

Mhe.Mavunde amewataka wachimbaji wa Itumbi kujiunga na kujisajili rasmi katika vikundi ili watambulike na kuwekwa katika mikakati ya serikali itayowawezesha kujengewa uwezo na kutatua changamoto zao.

Mhe .Mavunde amemuagiza Afisa Madini Mkazi Chunya ndugu Sabahi Nyansiri kusimamia na kuratibu zoezi hilo la kuunda vikundi na kuvisajili katika mifumo rasmi ili vitambulike na mamlaka husika.

Soko la Madini Wilayani Chunya lilianzishwa Mei 2, 2019. Kabla ya soko kuanza dhahabu iliyokuwa ikionekana katika takwimu za Serikali ni kilogramu 20 na baada ya soko kuanza wastani wa dhahabu inayopatikana kwa mwezi ni zaidi ya kilogramu 250.

By Jamhuri