Nianze na salamu za mfungo wa mwezi kwa Wakristo wenzangu. Najua lengo
mojawapo ni kuombea amani na upendo baina yetu. Najua kwamba wengi wetu
tunafaidi hii hali ya utulivu tulionao tofauti na mataifa mengine ambayo wakati
mwingine hawajui kesho yao ikoje na wataamkia wapi!
Wiki jana mwishoni mwishoni, tumesikia mambo mengi yahusuyo uongozi katika
Bara la Afrika, nikaogopa sana kuona tunafika mahali ambapo kiongozi wa juu
kabisa katika taifa kubwa na tajiri kwa Afrika, hata kama utajiri huo ni kidogo
wanaweza kumshurutisha rais wao aachie ngazi kwa makosa mbalimbali ambayo
ameyafanya au anayafanya.
Wiki jana tena tukapata taarifa za kifo cha kiongozi mkuu wa upinzani huko katika
taifa ambalo pia wananchi kwa maana ya chama kwa kushirikiana na jeshi lao,
walimuomba kiongozi mkuu wa nchi aachie ngazi ili kuruhusu awamu nyingine ya
uongozi, wanataka kuiona Zimbabwe mpya vizuri zaidi ikiwa haiko mikononi mwa
Mugabe.
Nimefikiria yote hayo na kuanza kuona msukumo wa Kaskazini ulivyotokea na
jinsi ambavyo msukumo wa Kusini unavyotambaa. Zamani sisi tukiwa vijana –
tena wafugaji tusioenda shule – tulijua dhahiri kuwa ugonjwa wa sotoka uliokuwa
katika kijiji cha pili nasi ulituhusu kuukabili kabla haujaleta madhara kwa mifugo
yetu.
Hili ni wimbi kama la sotoka, ninajua ni jinsi gani sotoka la mnyama wa Kaskazini
lilishindwa kudhibitika kula hali lilianza na kijana mmoja tu kwa kujichoma moto
hadharani na kutangaza kuanza kwa mabadiliko, nadhani ni ulevi tu wa viongozi
wao kuamini kwamba nguvu ya yule kijana na uhai wake havingeweza kuhimili
mabavu yao ya nguvu za dola na kadhalika.
Kutokana na kuishi kwingi, nimejua kuwa hakuna vita isiyo na msaidizi, na hili
linaweza kuthibitishwa rasmi na lile sakata la vita ya Tanzania na Uganda miaka
ile ya sabini, tuliwashika wasaidizi kutoka mbali na vita yetu, watu wale wa mataifa
ya mbali walikuja kutoa msaada kwa rafiki yao ili aweze kutekeleza azma ambayo
naamini waliijenga watu wa Kaskazini.
Nimeamua kutoa mifano hii ya waraka wangu ili niweze kueleweka vizuri
nakusudia kusema nini, simaanishi kikulacho kuwa nguoni mwako, nataka
kumaanisha unafiki wa rafiki katika ustawi wa taifa na kuleta zogo na hekaheka ili
kuondoa viongozi na hata kuleta vita, ili nchi iwe katika wakati mgumu wa mpito
na wale wenye malengo yao waweze kutumia mwanya huo kujineemesha.

Sehemu yoyote ya kazi kuna watu ambao kwa makusudi kabisa wapo kwa nia ya
kutenda maovu ili wapate furaha – iwe maovu ya kumtendea mtumishi mwenzie
au hata ofisi yenyewe – watu hawa wapo hakuna namna ya kuwazuia zaidi ya
kuwatenga, lakini watu hawa wamekuwa na sura mpya ya mara kwa mara
kuonesha kwamba mabaya yao yanajificha katika kitu kinachoitwa sheria za kazi
au utaratibu wa kazi.
Nimeshuhudia unafiki mwingi ambao unafanyika katika maofisi mbalimbali, wapo
ambao kimsingi wamejiridhisha kwamba utendaji wao wa kazi ni mdogo kuliko
wengine, lakini ili kujitafutia uhalali ni lazima watengeneze mazingira ya wengine
kutoweza kufanya kazi na kuendekeza majungu mazito ya fitina kwa wakubwa
wao.
Tumeshuhudia jinsi ambavyo wasioweza kazi wakipandishwa vyeo baada ya
kuuaminisha umma kwamba wanaweza lakini matokeo yake kila mtu anayajua, ni
kuporomoka kwa maendeleo na kugeuza maeneo ya kazi kuwa vilinge vya
majungu.
Sina shaka kabisa na utendaji kazi wetu wa kujali zaidi vyeti na siyo uwezo wa
mtu binafsi, sina shaka kabisa na vyeti na uelewa wa kinadharia na siyo vitendo,
lakini pia nina shaka kubwa na wamiliki vyeti wenye uwezo mkubwa wa kinadharia
badala ya vitendo, na hapa ndipo ninapoanza kumkumbuka Mwalimu na falsafa
yake ya uongozi ni heshima katika jamii, ni karama na kujitoa na siyo sifa na
kuwagawanya unaowaongoza.
Leo nimeamua kuandika waraka huu si kwa sababu siwapendi wasomi, lakini ni
kwa sababu wengi wao huamini katika wao na si wengine, wengi wao huamini
wakiaminicho na si wanachokiamini wengine.
Wengi wao huwapunguza nguvu wenye uzoefu kwa sababu tu wanaona kama
wanataka nafasi zao, wengi wao hawajiamini bali wanaishi kwa majungu na fitina
sehemu za kazi, mwisho wa siku tunaamini kikulacho ki nguoni tukasahau kuna
marafiki washauri wabaya na wazuri kutoka Kaskazini na Kusini.
Wakatabahu,
Mzee Zuzu

Please follow and like us:
Pin Share