Dar es Salaam

Na Andrew Bomani

Kitabu cha maisha ya mzee Ali Hassan Mwinyi kilichozinduliwa hivi karibuni hakika kinathibitisha umuhimu wa viongozi wa nchi kuwa na tabia ya kuandika vitabu kuhusiana na uzoefu waliopata wakiwa madarakani.

Kwa vyovyote vile nafasi ya rais inaambatana na mambo mazito ambayo ni vizuri kuyasikia moja kwa moja kutoka kwa mhusika. 

Nadiriki kusema hata ubahatike kupata muda gani wa kuzungumza na kiongozi wa juu wa zamani, hakufanani na maelezo kwa njia ya maandishi.

Bahati nzuri, juzi tu Spika wa zamani wa Bunge, mzee Pius Msekwa, katika makala yake ya kila wiki kwenye Daily News, aliianza kwa kutumia maneno ya Kilatini “verba volant, scripta manent”, ikiwa na maana ‘kinachozungumzwa huweza kusahauliwa na kupotea, lakini kilichoandikwa hudumu milele.’ (Tafsiri yangu).

Katika kuanza mapitio ya kitabu cha mzee Mwinyi, nimeona sehemu nzuri ya kuanzia ni kwa kumnukuu mwenyewe kuhusiana na alichokuwa anakiamini: “Mageuzi tuliyoyafanya na ‘rukhsa’ tulizotoa ni mambo ambayo hayakutanguliwa na falsafa kubwa au mijadala ya itikadi. 

“Mie si mtu au kiongozi wa aina hiyo. Nilichojua ni kuwa ilikuwa wajibu wangu kupunguza mateso ya wananchi na kuondosha vikwazo vya uchumi kukua na nchi kuendelea. 

“Nilikuta wananchi wanateseka kwa kukosa bidhaa na mahitaji muhimu kama vile chakula na mavazi, zikiwamo nguo za ndani, sabuni na dawa za mswaki, karatasi za chooni na pedi za kujihifadhi kina mama, na kadhalika. 

“Kwa kutambua kuwa serikali haina fedha za kuagiza mahitaji ya kuwatosha wananchi, nikasema ‘rukhsa’ kwa mwenye fedha zake kuagiza na kuuza. Taabu ya wananchi ikaishi mpaka uchumi na biashara vilipotengemaa.”

Kwa kweli, hali ya nchi kiuchumi wakati mzee Mwinyi anakuwa rais mwaka 1985 ilikuwa mbaya mno hadi gazeti moja la kimataifa linaloheshimika la International Herald Tribune, la Julai 14, 1992, liliandika yafuatayo: “Tanzania kwa vyovyote vile ni nchi ya kuhuzunisha sana kutokana na kuwa imefurahia miaka 30 ya amani na msaada mkubwa wa kigeni, lakini uchumi umeharibiwa na usimamizi mbovu wa ujamaa. 

“Mji wake mkuu wa Dar es Salaam umechakaa vibaya zaidi kuliko Hanoi, mji mkuu wa Vietnam. Miundombinu ya barabara ilikuwa ni mbovu kupita maelezo, simu zilikuwa hazifanyi kazi, upatikanaji wa umeme ulikuwa wa kusuasua na upatikanaji wa bidhaa madukani ulikuwa ni hafifu. Tanzania ilikuwa nchi ya tatu kwa umaskini duniani.” (Tafsiri yangu).

Mfano mmoja unaotolewa na  mzee Mwinyi kuhusiana na mateso ya wananchi ni Kiwanda cha Bia Tanzania. Anaandika: “Watu wa Dar walifikia hatua ya kufuata bia hadi Kibaha wakisikia zimeonekana huko.”

Anaongeza: “Enzi zile ukifika mahali kuna bia, ama kwenye baa au kwenye harusi, basi mtu huchukua bia nyingi awezavyo na kuzificha chini ya kiti.

“Mahali pengine kama wewe si mtumiaji wa kilevi bado ilibidi uende baa kupata kinywaji baridi (soda), lakini sharti lake wewe mnywa soda hupewi glasi na utalazimishwa kununua pombe kali ya viroba, kama vile Konyagi. Unanunua na kuwagawia wengine au kutupa mbele ya safari.”

Mzee Mwinyi hakusita kufafanua: “Wapo wasiojua, au wanaolaumu sera ya Ujamaa na Kujitegemea kwa matatizo yote yaliyotupata miaka hiyo…hasa kiini cha tatizo si nadharia yenyewe ya Ujamaa, bali utekelezaji wake ambao haukufikia kiwango cha utendaji ambacho muasisi wake, Mwalimu Mwalimu Nyerere alitarajia.”

Hakika hatua za dharura zilihitajika kuwapa ahueni wananchi na matokeo yalianza kuonekana ndani ya kipindi si kirefu sana. Sina budi sasa niseme kuwa kadiri nilivyoendelea kusoma maelezo mbalimbali ya mzee Mwinyi hadi anamalizia kipindi chake cha pili mwaka 1995, nilijikuta kwa masikitiko namkumbuka mwanasiasa mmoja maarufu wa zamani nchini Uingereza, Enock Powell, ambaye alipata kusema: “Maisha yote ya kisiasa, endapo hayatafupishwa katikati katika hali ya furaha, huishia katika kushindwa, sababu hiyo ndiyo asili ya siasa na mambo ya wanadamu.” (Tafsiri isiyo rasmi).

Hii kauli inawahusu wanasiasa wengi sana duniani.

Kwa jinsi mzee Mwinyi anavyoeleza mazingira yaliyomwezesha kupeperusha bendera ya CCM baada ya Mwalimu Nyerere kustaafu, naamini alipaswa kuitumikia nafasi ya rais wa Tanzania kwa kipindi kimoja tu!

Na hakuficha hata kidogo bahati iliyomkuta kuanzia kuwa rais wa Zanzibar. Na fikirieni hadi alitoa mfano wa ‘kichuguu na Mlima Kilimanjaro’, ni kwamba alikuwa sawa na kiongozi wa mpito. Na mpito kwa kawaida ni miaka michache.

Vilevile, kwa mtu ambaye hakusukumwa na masuala ya falsafa au nadharia, kuongeza kipindi cha pili bila shaka kingemaanisha kukutana na mawimbi makali ambayo pengine yangemzidi nguvu.

Hapo hapo, utaratibu uliokuwapo wa CCM ulikuwa wa kushangaza hadi mtu kama Mwalimu Nyerere mwenye upeo wa kipekee kuhusu nafasi ya chama kama wakala wa mabadiliko, kuendelea na uenyekiti badala ya kukabidhi mapema kabisa. 

Yaani nionavyo ilibidi mwaka 1984, takriban mwaka moja kabla ya kustaafu, awe na mrithi wake tayari chamani halafu ya serikali ingefuata.

Kwa maneno mengine ni kama Mwalimu Nyerere hakuwa na mrithi ndani ya CCM kwani uongozi wa kisiasa huanzia kwenye chama na ilibidi mzee Mwinyi awe amehusika vya kutosha katika kuandika ilani ya mwaka 1985. Kiuhalisia huwezi kuzungumzia mageuzi makubwa au hata mapinduzi bila kuanzia awali kabisa kwenye chama!

Ni kichekesho mzee Mwinyi akiandika: “Ndiyo maana mwaka 1986 Serikali ya Awamu ya Pili ikapewa ruhusa na CCM kuanzisha mageuzi ya mfumo wa uchumi.”

Kwa maelezo mengine ya mzee Mwinyi, ni wazi alikuwa na wasiwasi na makundi mengine ndani ya CCM: “Mimi na Mwalimu tulishakubaliana kuwa aendelee kuwa mwenyekiti kwa miaka mingine mitano ili mimi nitumie muda wangu wote kushugulikia vipaumbele ndani ya serikali. Lakini pamoja na hayo, nilishachoshwa na maneno yaliyokuwa yanaenezwa na baadhi ya waliojiona ndio mhimili wa ujamaa baada ya mimi kuonekana kushabikia uchumi unaoshirikisha sekta binafsi, hivyo siwezi kuaminiwa kuulinda ujamaa. Nikaona bora Mwalimu abaki nao huo uenyekiti wa CCM na kujaribu kuwatuliza wakati mimi ninaendelea na kazi ya kuinua uchumi na kushugulikia kero halisi za wananchi.” 

Lo! Hapo hapo kuhusu nafasi ya Mwalimu Nyerere, ilifikia hatua gazeti moja la kila wiki la Kanisa Katoliki la Kiongozi, liliandika ‘ni kweli kuwa Mwalimu anaweza kutoa mchango muhimu kutokana na uzeofu wake, lakini wakasema anaweza kutoa mchango huo kama raia wa kawaida, na si lazima awe mwenyekiti ndipo atoe ushauri.’

Hatimaye Mwalimu Nyerere aliaachia uenyekiti wa CCM mwaka 1990 na mzee Mwinyi kumrithi. Wakati huo vuguvugu lilianza kuhusiana na nchi kurejea kwenye mfumo wa vyama vingi au la. Mwalimu Nyerere alikuwa mstari wa mbele kujenga hoja kuwa nchi hii si kisiwa pamoja na kutoa angalizo kuhusu athari ya vyama vingi.

Binafsi ninaamini kwa dhati mzee Mwinyi angekuwa mwana falsafa nchi ingefaidika sana katika kurutubisha hoja zilizokuwapo. Kwa mfano, mzee Mwinyi angeweza kutupa jicho la aina yake katika uhusiano wa karibu baina ya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa na ingebidi kutoharakisha kubadili mfumo huo wa muda mrefu.

Katika kufafanua maana yangu, nitarejea kwenye kamati ya CCM iliyoteuliwa Oktoba 1990 kushauri juu ya mageuzi na ambayo iliongozwa na marehemu Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Bakari Mwapachu. Kama kawaida nchini Tanzania, taarifa kama hiyo inakuwa mtihani kujulikana na watu wengi, wakiwamo viongozi wakuu.

Nikinukuu sehemu ya kwanza: “Kuwapo kwa uchumi mzuri pia kutafanya hata vyama vitakavyoanzishwa kuwa vya kweli na si miradi ya viongozi na wanachama wake kupata njia ya kuendeleza maisha.

Sehemu ya pili: “Vyama vitakavyoanzishwa vitakuwa na nafasi nzuri ya kuwa na wanachama watakoendesha chama chao wenyewe bila kutegemea wafadhili wachache au misaada ya chini chini na ya vificho kutoka nje.”

Hivi kweli kuna mtu makini ambaye angepuuza maneno hayo? Sasa matokeo ya kutoyafanyia kazi ni wazi leo hii kwa kila mwenye macho. 

Sasa tukiangazia kidogo taarifa ya Nyalali, mzee Mwinyi anasimulia mkutano wake wa mashauriano na marehemu Kingunge Ngombale-Mwiru, ambapo alimwambia Ngombale-Mwiru yaliyokuwapo katika ripoti na mapendekezo yaliyotolewa na tume. 

Ngombale-Mwiru akawa upande wa kuruhusu mfumo wa vyama vingi na mzee Mwinyi alimjibu: “Vema, lakini tunafanyaje wakati walio wengi wanataka mfumo uliopo uendelee?”

Hii ninakubali ilikuwa ni changamoto, ila ninarudia kusema kauli yangu ya awali kuwa kama mzee Mwinyi angekuwa mwana nadharia tangu mwanzo, ingesaidia kwa kiasi kikubwa kuongoza mchakato huo mzima na mzito. 

Mwisho wa siku kwa ushawishi mkubwa wa Mwalimu Nyerere na watu wengine wachache, CCM ilikubali kurejea kwenye mfumo wa vyama vingi.

Katika kuhitimisha mjadala wa kubadili mfumo, mzee Mwinyi anafafanua kuwa: “Kwa ujumla Mwalimu Nyerere alifurahishwa na mchakato na mapendekezo. Tulishindana naye kwenye jambo moja tu – la wagombea binafsi. 

Yeye alitaka wawepo, lakini wengi kwenye chama na serikali walihofu, kwa haki kabisa, kuwa hiyo itakuja kuidhoofisha CCM, pale wasiopita kwenye mchujo wakiamua kusimama kama wagombea binafsi. 

Aidha, tulijitahidi kufanya iwe vigumu kwa vyama kuungana, tukasema wakitaka kuungana lazima wajifute kwanza na kisha kuanza na kujisajili upya. 

