Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Wizara ya Maji imeingia mkataba wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 134 na Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Maji katika miji ya Rorya na Tarime, mkoani Mara.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini ya utekelezaji wa mradi huo jijini Dodoma, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kazi hiyo inatarajiwa kuchukua miezi 30, lakini akamtaka mkandarasi atumie muda mfupi zaidi kukamilisha kazi hiyo.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kulia) pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga katika hafla ya utiaji saini wa utekelezaji wa Mradi wa Maji katika miji ya Rorya na Tarime, mkoani Mara

Waziri Aweso amesema mradi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kumaliza kero ya maji kwa wananchi wa mkoa Mara na kuuomba uongozi na wananchi wa mkoa huo kutoa ushirikiano ili mradi huo uweze kukamilika haraka na kwa ufanisi.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema mradi huo utahusisha kazi za ujenzi wa chanzo cha maji, chujio la kutibu maji, ulazaji wa mabomba makubwa ya kusafirisha na kusambaza maji, ujenzi wa matenki, vituo vya kusukuma na kuchotea maji.

Mhandisi Sanga amesema ujenzi wa mradi huo utachukua muda wa miezi 30 na utanufaisha wananchi 460,885 katika halmashauri za Rorya na Tarime.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (katikati) akishuhudia utiaji saini wa mkataba kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya China Civil Construction Corporation, Zhang Junle kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Maji katika miji ya Rorya na Tarime, mkoani Mara.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation, Zhang Junle amesema kuwa wana uzoefu wa utekelezaji wa miradi mingi mikubwa ya maji nchini kama Magu, Lamadi na Ngudu.

Akiishukuru Serikali kuiamini kwa kuwapa kazi hiyo, akisisitiza kuwa watafanya kazi hiyo kwa wakati na ufanisi mkubwa.

Wakati huo huo, Mbunge wa Rorya, Jafari Chege ameishukuru Serikali kwa kuchukua hatua ya kutatua kero ya majisafi na salama kwa wananchi wa Rorya na kuahidi ushirikiano katika hatua zote za utekelezaji wa mradi huo.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (wa kwanza kulia) akiwa pamoja na wabunge wa majimbo ya Rorya, Jafari Chege (katikati) na Tarime, Mwita Waitara ambao ni wanufaika wa utekelezaji wa Mradi wa Maji katika miji ya Rorya na Tarime, mkoani Mara.

Pia, Mbunge wa Tarime Mwita Waitara amesema kuwa mradi huo utakuwa ni mkombozi mkubwa kiuchumi katika Halmashauri ya Tarime kwa kuchochea shughuli za maendeleo katika halmashauri hiyo.

By Jamhuri