*Wanatembea kilometa 24 kila siku

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Nimekuwa na utaratibu za kuzuru maeneo mbalimbali vijijini. Katika pitapita zangu wiki iliyopita nilifika katika eneo ambalo mikoa mitatu ya Manyara, Morogoro na Tanga inapakana. Wilaya zinazokutana hapa ni Kiteto (Manyara), Gairo (Morogoro) na Kilindi (Tanga).

Niliweka kambi ya muda katika Kijiji cha Olgira kilichopo Kata ya Sunya, Wilaya ya Kiteto.

Barabara kuu inayounganisha kijiji hiki na kijiji jirani cha Majengo kilichopo Wilaya ya Kilindi, inapita katikati ya nyumba chache zilizoko katika ‘centre’ ya hiki kijiji. Kwa sababu hiyo, ukisimama mbele ya nyumba unakuwa na fursa ya kuwaona vizuri wapita njia.

Ni katika mazingira hayo hayo, niliwaona wanafunzi wa shule ya msingi wakienda shuleni kuanzia saa 12 asubuhi.

Ule utaratibu wa miaka yote wa wanafunzi kuwahi shuleni ili waanze masomo inapotimu saa 2:00 bado haujabadilika. Kwa kutambua hilo, unapoona wanafunzi wakiendelea kupita kwenda shuleni hata inapokuwa tayari ni saa 3 asubuhi, kwa mzazi au mlezi yeyote ni kawaida kabisa ajiulize maswali kadhaa.

Siku ya kwanza nilidhani hawa wanafunzi wanapita kwenda shuleni saa 3 hadi saa 4 asubuhi, kwa kuwa huenda wakawa katika ratiba ya michezo. Lakini nilipoona hali ni hiyo hiyo kwa siku iliyofuata, nikalazimika kuwauliza baadhi yao.

Majibu niliyoyapata ndiyo yaliyonisukuma kuandika makala hii kwa lengo mahususi la kuwasihi viongozi katika ngazi zote za vijiji, kata, wilaya, mkoa hadi taifa walete ufumbuzi wa haraka ili kumaliza kadhia hii kwa watoto wa eneo hili la Tanzania.

Watoto hawa wanaingia shuleni saa 3 hadi saa 4 asubuhi si kwa kupenda, bali ni kutokana na umbali kutoka wanakoishi na mahali iliko shule pekee ya msingi ambayo nayo haina vyumba vya kutosha.

Watoto hawa wanatembea kilometa 12 kwenda shuleni, na kilometa 12 kurejea nyumbani – hii ikiwa na maana kwamba kila siku mtoto analazimika kutembea kilometa 24 kufuata masomo na kurejea nyumbani.

Kunahitajika muujiza wa akili kwa mtoto aliye kwenye mazingira ya aina hii kufaulu mitihani, na zaidi ya yote, kufaulu maisha.

Ndugu zangu, hizi ni kilometa 24 za kwenda kwa miguu, na si kwa gari, pikipiki au baiskeli. Watoto hawa ni wale wa kuanzia shule ya awali hadi darasa la saba. Fikiria tena kilometa 24 za kwenda kwa miguu!
Iko hivi: Kijiji cha Olgira kina vitongoji vitano. Kati ya hivyo, vitongoji vitatu vya Mtarudi, Songambele na Machakosi ndivyo pekee vilivyo karibu na Shule ya Msingi Olgira.

Kitongoji cha Mbikasi ambacho kipo mbali na Shule ya Olgira, tayari kilikwisha kupata shule, japo nayo watoto hutembea hadi kilometa 10 kwenda shule na kilometa nyingine kama hizo kurejea nyumbani.

Shida kubwa ipo kwa watoto walio katika Kitongoji cha Natushu ambacho ndicho ninachokilenga. Kitongoji hiki kipo kilometa 12 kutoka yalipo makao makuu ya Kijiji cha Olgira. Hakina shule. Kwa kuwa suala la elimu linasisitizwa, watoto hawa wamejikuta wakitaabika kutembea umbali mrefu kupata haki yao ya elimu.

Je, wazazi na walezi wa hawa watoto hawaoni adha wanazopata watoto wao? Wanaziona na kwa hakika zinawakera mno. Nimezungumza na wazazi na baadhi ya viongozi wa eneo hili. Uongozi wa Kijiji cha Olgira na Kitongoji cha Natashu waliketi na kukubaliana kwa kauli moja kutenga eneo na kujikamua kiuchumi kujenga shule ili kuwaondolea mateso watoto wao.
Wananchi wenye dhamira wakatoa eneo lao la ardhi lenye ukubwa wa ekari 70 ili litumike kujenga shule, nyumba za walimu na huduma zote zinazotakiwa kwa maendeleo ya wanafunzi kama vile vyoo, viwanja vya michezo na mashamba.