Lengo la hatua hizi mbili halikuwa kuipendelea CCM, bali kuimarisha msingi wa mfumo wa vyama vingi. Ukiendekeza wagombea binafsi na vyama kuungana kirahisi unaishia kudhoofisha vyama kama taasisi muhimu na mhimili wa siasa za ushindani. 

Badala ya kujiimarisha kama taasisi na kujiandaa kuwa serikali mbadala, vitakuwa vinatafuta mbinu tu kushinda uchaguzi. Hatimaye kutakuwa hakuna vyama madhubuti, bali mashirikiano tu kwa ajili ya kutafuta ushindi kwenye uchaguzi. Katika mazingira hayo ya vyama dhaifu, hata kusimamia nidhamu ndani ya vyama itakuwa taabu.”

Hii nukuu kwa haraka inaonekana ni nzuri sana lakini inaashiria matatizo ambayo hadi sasa yanatukabili kama taifa. Kwanza, kuhusu mgombea binafsi, haiingii akilini kabisa kwenye mfumo wa vyama vingi kuzuia kama si kwa masilahi ya chama tawala tu. 

Kama kweli kuna jambo moja la kisiasa ambalo mzee Mwinyi alipaswa kuonyesha kwa vitendo kuwa yeye ni ‘Mzee Rukhsa’ ni hapo. Matokeo ya kuzuia ni suala hilo kujikuta mahakamani zaidi ya mara moja bila sababu yoyote ya maana. Kwa shinikizo iliingizwa kwenye katiba pendekezwa ya mwaka 2014.

Mzee Mwinyi anapozungumzia suala la nidhamu ndani ya vyama, kwa maoni yangu kuruhusu mgombea binafsi ingekuwa ni njia moja kusaidia kutokana na wale miungu-watu kugundua ukiwazingua wanachama wako, basi kesho watagombea kama wagombea huru.

Anapoeleza kuhusu vyama kuungana na juhudi za kutengeneza mazingira magumu kwa lengo la ‘kuimarisha msingi wa mfumo wa vyama vingi’, niweke wazi kuwa mimi binafsi ni muumini wa kuwa na vyama vichache na si utitiri wala vya msimu!

Tena ninakumbuka Mwalimu Nyerere alieleza wazi wazi wakati wa kung’atuka uenyekiti wa CCM mwaka 1990, kuwa ‘alitamani nchi kuwa na vyama viwili vya kijamaa’.

Sasa mzee Mwinyi kama angekuwa mwana nadharia angejikita hasa kwenye aina ya vyama vinavyotakiwa nchini kabla ya kufikiria kuviwekea vizingiti visivyokuwa vya lazima. Ukweli ni kwamba unapozungumzia biashara ya chama cha siasa popote duniani kitu cha kwanza ni itikadi au imani.

Na kutokana na huo ukweli, kuelekea uchaguzi wa vyama vingi wa 1995, mwanahabari mkongwe, Jenerali Ulimwengu, alifafanua vizuri sana aibu ya nchi kuhusiana na sera ambazo hutokana na itikadi au imani ya chama.

Nikimnukuu: “Tumewahi kusikia kiongozi wa chama kimoja akisema kwamba chama chake hakitangazi sera zake kwa kuhofia wezi wa sera watakiibia na mwingine naye akatangaza kwamba hatoi sera zake mpaka hapo akiisha kuchaguliwa ndipo wananchi watakapogundua kwamba sera zake ni kiboko!

“Haya ni maneno ya ajabu. Dhana ya kwamba sera inaweza kuibwa na mshindani lazima itakuwa inatokana na hisia kwamba sera si kitu cha kweli, cha dhati, kinachoongoza chama na kazi zake za kisiasa. Imekuwa kana kwamba ‘sera’ ni kiini macho cha kuwazuga wananchi, ni ujanja wa kuwahadaa na hauna uhusiano hasa na hulka ya chama chenyewe na viongozi wake.”   

Sina budi niseme kimsingi maelezo ya mzee Mwinyi yanatusaidia sana kutukumbusha angalizo la Mwalimu Nyerere kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM wa mwaka 1992 kuhusu hatari ya kutengeneza umoja bandia ndani ya CCM.

