Waziri Nyalandu adanganya

Usanii wa kisiasa unaofanywa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, unazidi kubainika baada ya rafiki zake kumkabidhi hundi hewa ya dola milioni 2.25 za Marekani.

Kiasi hichocha fedha kwa mwaka jana kilikuwa sawa na Sh bilioni 3.668.

Waziri huyo, kwa kushirikiana na rafiki zake wa Kampuni ya Friedkin Conservation Fund inayojihusisha na masuala ya uwindaji wa kitalii, na wanaojitangaza kama wadau wanaopinga ujangili walikabidhiana mfano wa hundi hiyo feki wakati wa kilele cha matembezi yaliyopewa jina la “Walk for Elephant” yaliyoshirikisha watu 18 kutoka Arusha hadi Dar es Salaam (umbali wa kilometa zaidi ya 600).

Nyalandu alipokea mfano huo wa hundi kutoka kwa Mkurugenzi wa Friedkin Conservation Fund, Mitchel Allard. Matembezi yaliratibiwa na asasi ya African Wildlife Trust, inayoongozwa na Pratik Patel. Huyu ni mmoja wa watu wanaozunguka huku na huko ulimwenguni kukusanya fedha kwa madai ya kuzitumia kuwahami tembo dhidi ya majangili.

Patel anatajwa kuwa mmoja wa marafiki wa karibu mno wa Nyalandu, na ambaye wakati mwanasiasa huyo akitangazwa kuwa Waziri kamili, hakusita kuonesha furaha yake kwa kuwakusanya “Friends of Nyalandu” mjini Arusha kusherehekea uteuzi huo uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete.

Pamoja nao, wengine walioshuhudia kituko hicho ni Meneja Maendeleo ya Jamii kutoka Friedkin Group of Companies, Aurelia Mtui; Faraja Nyalandu; Nancy Sumari na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa.

Pamoja naye, alikuwapo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli. Kwa siku za karibuni Lembeli na Nyalandu wamekuwa marafiki wakubwa, kiasi cha kujipanga kuyashitaki magazeti wanayoyatuhumu kuhoji urafiki wao.

Miongoni kwa mambo yaliyowaudhi ni kutibuliwa kwa mpango wa kukodishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Katavi kwa kampuni ya African Parks Network (APN) ya Afrika Kusini ambayo Nyalandu ni mjumbe wa Bodi. Hasira zao sasa wanataka kuzihamishia mahakamani kwa kile kinachoelezwa kuwa ni mkakati wa kuwafunga mikono wanahabari wanaofukua tuhuma mbalimbali ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Akiwa Naibu Waziri wakati huo, alipokea matembezi hayo kuanzia Ubungo na kuyahitimisha katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini humo. Watembezi hao walitumia siku 19.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa baada ya hafla kubwa iliyotangazwa kwa mbwembwe katika vyombo vingi vya habari, Wizara ya Maliasili na Utalii ilijaribu kupata fedha hizo, ndipo ilipobainika kuwa kilichofanywa na hao waliojiita ‘wafadhili’ kilikuwa kiini macho tu!

Baadaye ikabainika kuwa hundi hiyo ilitolewa na kampuni hiyo ya Friedkin na kupelekwa kwa kampuni yake nyingine, huku Nyalandu akitumika kujipatia umaarufu kwa “kufanikisha” kupata fedha za kuiwezesha Serikali kwenye mapambano dhidi ya ujangili!

Hadi wiki iliyopita, Wizara ilikuwa haijapata hata dola moja kutokana na hundi hiyo. Mmoja wa watumishi amesema misaada kadhaa kati ya mingi inayotangazwa na kuoneshwa kwa mbwembwe kwenye vyombo vya habari ni usanii tu.

“Wengi wanatumia njia hii kujipatia umaarufu na kunyoosha masuala yao. Nyalandu ni rafiki mkubwa wa kampuni hii. Alishiriki kuafiki wazo la matembezi hayo kama njia ya kuonesha ana uwezo wa kushawishi na kufanikisha kupata fedha kwa ajili ya kupambana na ujangili. Lengo lake lilikuwa kujiandalia mazingira ya kuwa Waziri,” amesema mmoja wa watumishi kwa masharti ya kuhifadhiwa jina lake.

Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nurdin Chamuya, alipoulizwa na JAMHURI kwa simu alisema, “Nitakupigia, nipo benki kidogo.” Hata hivyo, hakupiga simu. Alipotafutwa, simu iliita bila kupokewa.

Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alipoulizwa, alisema, “Jamani naomba mniache kwa sababu mimi si Waziri tena…Waulizeni waliopo.”

Alipoulizwa zaidi alisema, “Sina kumbukumbu sawa sawa za suala hilo, lakini nadhani hizo fedha hatukuziona, pengine zililetwa nikiwa nimeshaondoka wizarani.”

Urafiki wa Nyalandu na kampuni za Friedkin Conservation Fund ni wa wazi, na sasa Waziri anajitahidi kushinikiza mmoja wa Watanzania wenye asili ya Kiarabu anyang’anywe kitalu ili zipewe kampuni hizo za Kimarekani.

Limekuwa jambo la kawaida kwa kampuni hiyo na nyingine zenye uhusiano nayo, kushinikiza mambo yafanyike bila kufuata sheria na taratibu mradi tu jambo wanaloshinikiza lina maslahi kwao.

Pale wanapokataliwa wamekuwa na tabia ya kusingizia Idara ya Wanyamapori au watumishi kuwa wanawanyanyasa na kwamba wanapokea rushwa.

Wanapata kiburi kutoka kwa Nyalandu na wanasiasa wengine wanaohaha usiku na mchana kuhakikisha wazawa wananyang’nywa vitalu ili wao wapewe.

