Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo ameelezea mafanikio ya miaka 60 ya Muungano kuwa Wakati Tanganyika na Zanzibar zinaungana, usalama wa chakula ulikuwa asilimia 60 huku lengo la nchi lilikuwa ni kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 100 na kuwa na akiba.

Prof. Mkumbo ameeleza hayo leo Aprili 17,2024 Jijini Dodoma kwenye mkutano wake na waandishi wa habari na kueleza kuwa kwa sasa nchi ina usalama wa chakula kwa asilimia 124 na kwamba hatua ya kwanza kujipima katika maendeleo ni kuwa na usalama wa chakula.

Amesema ,katika miaka 60 ya Muungano, Tanzania kama nchi,inapambana kuhakikisha kwamba muungano huo unadumu ikiwa ni pamoja na kutilia mkazo suala la kulinda amani, utulivu na mshikamano mambo ambayo yanaonekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Mafanikio kama nchi, tunazungumzia uhai wa taifa,sisi kama taifa hatua ya kwanza ya kujipima katika miaka 60 ya muungano ni uhai wa muungano wetu,hatua ya pili kujipima katika maendeleo ni ustawi wa watu na nchi kwa kuangalia mambo ya msingi ya kibinadamu ikiwemo chakula, mavazi na malazi ambayo nayo tumepiga hatua kubwa, “amesema

Ameeleza kuwa, ” Wakati tunapata Uhuru, umri wa kuishi kwa Mtanzania ilikuwa wastani wa miaka 32, mwaka 2000 umri wa kuishi ukasogea hadi wastani wa miaka 52.,tamaa yetu ifikapo mwaka kesho 2025 wastani wa kuishi uwe miaka 68,Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, wastani wa kuishi ni miaka 66,”amefafanua.

Amefafanua kuwa mambo matatu ya kukuza ustawi wa binadamu ni kumpa binadamu elimu ili aweze kuishi vizuri ambapo mwaka 2000 nchini Tanzania, kiwango cha kuandikisha wanafunzi kilikuwa asilimia 69.

“Kwa malengo tuliyojiwekea kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, ni kufikia asilimia 100 ya uandikishaji wa wanafunzi ambapo hadi sasa tumevuka malengo, tupo asilimia 108.5,” amesema.

Kuhusu suala la mafanikio ya elimu amesema mwaka 1964 ilikuwa asilimia 5 ya watu wanafika elimu ya Sekondari ambapo mwaka 2000, watoto waliofanikiwa kufika sekondari kutoka shule za msingi ilikuwa chini ya asilimia 20 lengo ifikapo mwaka 2025, kuwe na asilimia 48 na kwa takwimu za hivi sasa, tupo asilimia 70.

“Dira ya Maendeleo ya Taifa inayokuja, tutahitaji elimu ya msingi Tanzania iwe kwa Watanzania wote na wote lazima kufika sekondari kwa asilimia 100,eneo la pili la kukuza ustawi wa binadamu ni afya hasa kwenye eneo la mama na mtoto, na la tatu ni maji ambapo wakati tunapata uhuru, uwepo wa maji vijijini ulikuwa chini ya asilimia 15 na mwaka 2000 ilikuwa asilimia 32. Kwa sasa ni asilimia 77,”amesema

Waziri huyo pia ameeleza kuwa Tanzania inahitaji uwepo wa uchumi na kukua kwa uchumi na kwamba ili nchi ione inapiga hatua ni lazima iangalie uchumi unaendaje.

“Wakati wa Uhuru ilikuwa ni kilimo peke yake, lakini katika miaka takriban 20 iliyopita, uchumi wetu umekuwa ukikua vizuri kati ya wastani wa asilimia sita mpaka saba,tuna mengi ya kujivunia katika muungano, tumefanikiwa kuzikabili na kuzitatua changamoto zilizojitokeza,”ameleeza Prof. Kitila

Please follow and like us:
Pin Share