Ukiondoa hayo, kwenye kitabu cha mzee Mwinyi kuna masuala kadhaa mazito yaliyoachwa kabisa na ambayo lazima yatazamwe kwa faidi ya vizazi vijavyo.

La kwanza linahusiana na mpango uliokuwapo wa kutaka mzee Mwinyi kuendelea kuongoza nchi kwa maana ya kipindi cha tatu. 

Watu wengi hawalijui nadhani kutokana na Mwalimu Nyerere kuuzima mapema sana kwenye kipindi cha pili na pengine bila nguvu yake, Tanzania ingejikuta ni kinara wa mpango wa viongozi wa Afrika kubadili katiba.

Tena nilikumbuka jinsi gani mzee Mwinyi alivyokuwa anampigia chapuo marehemu Magufuli aongezewe kipindi cha tatu, hivyo inawezekana kabisa aliona mpango huo ulikuwa sawa. Yote ni rukhsa!

La pili ni kuhusiana na baada ya mpango huo kushindikana na mchakato uliofuata wa jinsi gani ya kumpata mgombea urais kupitia CCM mwaka 1995. Ukweli ni kuwa kwa viongozi wengi wa Afrika mara nyingi sana kuna mtihani mkubwa kwenye suala hilo.

Tunapata msaada mkubwa hapo kutoka kwa aliyewahi kuwa naibu waziri wa kilimo na kinara wa kundi la G55, Njelu Kasaka: “Tulipomweleza Mwalimu Nyerere kutoridhishwa kwetu na utaratibu unaotumika CCM kumpata mgombea urais, alikubaliana na sisi na kusema mfumo wa sasa haukuwa na uwazi wa kutosha. 

Tulimweleza jinsi tulivyojitahidi kupitia mikutano ya wabunge wa CCM kutaka mfumo ubadilishwe, bila mafanikio. Sisi tulitaka wagombea wajitokeze wenyewe na chama kibaki na jukumu la kuwachuja kwa kutumia vigezo vilivyowekwa.

“Mwalimu Nyerere alikubaliana nasi katika wazo hilo na akasema atahudhuria mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM uliopangwa kwa lengo la kuwaambia viongozi wa CCM kuwa muda umefika wa kubadili utaratibu wa kuwapata wagombea wa urais. ‘Nitaingia kwenye mkutano huo hata wasiponikaribisha’,” alisema kwa utani.

Naamini mzee Mwinyi angekuwa mwana falsafa, inawezekana angeona umuhimu wa kumpata mgombea urais wa chama tawala kwa njia ambayo kweli ilikuwa inaendana na mfumo mpya wa demokrasia ya vyama vingi. Yaani hadi akina Kasaka walipitia kwa Mwalimu Nyerere ilikuwa si sawa.

La tatu sasa ni kuhusiana na mchakato wenyewe wa kumchagua mgombea urais wa CCM 1995. Mzee Mwinyi hajazungumzia kabisa kilichotokea kama tu ambavyo Benjamin Mkapa naye kwenye  kitabu chake hakufanya. Hii si sawa!

Yaani unatuambia kilichotokea wakati wa kuingia lakini si wakati wa kuondoka. Inawezekana wakati wa kutoka ina umuhimu kuliko wakati wa kuingia!

Yeye na Mkapa wameeleza tu kilichofanyika kwa upande wa vyama vya upinzani wakati ndani ya CCM ndiko kulikuwa na kitimtimu hadi nguvu ya ziada ilihitajika!

Tena katika tukio la kihistoria la mwaka 1995, jumuiya ya vijana wa CCM ilifikia kupendekeza majina manne ya watu ambao iliona wanafaa kufikiriwa kuwa mgombea mwaka 1995. Majina yao yalikuwa ni Dk. Salim Ahmed Salim, Edward Lowassa, Jaji Mark Bomani na marehemu Dk. Lawrence Gama. 

Matokeo ya kazi hiyo ilisababisha mwenyekiti wake, marehemu John Guninita, kujikuta matatani wakati kiukweli walifanya kwa nia nzuri na wala hawakusukumwa na utashi wa mtu yeyote tofauti na miaka ya baadaye.

