WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Bi. Isabella Chilumba na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk. Oscar Mbyuzi waache malumbano ambayo yanawavuruga watendaji walio chini yao.

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Januari 6, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwenye kikao kilichofanyika hoteli ya Mt. Vicent, mjini Mbamba Bay, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.

Amesema katika ziara zake zote za mikoani, amekuwa akipata malalamiko mengi kwenye Halmashauri na mabaraza ya madiwani lakini katika wilaya ya Nyasa amekuta hali ni shwari  isipokuwa kuna migogoro midogo kwenye uongozi wa juu.

“Tatizo ni dogo huku juu, bado mnavurugana Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi. Ninyi ni viongozi wa juu, acheni kuvurugana, fanyeni kazi. Mkigombana wanaoumia ni wananchi,” alisema.

“Mkuu wa Wilaya anaweza kuingia kwenye kikao chochote cha Halmashauri na kudai apewe taarifa, mpeni. Yeye siyo mjumbe wa kikao hicho lakini anayo mamlaka ya kushiriki.”

“Mkurugenzi wewe ni mtendaji mkuu, tumekukabidhi watumishi uwaongoze. Tumekukabidhi fedha kwa ajili ya maendeleo ya wilaya hii. Mtu akizitamani, mwambie hizi fedha zina maelekezo rasmi, hazipaswi kwenda kokote,” alisisitiza.

Aliwataka madiwani wasijenge tabia ya kuongeza siku za vikao kwa makusudi ili tu wapate posho za ziada. “Msitengeneze siku za ziada na kumpa presha Mkurugenzi. Kama kikao ni cha siku moja, basi kiishe. Siyo kulaza ajenda ili mmalizie kesho yake. Mkurugenzi akiwanyima fedha, msianze kugombana naye kwa sababu yeye hana fedha za kumgawia mtu,” alisisitiza.

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU, 

JUMAPILI, JANUARI 7, 2018.

By Jamhuri