Na Sabiha Khamis, Maelezo Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Dkt. Saada Mkuya Salum amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi vikosi vya SMZ ili  kuendelea kuimarisha ulinzi na usalama nchini.

Akizungumza katika ufunguzi wa mahanga na ofisi za Kikosi cha Valantia (KVZ) kambi ya  Mwanyanya Wilaya ya Magharib “A” ikiwa ni shamrashamra za kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar amesema kufanya hivyo kutasaidia vikosi hivyo ikiwemo KVZ kuimarisha jukumu lao la  msingi la kulinda  raia na mali zao na  kuzidisha doria katika maeneo hayo na nchi kwa ujumla.

“Kumekuwa kunajitokeza makundi hatarishi katika maeneo haya ya msitu kunakuwa na vijana watukutu  ambao hufanya vitendo vya uhalifu na kuhatarisha maisha wa wakaazi wa maeneo ” amesema Dkt. Saada.

Alifahamisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha  maslahi ya watendaji wa vikosi hivyo na kuwaejenga mazingira bora pamoja na  kuvijengea uwezo vikosi hivyo  juu ya dhana ya  kujiendeleza kiuchumi ili kuleta maslahi na kupiga hatua za maendeleo  ikiwa ni katika utekelezaji wa  ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Ameeleza kuwa Vikosi hivyo vimekuwa vikifanya kazi nzuri kwa miaka  mingi lakini katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya nane chini ya  Dkt. Mwinyi vikosi hiyvo vimefanya kazi nzuri zaidi katika kujiinua kichumi ikiwemo Kikosi cha Valantia (KVZ).

“Miaka yote vikosi hivi vimekuwa vikifanya vizuri katika majukumu yake lakini kwa miaka hii mitatu ya Dkt. Mwinyi vimefanya vizuri zaidi” alisema Waziri.

Hata hivyo amewasisitiza wapiganaji hao kuwa waaminifu katika kutunza siri ili kuepusha changamoto katika sehemu za kazi pamoja na kuandaa utaratibu mzuri wa kuwapa hamasa watoa taarifa ambao ni wananchi wanapotoa taarifa za kiusalama ambazo zisaidia kudhibiti vitendo viovu na kusisitiza kuwa na usiri mkubwa kwa watoa taarifa hao.

Vilevile amewashauri kikosi hicho kuanza kujenga majengo ya ghorofa kwani kila maendeleo yanapopatikana na idadi ya askari inaongezeka na kuzungusha ukuta katika eneo hilo ili  kuliepisha uvamizi .

Akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu ujenzi wa mahanga na ofisi za KVZ kambi ya Mwanyanya  Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya RaisTawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Issa Mahfoudh Haji amesema zaidi ya Milioni 600 zimetumika kumlipa Mzabuni kwa ajili ya vifaa vya ujenzi huo.

Amesema ujenzi huo unahusisha majengo manne ikiwemo nyumba mbili za Maafisa, Hanga moja kwa ajili wa wapiganaji na Afisi moja kwa ajili ya kazi za utawala  ambapo nguvu kazi ya kikosi cha KVZ  ilitumika katika  kukamilisha ujenzi.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza ari na bidii ya utendaji kazi kwa maafisa na wapiganaji wa kikosi hicho sambamba kupunguza changamoto ya majengo ya kisasa ya kiutawala na malazi.

Kwa upande wake mkuu wa Kikosi cha Valantia (KVZ) L.T Kanal Said  Shamhuna amesema kukamilika kwa mradi huo kutatoa huduma mbalimbali kwa  jamii  ikiwemo huduma za maji safi na salama, afya pamoja na huduma za ulinzi na usalama ambazo zitasaidia kutokomeza vitendo vya kihalifu pamoja na  unyanyasaji wa kijinsia.

Amesema mradi wa ujenzi huo katika kambi ya Mwanyanya  umekwenda sambamba na ujenzi wa majengo kama hayo  katika kambi za Muyuni na Kikungwi zilizopo mkoa wa Kusini Unguja na Mto wa maji kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Wziri wa Nchi (OR),fedha na mipango dkt.Saada Mkuya Salum akikagua Ofisi ya kikosi cha valantia Zanzibar  kambi ya mwanyanya kabla ya kufungua   mahanga na Ofisi hiyo  katika shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi.

Waziri wa Nchi (OR),fedha na mipango dkt.Saada Mkuya Salum  akikata utepe kuashiria ufunguzi  wa mahanga na Ofisi   ya Kikosi cha valantia (kvz) kambi ya  mwanyanya ,mradi  uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 600 katika shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi.

Waziri wa Nchi (OR),Fedha na Mipango dkt.Saada Mkuya Salum akikunjua kitambaa kuashiria UFUNGUZI wa Ofisi na  mahanga ya  kvz  kambi ya mwanyanya katika  shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi. 

Waziri wa Nchi (OR),Fedha na Mipango dkt.Saada Mkuya Salum akihutubia mara baada ya kufungua Ofisi na mahanga ya  Kikosi cha valantia  kvz kambi ya mwanyanya katika  shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi 

Mkuu wa kikosi cha kvz luteni kanal Saidi Shamhuna  akizungumza machache wakati wa ufunguzi wa mahanga na Ofisi za Kambi za Kvz Mwanyanya uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 600 katika  shamrashamra za kutimiza miaka 60 ya Mapinduzi 

PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANIBAR

By Jamhuri