DAR ES SALAAM

NA THEONESTINA KAIZA-BOSHE

Katika makala iliyopita nilizungumzia mazuri, shutuma na ya kujifunza kuhusu hatua ya serikali kuhamisha Wamasai kwa hiari kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) kwenda Kijiji cha Msomera, Handeni mkoani Tanga.

Nikaipongeza kwa tukio hilo la kihistoria na la kipekee. Hata hivyo, kuna jambo kubwa sikuzungumzia katika makala hiyo; nalo ni kama hatua hiyo inaweza kuwa mwarobaini wa mgogoro sugu wa wafugaji ndani ya NCA unaotishia uhai wa hifadhi hiyo. 

Kwa maneno mengine, kuna haja kwa serikali kutafakari kama hatua hiyo itaiwezesha hifadhi hii kudumu.

Kabla ya kujadili suala la kudumu kwa NCA, ningependa kutoa maelezo mafupi kuhusu hifadhi hiyo. Hii itasaidia kuona kiini cha mgongano na changamoto katika kutafuta suluhu.

NCA ni eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 8,288 katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, lililotengwa mahususi kwa Sheria namba 14 ya mwaka 1959 kuwa eneo la kipekee kuhifadhi wanyamapori kukiwa pia kumeruhusiwa kuishi binadamu na mifugo yao kwa mfumo wao wa maisha ya pamoja.

Ni muhimu kutambua kuwa sheria hiyo iliwahusu Wamasai kwa vile ndilo kabila lililohamishwa katika mabadiliko ya hadhi ya Hifadhi ya Serengeti na uanzishwaji wa NCA.  

Katika mabadiliko hayo, serikali ya mkoloni iliruhusu wafugaji iliowahamisha kutoka Serengeti wakaishi kwenye eneo la Milima ya Ngorongoro na Bonde la Ngorongoro (Ngorongoro Crater), maarufu, kreta.

Kreta kwa wakati huo ilikuwa Ngorongoro Closed Reserve, ambamo kabla ya kuhamishiwa watu hai hakukuruhusiwa kuishi binadamu, ama kufanya shughuli zozote za kibinadamu. 

Ruhusa hiyo ilikuwa ni fidia kwa wafugaji kuhamishwa kutoka eneo lililokuwa limefanywa kuwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti; hadhi ya uhifadhi isiyoruhusu makazi, wala shughuli zozote za kibinadamu.

Aidha, sheria iliyoanzisha Hifadhi Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Ordinance) ilikuja baada ya makubaliano baina ya serikali ya wakati huo na Wamasai kama ilivyotamkwa na Gavana wa Tanganyika wa wakati huo kwa Baraza la Jimbo la Wamasai (Maasai Federal Council) Agosti 27, 1959.

Tamko hilo, pamoja na mengine, linasema: “Kukitokea mgongano wa kimasilahi baina ya wanyamapori na wakazi, masilahi ya wakazi yaheshimiwe (yapewe kipaumbele).” Ni tamko hili lililoendelea kushikiwa bango na Wamasai katika kudai wanachokiona ni haki zao, na kulalamikia serikali kuwaonea na kutowathamini.

Mbali na sheria ya nchi, uendeshaji wa shughuli za uhifadhi NCA zinaongozwa na miongozo ya kimataifa inayolinda hadhi ya hifadhi hiyo kama Biosphere Reserve na International Heritage Site.

Hivyo, kimsingi, kudumu kwa Ngorongoro kunategemea uwepo wa uwiano baina ya binadamu, mifugo, wanyamapori, rasilimali za kiikiolojia, nyara za kitamaduni na mambo ya kale, na shughuli za kitalii; kwa namna inayoruhusu hifadhi hiyo kuendelea kukidhi matakwa ya hadhi yake kisheria na mikataba ya kimataifa inayoihusu. 

Hapa ni muhimu ifahamike kuwa baada ya nchi yetu kupata Uhuru, kama ilivyo kwa sheria nyingine, kuliundwa sheria mpya ya Hifadhi inayoitwa Ngorongoro Conservation Act (Cap. 284).

Ni miongo kadhaa sasa, wadau wa uhifadhi wamekuwa wakijadili suala la ustawi wa Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na hali yake kubadilika sana ukilinganisha na wakati ilipoanzishwa; hali inayotishia hifadhi kuendelea kuwapo katika hadhi iliyolengwa kisheria na kiikolojia.

Mamlaka ya Hifadhi imekuwa ikitaadharishwa na watafiti, na hata Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), linalosimamia na kuratibu maeneo yenye hadhi ya Eneo la Urithi wa Dunia (World Heritage Site) kuhusu dalili za kupoteza hadhi ya uhifadhi iliyokusudiwa na serikali na wadau wa kimataifa.

Hofu ya hifadhi kupoteza hadhi yake ya uhifadhi kitaifa na kimataifa inatokana na ongezeko kubwa la binadamu, mifugo, makazi, shughuli za kitalii na viumbe vamizi; mambo yanayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ya wanyamapori, mandhari na uoto wa asili.

