Yah: Umiliki wa mashamba na majengo ya walalahoi uzingatiwe

Nimesikia matangazo ya watu mbalimbali, kila mtu akinadi kile anachokijua, sasa ni kama nimevurugwa na akili yangu haifanyi kazi ipasavyo kutokana na matangazo hayo ya wananchi wenye kunena kwa niaba ya Serikali, huku wakijua wazi kwamba hawana mamlaka ya kunadi wasichokijua ili kuwapotosha wananchi, hasa sisi tulio wengi huku Kipatimo.
Najua kuna taarifa rasmi ya kulipia majengo na ardhi ambayo ilitangazwa, na siye wenye mbavu za mbwa tuliambiwa mapema kabisa kwamba itabidi tujenge nyumba bora ndiyo tuanze kulipia kodi, hatukuambiwa kwamba tukishindwa tutavunjiwa, hatukuambiwa kuwa ardhi zetu za urithi tutapokwa kwa kuwa hatuwezi kuziendeleza.
Pamoja na ujinga nilionao mimi na wazee wenzangu, tunajua kuwa ardhi ni mali ya Serikali inaweza kuamua kuitumia wakati wowote kwa manufaa ya walio wengi, lakini pia tunajua kuwa Serikali inapochukua ardhi ya mwananchi hulipa fidia kwa mazao na maendelezo yoyote ambayo yapo juu ya shamba au kiwanja husika.

Sasa hivi tupo katikati ya sintofahamu ya waswahili ambao wengi wao ni madalali wa maneno na kutuangalia tunafanya nini, wazee wachache wenye kujua sheria wamekuwa wakali kila wanapovamiwa na wajanja wa maneno katika kuporwa maeneo yao, wengi wao tayari wamekwishaingia katika mtego wa kugawa maeneo kwa bei ya kutupa ili kukwepa kodi ya ardhi ambayo tunaambiwa ina malimbikizo.
Kila mtu anafahamu kuwa nchi yetu ni kubwa na mawasiliano ni finyu hasa katika mambo mazito na makubwa kwa Taifa, mambo ambayo ni rahisi kupatikana kwa taarifa ni pamoja na umbeya na mambo ya uzushi, mambo ya zinaa na fumanizi, mambo ya uongo na utapeli.
Sasa hivi tunasikia mambo mengi ya uzushi na baada ya muda mrefu ndipo tunaambiwa ukweli wenyewe nadhani kwa kuchelewa sana, katika kipindi chote hicho cha uongo wa jambo hakuna anayekanusha, tunajenga taswira mbaya kwa aliyezushiwa na kusingiziwa, tunajenga imani mbaya kwa Serikali kwa uongo uliosambazwa.

Sasa huu uongo unaosambazwa juu ya ardhi na taarifa zake kuwa finyu unatufanya tuingie katika migogoro mingi na majirani zetu na viongozi wetu wa mitaa na vijiji, wengi wetu tuna maeneo ya urithi kutoka kwa mababu zetu na wazazi wetu, wengi wetu hatujui ukubwa hasa wa maeneo yetu na makadirio ya gharama za kulipa kodi, wengi wetu hatuna hati za umiliki wa maeneo yetu kwa sababu za ukiritimba ambao tulikutana nao enzi hizo.
Tupo njia panda na ambacho tunakifahamu ni kidogo kuliko kinachozungumzwa, tunajua kuwa iwapo tumefikisha miaka sitini hatupaswi kulipa kodi ya jengo, tunajua kuwa iwapo nyumba zetu ni mbavu za mbwa hatupaswi kulipia gharama ya jengo lakini zaidi ya hapo hatujui chochote zaidi ya uvumi ulioshika kasi mpaka sasa hivi.

Siku za hivi karibuni kumeibuka kundi la wajanja wakisema tunatakiwa kulipia maeneo yetu ambayo tunayamiliki bila hati ya Serikali, yameibuka makundi yanayotaka kuwasaidia wazee kuwatafutia hati ya mashamba yao, kumeibuka makundi ya upimaji ardhi kwa gharama ya kugawana ng’ombe kama huna fedha ya kulipia upimaji.
Yameibuka makundi yanayoitwa ya ukadiriaji wa gharama za kodi ya mashamba na majengo huko vijijini, wazee sasa tunaishi maisha ya mashaka na kuona tunaweza kuishia jela kwa kumiliki maeneo ambayo hatujayalipia kodi tangu mwaka 1961 na pia hatujayamiliki kisheria.

Wazee sasa tunahitaji kauli ya Serikali iliyo madhubuti na kutuhakikishia usalama wetu na mali zetu yakiwamo mashamba na nyumba za kilalahoi tunazoishi, tunataka kujua gharama za namba ya nyumba na thamani ya nyumba inayopaswa kulipiwa kodi.
Wazee sasa hatuna nguvu tena, lakini tunapambana na wanyang’anyi wasio na huruma kwa kutupangia kodi bila kutuelekeza vizuri na mbaya zaidi wakiwa siyo watumishi wa Serikali.
Vijana sasa wamekuwa na hasira na sisi, na hawataki kutusikiliza kama sisi tulivyowasikiliza walivyokuwa watoto wetu.
Najua kulipa kodi ni wajibu wa kila mtu, najua kulipa kodi ni kwa maendeleo ya Taifa letu, najua kulipa kodi siyo shuruti na ni vema tukajijengea utaratibu na mazowea ya kulipa kodi lakini kodi isiwe adhabu kwa mlipaji, na anayedai awe na vigezo vilivyo wazi ili kuepusha magonjwa ya moyo na sononi kwetu wazee ambao kimsingi tumewalindia maeneo haya mpaka leo.

Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo