MOMBASA

Na Dukule Injeni

Takriban miaka 10 iliyopita Uhuru Kenyatta akiwa kiongozi wa Chama cha TNA aliungana na William Ruto wa URP wakati huo na kuunda muungano wa Jubilee ulioshinda Uchaguzi Mkuu mwaka 2013.

Katika moja ya kampeni zao, Kenyatta, aliwaomba Wakenya kumpa ridhaa ya kuwa Rais kwa miaka 10, kisha miaka 10 inayofuata wamchague Ruto, ikitafsiriwa kama mipango ya kuzima ndoto za Raila Odinga kuongoza Kenya.

Hata hivyo, tofauti za Rais Kenyatta na naibu wake, Ruto, ziliibuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017 ambao matokeo yake yalibatilishwa na Mahakama ya Upeo wa Juu (Supreme Court). 

Odinga alisusia marudio ya uchaguzi hadi malalamiko yao kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) yapate ufumbuzi.

Ili kuepusha Kenya kuingia katika machafuko ya kisiasa kama ilivyotokea baada ya uchaguzi mwaka 2007, Rais Kenyatta aliamua kufanya maridhiano na Odinga, jambo ambalo halikupokewa vema na Ruto ambaye kwenye kampeni zake amekuwa akisema: ‘Handshake’ ilikuja kuvuruga mipango ya serikali.

Matokeo yake Naibu Rais akawa kama mpinzani ndani ya serikali huku Odinga ambaye ni mpinzani akionekana kuhusishwa na mambo mengi yanayofanywa na serikali kiasi hata wakati mwingine mawaziri kushuhudia wakienda kumpa taarifa za mipango ya serikali.

Ukaribu wa Kenyatta na Odinga umesababisha amuunge mkono kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, mwaka huu kupitia muungano wa Azimio la Umoja na kuwaacha wafuasi wa Ruto wakinung’unika na kulalamika kusalitiwa, wakimkumbusha aheshimu kauli yake; “miaka 10 yangu na miaka 10 ya Ruto.”

Lakini ambacho kimebainika wazi hususan kipindi hiki kampeni zikiendelea ni malalamiko aliyokuwa akiyatoa Odinga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017, ndiyo sasa anayatoa Naibu Rais Ruto anayewania urais kupitia Chama cha UDA (United Democratic Alliance) chini ya muungano wa Kenya Kwanza.

Wengi wanahoji, vipi sasa Ruto anaona ni makosa wakati mwaka 2017 wenzie walipolalamika hakuona kuna dosari? Naibu Rais amekuwa kwenye malumbano na mawaziri wanaojihusisha kwenye kampeni, jambo ambalo Supreme Court iliitolea uamuzi mwaka 2017.

UDA imemtaka Mkurugenzi wa Mashitaka na Makosa ya Jinai (DPP), Noordin Haji, kufungua jalada la jinai dhidi ya mawaziri watano kwa kile wanachodai kumfanyia kampeni mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance, Odinga.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2017, Odinga alilalamikia mwenendo wa kutoridhisha wa baadhi ya mawaziri kumfanyia kampeni Rais Kenyatta achaguliwe tena na kusisitiza kama watumishi wa umma, mawaziri walibanwa na Katiba, Sheria ya Vyama vya Siasa, Sheria ya Maadili ya Watumishi wa Umma na Sheria ya Makosa ya Uchaguzi kushiriki katika shughuli za kisiasa.

Odinga alishinikiza mawaziri wanaohusishwa wafunguliwe mashitaka, pia kuitaka Supreme Court kutangaza kwamba Kifungu cha 23 cha Sheria ya Uongozi na Uwajibikaji kinakiuka katiba kwa kuwaruhusu mawaziri kuwa na upande kinyume cha Kifungu cha 232 cha Katiba.

Licha ya Supreme Court kutupilia mbali matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2017 yaliyompa Rais Kenyatta ushindi na kuamuru urudiwe, mahakama hiyo pia ilikataa madai ya Odinga kuhusu mawaziri kujihusisha na kampeni za kisiasa. Mahakama iliamua kwamba mawaziri wanaweza wakashiriki siasa kikamilifu huku wakiendelea kuitumikia serikali.

“Hawa ni wateule wa kisiasa wakiwa na jukumu la kutekeleza ‘manifesto’ ya wale waliowateua au chama cha siasa. Hii ni sehemu muhimu ya demokrasia kwa serikali iliyoingia madarakani kwa mfumo wa kisiasa,” mahakama iliamua.

Uamuzi huu wa mahakama haukupingwa na Ruto, licha ya Odinga kuulalamikia sana kutokana na kuwa wakati huo ulikuwa unampendelea na kuwapa uhuru mawaziri kuendelea kuwafanyia kampeni hadi kushinda marudio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017.

Miaka mitano baadaye na hususan Kenya ikielekea debeni ambapo rais wa tano atakayemrithi Rais Kenyatta atachaguliwa, wapo baadhi ya mawaziri ambao wameungana na bosi wao, Kenyatta, kumfanyia kampeni ya wazi Odinga.

Mawaziri hao ambao Ruto anataka DPP kuwafungulia jalada la makossa ya jinai huku pia akitaka wajiuzulu nyadhifa zao ni Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani), Joe Mucheru (Teknolojia), Peter Munya (Kilimo), Eugene Wamalwa (Ulinzi), James Macharia (Uchukuzi na Miundombinu) na Keriako Tobiko (Mazingira).

Katibu Mkuu wa UDA, Veronica Maina, amemwambia DPP watumishi hao wa umma kuendelea kujihusisha na siasa kunahatarisha uwepo wa uchaguzi huru na wa haki Agosti 9, mwaka huu.

Hata hivyo, mkuu wa kampeni wa Odinga ambaye pia ni Gavana wa Laikipia, Ndiritu Muriithi, amepuuza malalamiko ya UDA akiyataja kama ya kutapatapa baada ya kuhisi wanashindwa kwenye uchaguzi mkuu.

Aidha, mawaziri Wamalwa, Mucheru na Matiang’i nao wameshangazwa na malalamiko ya Naibu Rais Ruto wakihoji kwa nini sasa hivi liwe kosa kumfanyia kampeni Odinga katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wakati ilikuwa sahihi wao kumfanyia yeye (Ruto) kampeni mwaka 2017 akiwa mgombea mwenza wa Kenyatta?  

Suala la mawaziri kujihusisha na kampeni za uchaguzi kuepuka wagombea kulalamikia njama za kuwahujumu linapaswa kuwekwa kisheria ili yasijitokeze kama tunavyoshuhudia katika nyakati tofauti kati ya Ruto na Odinga.

By Jamhuri