Na WAF, DODOMA

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameitaka jamii ya watanzania kutumia dawa kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kuondokana na changamoto ya usugu wa vimelea vya dawa mwilini (UVIDA)

Waziri Ummy ametoa wito huo Juni 12,2024 jijini Dodoma wakati wa mazungumzo maalum na Balozi wa Kampeni ya Holela Holela itakukosti Bwana Kido, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kutumia dawa kulingana na maelekezo ya Madaktari.

Waziri Ummy amesema kutokana na mtindo usiofaa wa watu kutumia dawa bila ushauri wa wataalam pamoja na kutomaliza dozi kwa usahihi kumeibua changamoto ya vimelea vya magonjwa kuwa sugu kutokana na matumizi ya dawa kiholela.

“Suala hili ni tatizo kubwa, tumeona kuna athari kwanza mgonjwa anachelewa kupona, unaweza kuzidi kuumwa na unaweza ukapata kifo, madhara mengine ni ya kiuchumi ukipata dawa mapema unarudi katika biashara zako,” ameeleza Waziri Ummy

Waziri Ummy ameongeza kuwa changamoto kubwa ni kutozingatiwa kwa matumizi sahihi ya dawa kulingana na maelekezoya daktari.

“Ukiandikiwa dawa hakikisha unamaliza dozi yote, kama siku tano maliza siku tano kama umeandikiwa siku saba maliza siku saba,kama ni 2×3 hakikisha unatumia ndani ya saa 24 watu wanatumia dawa bila ushauri wa madaktari,”amesema Waziri Ummy.

Pia amewataka wananchi kujizuia kutumia dawa bila kupata ushauri wa daktari hasa dawa za Antibaotiki.

“Ukiandikiwa dozi ukiambiwa dawa kunywa siku saba basi ikamilishe sio kwamba umeona siku mbili mambo yamekaa vizuri unaacha maliza dozi, Usitumie dawa ambazo ulitumia katika ugonjwa uliopota, Usitumie dawa ambazo ameitumia mtu mwingine nenda kwa daktari upate ushauri,” ameshauri Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amewaomba wataalamu wa afya wakiwemo wafamasia kuzingatia miongozo na taratibu za utoaji dawa.

“Kama kuna dawa unatakiwa kutoa kwa kuzingatia cheti cha daktari usimpe mgonjwa hakikisha unampa dawa ambayo imeandikwa na daktari,”amesisitiza Waziri Ummy.

Amesema Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na utumiaji wa dawa kiholela na utunzaji wa mazingira.