Bashir Yakub

Ndugu yangu Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, tatizo liko hapo TCRA. Hizi kampuni za simu zinafanya biashara, hivyo zinaweza kufanya lolote zisipopata usimamizi.

Tunahitaji kanuni za ‘vifurushi’, kama vifurushi, kutoka hapo TCRA ili zitusaidie. 

Kanuni iliyopo haitambui vifurushi. Hakuna popote katika kanuni yote ya gharama za simu; ‘the electronic & postal communications (tariffs) regulation 2018’ inapotajwa neno kifurushi au kwa Kiingereza ‘bundle’. 

Hii maana yake kampuni za simu hazichukulii kifurushi kama mawasiliano rasmi bali zinaita vifurushi ‘ofa’ au ‘msaada’ tu. 

Mawasiliano yote ya maandishi (ambayo ninayo) na ya mazungumzo (vikao) niliyofanya na kampuni za simu wanaita vifurushi; ofa.

Yaani eti, zile pesa zote tunazotoa kujiunga kwenye ‘internet’, mazungumzo, na SMS wanakuwa wametupa ofa (msaada). Usipokuwa mvumilivu unaweza kumtia mtu ngumi.

Wanasema eti muda wa mawasiliano rasmi ni ule unaotumia pesa/salio la kawaida la kwenye simu bila kujiunga. Ukijiunga kifurushi hiyo ni kitu kingine, ni ofa.

Kinachosikitisha zaidi TCRA nao wanakubaliana na hili jambo kuwa kifurushi ni ofa/msaada. 

TCRA wameniambia mimi hivyo katika vikao nilivyofanya nao kuhusu hili jambo na barua zao ninazo. Wamenijibu wakisema hivyo hivyo.

Kwa msingi huu wa bando kuwa ofa (msaada) maana yake ni kuwa anayetoa ofa ndiye pia hutoa masharti ya ofa. 

Ikiwa utapewa ofa ya ‘lunch’ basi huna uwezo wa kumwambia aliyekupa ofa kuwa lazima na supu ya kuku iwepo.

Vivyo hivyo ndivyo wasemavyo watoa ofa (msaada) ya vifurushi kuwa wewe mnunuzi wa kifurushi mpewa ofa (msaada) huwezi kuweka masharti kuwa kifurushi chako kisiishe muda (expire), bali wao ndio wanaamua hiyo ofa (msaada) itumike vipi.

Kwa hiyo ndugu zangu lile suala letu tunalokataa siku zote kuwa huwezi kuniuzia kifurushi nikakulipa fedha zako zote, halafu ukanizunguka ukakichukua tena kwa mwavuli wa muda wake kwisha, linakwama hapa.

Sasa, ndugu Nape tunaomba utusaidie. Tuwe na kanuni inayotambua vifurushi kama ilivyo kwa salio la kawaida (tariff). Na tabia ya kuita kifurushi tunachonunua kwa jasho letu ofa, ikome.

Kanuni iratibu vifurushi kama vifurushi, iviwekee ulinganifu wa matumizi (rates), uwezo wa kuhamishiana, iondoe muda wa ku-expire, itambue kifurushi kama mali ya mnunuzi, iweke mfumo mzuri wa mtumiaji mwenyewe kuweza kufuatilia matumizi ya kifurushi chake, na mengine mengi mazuri.

Kwa nini kifurushi kihitaji kanuni zake zinazojitegemea? Ni kwa sababu hakuna shaka kuwa kifurushi ndiyo mawasiliano yenyewe kwa sasa hivi. 

Zaidi ya asilimia 90 ya watumiaji wanatumia vifurushi. Wanaotumia salio la kawaida bila kujiunga ni kama hawapo kabisa kwa sasa.

Sasa unawezaje kuwa na kanuni ya kuratibu matumizi ya salio la kawaida ambayo ndiyo tunayotumia, ukakosa kanuni ya kuratibu kifurushi ambacho ndicho matumizi hasa ya simu kwa sasa.

Wakati mwingine tukishitaki kampuni za simu kwa kukata vifurushi kwa kigezo cha ku-expire wamekuwa wakiuliza ni sheria gani waliyovunja. 

Hakuna jibu kwa kuwa hakuna sheria ya kuratibu vifurushi. Ndugu Nape utusaidie hili na limo ndani ya uwezo wako. 

Kuhusu kesi yangu na kampuni za simu pamoja na harakati hizi za mawasiliano, hasa vifurushi  kwa ujumla, ipo na inaendelea, hii ni kwa wale ambao wamekuwa wakiuliza nimefikia wapi.

By Jamhuri