Kitongoji hiki kina wanafunzi wengi, na hilo linathibitishwa na idadi ya kaya 209 ambazo hadi mwaka jana zilikuwa zimeandikishwa kuwapo katika kitongoji hicho. Idadi hii inakuwa sifa au kigezo cha eneo hili kustahili kupata shule ya msingi, hasa ukizingatia uzazi wao nao si haba.

Wananchi wa Natushu bila kujali hali yao ya umaskini wakajipigapiga na kuchanga fedha zilizowezesha kupatikana matofali 6,000 ya kuchoma, lori 5 za mawe, lori 4 za mchanga, mifuko 30 ya saruji na nondo 10.
Kwa kuonyesha dhamira yao ni ya kweli, vifaa vyote hivyo wakavipeleka eneo la ujenzi. Hali ilivyo sasa ni kama kukwama au kusuasua kwa ujenzi huu kunasababishwa na uongozi wa wilaya na halmashauri husika.

Kijiji cha Olgira ni miongoni mwa vijiji vilivyo ndani ya Hifadhi ya Msitu ya SULEDO. Utunzaji msitu huo umesababisha ongezeko kubwa la wanyamapori, wakiwamo wanyama wakali.

Ukiacha hatari ya wanyama wakali, wakati wa mvua maeneo haya hayapitiki kwani kuna mabonde na makorongo makubwa yanayotiririsha maji mengi.

Kwa maelezo ya wazazi, kujengwa kwa shule ya msingi katika Kitongoji cha Natushu kutawasaidia pia mamia ya watoto wa Kitongoji cha Kimkulesha, Kijiji cha Ngayaki wanaotaabika sasa kwa kutembea kilometa 10 kusaka masomo eneo la Leshata wilayani Gairo.

Wakati mpango wa kuwa na shule katika Kitongoji cha Natushu ukiwa unakazaniwa na wazazi, ni vizuri hawa watoto wakatazamwa kwa jicho la huruma na mamlaka za nchi kuanzia Wilaya ya Kiteto hadi taifa.
Hali waliyonayo hawa watoto inatia huruma na simanzi. Watoto wanatoka nyumbani kiza, wanarejea kiza. Wanalazimika kuamka mapema na kuanza kutembea saa 11 alfajiri kabla ya kuwasili shuleni saa 3 asubuhi au zaidi ya hapo.

Wawapo shuleni hawapati kifungua kinywa wala chakula cha mchana. Watoto wanapiga miayo tu. Nyuso zinaonyesha wazi kukata tamaa. Kwa kawaida masomo yanaahirishwa saa 10 jioni. Hata hivyo, walimu niliozungumza nao wanasema umewekwa utaratibu maalumu wa kuwaruhusu wanafunzi wa Natushu na wengine wanaoishi mbali kuondoka shuleni saa 9 alasiri. Hii ina maana wanakosa vipindi vya saa nzima. Huu ni ushahidi wa namna watoto hawa wanavyopata shida, pia wanavyokosa haki ya kupata elimu iliyo timilifu.

Mazingira magumu yamesababisha maendeleo ya wanafunzi hawa kuwa mabaya, huku wengine wakikatisha masomo kwa mimba za utotoni, na wengine kwa kukwepa adha ya kutembea kilometa 24 kila siku.
Wanafunzi wa eneo hili la ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanayo haki ya kikatiba ya kupata huduma muhimu, zikiwamo za elimu kama walivyo watoto wengine nchini.

Yawezekana mateso haya wanayapata kwa sababu viongozi katika ngazi mbalimbali hawayajui haya, na hawayajui kwa kuwa, ama hawana taarifa, au hawahangaiki kuzuru maeneo yasiyofikika kwa urahisi.

Basi, kupitia safu hii nawasihi viongozi wenye dhamana na masuala ya elimu wayapokee haya kwa nia njema kwa lengo la kurejesha furaha kwa wanafunzi na wananchi wa eneo hili la Kiteto, Kilindi na Gairo. Waziri Mkuu akiamua, shule hii itajengwa ndani ya wiki kadhaa, hivyo kuleta furaha ya miaka mingi ijayo.

Mwalimu Julius Nyerere alisema: “Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.” Kila mmoja atimize wajibu wake. Wajibu wangu wa kuwaeleza wahusika nimeutekeleza.

By Jamhuri