Hapo je, mzee Mwinyi alichukuliaje suala hilo kama mwenyekiti wa chama?

Zaidi ya hayo, mzee Mwinyi mpaka sasa amekuwa na bahati ya kuwaona wagombea urais wa CCM wengi kuliko wenzake wote. Angeweza kuwa na jambo la kutufikishia hapo.

Kwa mfano, katika kueleza alivyofanikiwa yeye mwenyewe kuwa mgombea urais wa Muungano mwaka 1985 dhidi ya Salim Ahmed Salim, ambaye alikuwa ni kipenzi cha Mwalimu Nyerere, isipokuwa mzee Mwinyi ameweka wazi “alituhumiwa bila ushahidi na baadhi ya wazee kutoka Zanzibar na wachache kutoka Bara, kuwa ni msaliti aliyeshiriki mipango ya kumuua Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Aman Abeid Karume,” alionaje sasa wakati Salim alipojitosa kwa nguvu zote 2005?

Isitoshe, eti ‘walimtuhumu pia, bila uthibitisho, kuwa hasemi kauli ya “Mapinduzi Daima!!”

Binafsi nilitegemea mzee Mwinyi angeweza kusimama kidete alipoona ile hali ya 1985 inajirudia na kuwakumbusha wana CCM juu ya ahadi yao ya ‘Nitasema ukweli daima; fitina kwangu mwiko’.

Hii pia ni kwa kuzingatia mzee Mwinyi mwenyewe kumtambua Salim kuwa ni kiongozi “hodari sana” na “kwa mujibu wa Katiba mpya ya 1984, asingeweza kuendelea kwenye wadhifa wa waziri mkuu”, lakini alipenda awe naye bega kwa bega hadi alimteua kuwa naibu waziri mkuu. Kwa kawaida angekuwa anaitikia wito wa ‘muungwana ni vitendo’.

Kwa ujumla, ninarudia kauli kuwa kitabu cha mzee Mwinyi kimesaidia kuelewa kwa undani zaidi mazingira yaliyomkabili kwa miaka yake kumi. 

Siwezi kuacha kueleza mshangao wangu kidogo kuhusiana na baadhi ya changamoto alizokutana nazo kutoka upande wa Zanzibar. 

Anakiri mwenyewe kuwa: “Kufika mwezi Agosti 1993, nikaona mambo matatu, hili la utaratibu wa kupata Makamu wa Rais, Zanzibar kujiunga na OIC na hili la G55 na madai ya Serikali ya Tanganyika yalielekea kunizidi kimo.”

Sasa kwa mfano kwenye suala la kupata Makamu wa Rais, ambalo lilikuwa pendekezo la Kamati ya Jaji Bomani, mzee Mwinyi hakumung’unya maneno kusema: “Hoja ya Bomani na wenzake ilikuwa wazi, bila utata wowote.” 

Sasa ilikuwaje Mwalimu Nyerere tena kuhitajika kuokoa jahazi wakati angeweza yeye mwenyewe kuweka sawa suala ambalo halikuwa na ‘utata wowote’?

Na leo tunaona matunda yake kwa Zanzibar bila hofu yoyote.

Mwisho wa yote, ninairudia ile kauli murua ya Enock Powell juu ya maisha ya kisiasa.

Kwani ndani ya kipindi kimoja huwezi kufanya mambo ya kuridhisha? Ina maana hata Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amepata bahati ya mtende hawezi kukaa Magogoni kwa kipindi kimoja?

Bahati nzuri sana kuna mfano hai wa aliyekuwa rais wa Zanzibar, Idris Abdul Wakil, ambaye alimrithi mzee Mwinyi mwaka 1985 hadi 1990.

Nikimnukuu mzee Mwinyi kuhusu Abdul Wakil: “Alitushangaza sote; lakini alikataa kabisa ushawishi wowote ule wa kuendelea.”

Najaribu kupata picha, mzee Mwinyi na Abdul Wakil kwa pamoja wangeachia?

Historia ina mafunzo tele!

Mwandishi ni mwanasayansi wa siasa na Kaimu Katibu Mwenezi wa UDP

O784219535/ a_bomani@yahoo.com

433 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!