Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amewahakikishia wakulima na wafugaji zaidi ya 120 kutoka Kijiji cha Loksale Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha kuwa malalamiko yao ya kuchukuliwa ardhi ekari 47,000 na serikali kwa ajili ya matumizi ya jeshi linashughulikiwa na muda si mrefu watalipwa haki zao kwa mujibu wa nyaraka zilizopo ofisni kwake.

Awali mashamba ekari 47,000 yaliyopo Loksale yalikuwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji kwa wakazi wa eneo hilo na Mkoa kwa ujumla, lakini mwaka 2003 serikali ilibadilisha matumizi na kuwa eneo la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Wizara ya Ulinzi na jeshi la Kujenga Taifa liliahidi kuwalipa fidia wote waliokuwa na hati ya kumiliki baadhi ya mashamba, lakini hadi sasa hawajalipwa.

Akizungumza katika kliniki ya kutatua changamoto za migogoro mkoani Arusha,Waziri Silaa alimwambia Katibu wa wakulima hao Joseph Ngaluko na wenzake kuwa suala lao analijua na liko sehemu nzuri kupata haki yao.


Amemwagiza Kamishina wa Ardhi mkoani Arusha kuhakikisha anafuatilia suala hilo, ili wakulima hao waweze kupata haki yao ya fidia.

‘’Msiwe na wasiwasi serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan haiwezi kudhulumu haki ya mtu, kwani serikali iko katika kuangalia kuwa mwenye haki ya ardhi yake anapata stahiki yake kwa mujibu wa nyaraka zake na kama serikali ilichukua eneo hilo kwa nini msilipwe.

‘’Nakuagiza Kamishina fuatilia suala hili hadi mwisho, ili wakulima hawa wapate haki yao kwani ni muda mrefu sana wanahangaikia haki yao, hivyo ni muhimu ukawasaidia wapate wanachostahili kupata,’’ amesema Waziri Silaa.

Naye Kamishina wa Ardhi Mkoa wa Arusha,Godfrey Mwamasojo amesema atalifuatilia suala hilo kama alivyoagizwa, ili wakulima hao waweze kupata stahiki zao.

Kwa upande wake Ngaluko alimshukuru Waziri Silaa kwa hatua hiyo na kusema wana imani na serikali, kwani wana hati ya ardhi ya umiliki wa mashamba hayo iliyotolewa mwaka 1990 na Halmashauri ya wilaya ya Monduli na wana nyaraka za nakala za barua zinazoonesha wanapaswa kulipwa fidia, baada ya serikali kubadilisha matumizi ya ardhi hiyo

By Jamhuri