Home Kitaifa WAZIRI MKUCHIKA AWAFUNDA WALENGWA WA TASAF

WAZIRI MKUCHIKA AWAFUNDA WALENGWA WA TASAF

by Jamhuri

Waziri wa Nchi Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Mhe. George Mkuchika (aliyevaa suti nyeusi) akikagua bidhaa zilizotengenezwa na Walengwa wa TASAFkatika mtgaa wa Inyala katika jiji la Mbeya  kama njia mojawapo ya kujiongezea  kipato. 

Waziri Mkuchika (aliyevaa tai) akimsikiliza mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lupeta katika jiji la Mbeya alipotoa maelezo ya maabara iliyojengwa na TASAF shuleni hapo.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika akikagua jengo la maabara lililojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF katika shule ya Sekondari ya Lupeta katika halmashauri ya jiji la Mbeya.

 Picha ya juu na chini zinawaonyesha wanafunzi wanaotoka katika kaya za walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika Mtaa wa Inyala katika jiji la Mbeya wakitoa ushuhuda kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. George Mkuchika (watatu  kutoka kushoto) namna wanavyonufaika na ruzuku kutoka TASAF  

Baadhi ya Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika mtaa wa Inyala katika jiji la Mbeya wakiimba nyimbo mbele ya Waziri George Mkuchika kushukuru hatua ya serikali kupitia TASAF kubuni Mpango huo ambao wamesema umeleta chachu ya maendeleo katika eneo hilo. 

Waziri Mkuchika na viongozi wa mkoa na wilaya ya Mbeya pamoja na TASAF wakisikiliza risala ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini  katika Mtaa wa Inyala (hayupo pichani) wakati waziri huyo alipokutana na walengwa wa Mpango huo kuona namna wanavyonufaika na huduma za Mpango huo unaotekelezwa na Serikali kupitia TASAF.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Mkuchika amewatembelea Walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF katika halmashauri ya Jiji la Mbeya na kuwataka kuongeza jitihada zaidi za kujitegemea kwa kutumia ruzuku wanayoipata kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali ili kukuza kipato chao.

Mheshimiwa Mkuchika amesema jitihada za serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF za kuhamasisha wananchi kuuchukia umasikini haziwezi kuwa endelevu ikiwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini hawatatumia fedha wanazozipata kubuni miradi ya uzalishaji mali.

“hiki mnachokipata kutoka serikalini kupitia TASAF kiwe chachu ya kuanzisha miradi ya uzalishaji mali ili hatimaye muweze kujitegemea” amesisitiza Waziri Mkuchika.

Akiwa katika eneo la Shule ya Sekondari ya Lupeta katika jiji la Mbeya , shule ambayo TASAF imejenga jengo la Utawala na Maabara,Waziri Mkuchika ameeleza kuridhishwa na matokeo ya ujenzi wa majengo hayo na kupunguza kero iliyokuwa inawakabili walimu na wanafunzi shuleni hapo.

Aidha Mheshimiwa Mkuchika amekutana na vikundi vya uzalishaji mali vilivyoanzishwa na Walengwa wa TASAF kwa kutumia ruzuku ya fedha kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambapo walengwa hao wamekuwa wakikopeshana fedha zinazotokana na uzalishaji wa bidhaa zikiwemo mikeka,na hivyo kuwaongezea uwezo wa kuhudumia kaya zao.

Hata hivyo Waziri huyo ametoa maagizo kwa uongozi wa mkoa wa  Mbeya kuhakikisha kuwa watu wanaonufaika na fedha za ruzuku kutoka TASAF ni wale wanaokidhi vigezo vya umasikini na kutaka fedha zilizolipwa kwa watu wasiostahiki zirejeshwe mara moja.

“rejesheni fedha za serikali ili ziwanufaishe walengwa wanaostahiki kupata ruzuku hiyo kama ilivyokusudiwa na serikali” ameonya Waziri Mkuchika.Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bi. Mercy Mandawa ameishukuru serikali kwa kuendelea kuusimamia kikamilifu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF ili uendelee kusaidia jitihada za kuwaondolea wananchi kero ya umaskini.

Amesema tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ,kumekuwa na mwitikio chanya kwa walengwa kutumia ruzuku hiyo kuboresha maisha yao huku mkazo ukiwekwa katika kuboresha elimu,afya na lishe kwa watoto wanaotoka  kwenye kaya za walengwa huku akisisitiza juu ya matumizi sahihi ya ruzuku inayotolewa kila baada ya miezi miwili.

You may also like