Baadhi ya watumishi wamekuwa waoga wanapokabiliana na madai ya kampuni hizo, hasa wanapotakiwa watekeleze maagizo bila kufuata misingi ya Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 na kanuni zake za mwaka 2010.

Mifano michache juu ya tabia hii ni pamoja na mgogoro wa Lake Natron Game Controlled Area ambako Kampuni ya Wengert Windrose Safaris (WWS) imekuwa ikilazimisha Idara ya Wanyamapori kuipa kitalu ambacho kiligawiwa kwa kampuni ya Green Miles Safaris (GMS).

Msimamo wa Wizara na baadaye hukumu ya Mahakama ni kwamba madai ya marafiki hao wa Nyalandu hayana msingi.

Hata hivyo, WWS ambao ndiyo hao hao Friedkin Conservation Fund, waliandika barua kwenda Baraza la Congress la Marekani kulalamika kwamba watumishi wa Idara wamekula rushwa na kutoa kitalu chao kwa Kampuni ya GMS ambayo ni ya Kitanzania. Wabunge karibu 20 walitia saini barua kwenda kwa Rais Barack Obama, wakitaka aingilie kati ili WWS wapewe vitalu wanavyovitaka.

Uchunguzi unaonesha kuwa baada ya madai hayo kuchunguzwa na Serikali ya Marekani, ilibainika kuwa ni ya kipuuzi, na hivyo kampuni hiyo ikatakiwa iombe radhi Idara ya Wanyamapori na Serikali ya Tanzania. Serikali ya Marekani ikasema wazi kuwa kampuni hiyo, na nyingine zinapaswa kufuata sheria na kanuni za Tanzania. Hadi sasa maswahiba hao wa Nyalandu hawajaomba radhi kama walivyotakiwa na Serikali ya Marekani.

Kampuni ya WWS imekuwa ikiendelea kufanya fujo kwa wageni wa GMS, hivyo kusababisha wageni hao kuondoka na wengine kufuta safari zao. Hali hii imesababisha Serikali kukosa mapato kwa kuwa shughuli za uwindaji hazikufanyika kabisa katika kitalu hiki.

Baada ya Nyalandu kuona mbinu za kuwaondoa wazawa hao ni ngumu, na hasa baada ya wakurugenzi aliowafitini kumwekea ngumu, sasa ameibuka kwa njia nyingine ya Bunge.

Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Peter Msigwa, anatajwa kama mmoja wa wanasiasa walioanza kupiga zengwe ili kampuni ya GMS iweze kuondolewa kwa madai kwamba inaua wanyama bila kufuata sheria.

Hii ni habari njema kwa Nyalandu ambaye kwa kutumia maneno ya Msigwa, anaweza kuhalalisha kufutwa kwa leseni ya GMS, hivyo kufungua njia kwa rafiki zake Wamarekani wa kampuni za WWS na nyingine kulitwaa eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa wanyamapori.

Msigwa ahoji Sarakikya kuendelea kupeta

Kuna habari kwamba Paul Sarakikya ambaye ameonekana kufeli kwenye vita dhidi ya ujangili, ndiye aliyeandaliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Wanyamapori.

Hata hivyo, Msigwa amehoji weledi na uadilifu wa Sarakikya hata Nyalandu aweze kumpa nafasi ya kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, kabla ya kuondolewa na mamlaka ya uteuzi.

Katika hotuba yake bungeni, Msigwa alisema, “Mheshimiwa Spika, Waziri Nyalandu alitoa taarifa za kuwavua nyadhifa zao Mkurugenzi Mkuu wa Wanyamapori na Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori nyadhifa zao. Nyalandu anadai kuwa moja ya sababu za kuwaondoa ni kutekeleza maazimio ya Kamati ya Lembeli kutokana na kutowajibika wakati wa Operesheni Tokomeza.

“Jambo la kujiuliza, kama aliwahi kusema kuwa taarifa ya kamati ni uongo mtupu, je, ni lini amethibitisha kuwa kile alichodai kwamba ni uongo, ulikuwa ukweli?

“Cha ajabu, aliyeteuliwa kukaimu nafasi ya ukurugenzi, Paul Sarakikya aliyekuwa kiongozi wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na aliyehusika moja kwa moja na kinachodaiwa kuwa uvunjifu wa haki za binadamu, ndiye amepewa nafasi ya kukaimu ukurugenzi! Wote tunafahamu ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu na ukatili uliofanywa katika Operesheni Tokomeza kiasi cha kusababisha mawaziri wanne kuwajibishwa kwa kutenguliwa nafasi zao.

“Mheshimiwa Spika, aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ilitumia vigezo gani kumteua Sarakikya kukaimu nafasi ya Ukurugenzi wa Wanyamapori huku ikijua alivyoshindwa kutokomeza ujangili hapa nchini na jinsi alivyoendesha Operesheni Tokomeza iliyokuwa imejaa dhuluma, uporaji, utesaji na udhalilishaji dhini ya wananchi. Jambo ambalo liliishangaza zaidi Kambi Rasmi ya Upinzani ni kitendo cha Waziri Nyalandu kumteua Ndugu Sarakikya kukaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori huku akijua kuwa Sarakikya alifanya makosa mengi katika utendaji wake wa kazi katika Idara hiyo ya Wanyamapori.

“Mheshimiwa Spika, ikumbukwe pia kuwa Ndugu Sarakikya ndiye aliyeongoza Kikosi cha Kuzuia Ujangili hata kabla ya Operesheni Tokomeza. Katika kipindi hicho, Tanzania ilishika nafasi ya kwanza kati ya nchi nane duniani zilizoongoza kwa matukio ya ujangili. Aidha, ili kuonyesha kwamba Serikali hii haizingatii weledi katika utendaji, alietuliwa tena kusimamia Operesheni Tokomeza.”