Na Mwandishi Wetu, London

Timu ya Wataalam wa Wizara ya Madini ikiongozwa na Katibu Mkuu Kheri Mahimbali inashiriki katika Jukwaa Maalum la Biashara kati ya nchi ya Tanzania na Uingereza.

Wataalam wa Wizara ni sehemu ya ujumbe maalum wa Serikali ya Tanzania unaoshiriki jukwaa hilo lililoanza Novemba 20, 2023 jijini London ambao pia unahusisha wafanyabiashara kutoka Tanzania.

Akizungumzia kuhusu ushiriki wa Sekta ya Madini kwenye jukwaa hilo, Katibu Mkuu Mahimbali amesema Wizara inatarajiwa kufanya wasilisho maalum litakalotoa wasaa wa kueleza fursa za kuwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini nchini hususan kwenye madini muhimu na mkakati.

Mahimbali ameongeza kwamba, pia, Wizara inatarajia kufanya mkutano na Taasisi ya Jiolojia ya nchini Uingereza ambao unalenga katika kuimarisha uhusiano na maeneo mapya ya ushirikiano na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

‘’ Tutakutana na kampuni za kiingereza zenye nia ya kuwekeza nchini Tanzania, pia tutashiriki kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania tulioambatana nao na wafanyabiashara wa nchini Uingereza hususan wenye nia ya kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani madini’’, amesema Mahimbali.

Wizara ya Madini inaendelea kutekeleza mikakati yake ikiwemo moja ya vipaumbele vyake vya kuendeleza madini muhimu na mkakati ambapo katika Mwaka wa Fedha 2023/24 wizara imepanga kutekeleza vipaumbele hivyo kwa kufanya utafiti na kutangaza fursa za kiuwekezaji zilizopo; kuhamasisha uwekezaji katika utafutaji uchimbaji wa madini mkakati na madini muhimu; kutoa leseni za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini mkakati na madini muhimu; na kuandaa Mpango Mkakati wa uendelezaji wa shughuli za uchimbaji wa madini muhimu nchini.

Aidha, kupitia Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri kupitia GST Wizara inapanga kufanya utafiti wa kina kwa njia ya ndege (Geophysical Airborne Survey) kwa angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030. Kimsingi, taarifa za utafiti ndizo zinazoshawishi uwepo wa uwekezaji na hivyo kuwezesha uwekezaji wa uhakika.

Kufuatia umuhimu wa Sekta ya madini katika maendeleo ya kiuchumi na kufuatia umuhimu wa jukwaa hilo kwa sekta, Mahimbali ametoa wito kwa wadau na watu wengine waliopo nchini humo wenye nia ya kuzungumza na timu ya wizara kuweza kufanya hivyo.

‘’ Pia, tungepata maoni mbalimbali hususan ndugu zetu Diaspora ili tubadlishane mawazo na ujuzi utakaosaidia kuleta mabadiliko nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla katika mnyororo mzima wa thamani madini’’, amesisitiza Mahimbali.

Aidha, kutokana na umuhimu wa jukwaa hilo kwa sekta ya madini, Mahimbali ametoa pongezi kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida kwa kuandaa ujumbe wa Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ukiongozwa na Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki pamoja na kampuni ya Clyde & Co Tanzania iliyoshiriki kuratibu ujumbe wa Tanzania nchini humo.

*Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri*

By Jamhuri