Ukweli ni kwamba, kwa kuzingatia yanayoonekana, na kwa kujua kuwa viumbe vyote vilivyo ndani ya hifadhi vinazaliana na vina mahitaji ya kuishi yanayoathiri mazingira kadiri vinavyoongezeka, na kwa kutambua pia kuwa utalii usipodhibitiwa nao unaathiri mazingira, ni dhahiri NCA haiwezi kuendelea kukidhi matakwa ya hadhi za uhifadhi kitaifa na kimataifa bila kuchukua hatua madhubuti kubadili mwelekeo wa sasa.

Ni kwa kutambua hali hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan, Februari, 2022 amewapa wahifadhi changamoto kuhusu tishio la kuipoteza Hifadhi ya Ngorongoro na kuwataka wachukue hatua za haraka kuinusuru. Kwa kuitika agizo hilo Mamlaka ya Hifadhi na Wizara ya Maliasili na Utalii zilianza kuchukua hatua za kuhamisha wafugaji kwa hiari, lakini wakataka mkutano na Waziri wa Maliasili kwanza.

Wakati wafugaji wa ndani ya hifadhi wakingojea kukutana na waziri, Loliondo nako wakaja juu kuhusu sehemu ya Pori Tengefu la Loliondo ya kilomita za mraba 1,500 kukatwa kutoka eneo la kilometa za mraba 4,000. 

Wakadai kwamba uamuzi huo unawanyang’anya ardhi ya mababu zao. Malalamiko katika hili yalikuwa pamoja na kushutumu serikali kuwapoka haki za binadamu, kuwaonea, kutowathamini, na kuwafukarisha. Mgogoro huo ulivuta hisia za wengi na kwa vile Bunge lilikuwa limekutana kujadili Bajeti, ikawa pia ni fursa ya kujadili mgogoro huo.

Taarifa zilipokuwa zimemfikia Rais Samia naye akamuagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kukutana na wananchi wa Loliondo, kama ilivyofanywa pia kwa wafugaji wa Ngorongoro.

Hata hivyo, kuwahamisha wafugaji wanaojitolea kuhama kwa hiari ni suluhu ya muda tu. Hii ni kwa vile inaacha wengine ndani ya hifadhi wakiendelea kuzaliana; sambamba na mifugo yao, na wakiwa wameshikilia madai yale yale.

Hii ina maana imepunguza makelele tu kwa muda yatakayokuja kulipuka tena hali ikiwa mbaya. Kwa maneno mengine, malalamiko yamebakia, na uharibifu wa mazingira kupungua kwa muda tu.  

Kwa namna hiyo, hifadhi haiwezi kudumu katika hali inayokidhi matakwa ya sheria na hadhi za kimataifa.

Inaelekea kikwazo kikubwa katika jitihada za serikali kupata suluhu ya kudumu kuhusu madai ya wafugaji hawa ni makubaliano ya sheria iliyounda hifadhi kuyapa masilahi yao kipaumbele dhidi ya yale ya wanyamapori. Tatizo hasa ni kuwapo wafugaji wanaoendelea kukumbatia sheria ya kikoloni na kugomea sheria ya Jamhuri.

Jambo linalogomba katika mgogoro huu ni wafugaji kuona kuwa masilahi yao hayapewi kipaumbele dhidi ya masilahi ya wanyamapori.  

Kwa nyakati mbalimbali masilahi haya yametajwa kuwa ni pamoja na kutohamishwa katika makazi yao ya mababu, kupewa mamlaka juu ya ardhi ya vijiji wanamoishi kama ilivyo kwenye vijiji vya kawaida nje ya hifadhi, kuruhusiwa kulima, kuwezeshwa kiuchumi, kupatiwa huduma zote za kijamii ndani ya hifadhi, ikiwa ni pamoja na barabara nzuri, maji safi na salama, vituo vya afya ya binadamu, huduma za mifugo na kadhalika.

Kwa sheria iliyopo, mengi yanatekelezeka, isipokuwa kutohamishwa, kumiliki ardhi ya vijiji, na kilimo ndani ya hifadhi. Na haya matatu yanakuwa kikwazo kutokana na wafugaji wengine kutokujua au kupenda kutojua masuala muhimu ya uraia. Kuna haja kwa serikali kutoa elimu mahususi kuhusu uraia na uzalendo; na hii si kwa Wamasai wa hifadhini tu, bali wote Tanzania.

Vingineyo Hifadhi ya Ngorongoro haitadumu, na serikali itajikuta inaendelea kujenga ‘nchi ya Wamasai ndani ya nchi ya Tanzania’. Ni muhimu wafahamu na kuzingatia kuwa enzi za Maasai Federal Council zimepita; na kuwa wao ni Watanzania kama Watanzania wa makabila mengine; hivyo wanapaswa kuishi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.

Mwandishi wa makala hii ni Mwanataaluma za Wanyamapori, Mazingira na Maendeleo Endelevu. 

0762-889342 

[email protected]

By Jamhuri