Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali,Mobari Matinyi amesema wizara 13 za Serikali zimeshiriki katika kufanikisha kazi ya kurudisha hali ya waathirika kutoka Hanang mkoani Manyara.

Ambapo amesema moja ya wizara iliyotumika ni wizara ya ardhi, nyumba na makazi ambapo wametumia sensa ya watu na makazi iliyofanyiwa Agosti mwaka 2022 kutambua makazi kulingana na hali ilivyotokea nyumba 100 zimebainika kusambaa kabisa.

Matinyi amesema hayo jana kwenye Mkutano Mkuu wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC) uliokutanisha klabu 28 ikiwa 26 kutoka Tanzania Bara na mbili Visiwani alipokuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo huku akipokea pole iliyotolewa na Rais wa UTPC kuhusisha na janga lililotokea eneo la Hanang mkoani Manyara ambalo limeleta historia .

Matinyi amesema kazi ngumu imefanyika Hanang kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuleta misaada ikiwa kulikuwa na majeruhi 139 hospitalini lakini mpaka sasa kumebaki majeruhi 30.

“Tope hilo lilikuwa likikimbia kilomita 6.1 lilikuwa likipitia nyumba moja na kuikumba nyingine chanzo kimechunguzwa na kubainika kuwa mchanga laini uliokuwa umejibumba na kuunda mlima ulikuwa unaloaana taratibu na mvua iliyokuwa imenyesha sio kubwa” amesema Matinyi.

Matinyi amesema mpaka sasa kuna ripoti ya vifo 87 na waliobahatika kupona wanasimulia hadithi za kusikitisha na namna walivyo okolewa.

Matinyi amesema serikali kwa sasa imerudi kwa mpango mkakati wa kutarajia kuwapatia vifaa vya ujenzi na kazi iliyofanyiwa niya utu na uzalendo mkubwa.

Matinyi alisema kila kitu kikitokea kina fundisho lake ambapo watu wamepigwa marufuku kuweka makazi bali wameruhusiwa kuwa umbali wa kilomita 30 ili wasipate madhara tena kama yalivyotokea.

Rais wa muungano wa klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC), Deogratius Nsokolo ametoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kufuatia majeruhi na vifo vilivyowakuta watu wanaoishi Hanang mkoani Manyara.