Asubuhi ya Januari 12, 1964, sultani wa Kiarabu na watu wake Zanzibar waliingiwa mshangao pale Waafrika ambao hadi wakati huo walionekana na kudhaniwa kuwa ni dhaifu, walipovamia kasri lake kumwondoa madarakani.

Mshangao huo uliwapata pia baadhi ya Waafrika ambao waliaminishwa na kuamini kuwa kamwe mtu mweusi asingeweza kumwondoa Mwarabu na yeye kutawala badala yake. 

Abeid Aman Karume na wenzake walithibitisha kuwa hizo ni hisia tu, kwani tangu wakati huo, utawala wa Waafrika umeipeleka Zanzibar mbele.

Watanzania hatuna budi kuwashukuru Karume na wenzake kutokana na ujasiri wao ambao uliwawezesha Waafrika kuonyesha uwezo wao katika kuongoza nchi yao. Kama si mapinduzi ya mwaka 1964, historia ya Zanzibar na Tanzania Bara isingekuwa kama ilivyo leo.

Hata watu wanaoyabeza mapinduzi hayo wanapaswa kufahamu kuwa uhuru wao wa kufanya hivyo unatokana na Mapinduzi. 

Kama kusingekuwa na Mapinduzi, kwanza wasingekuwa na uhuru wa kubeza, maana huenda wangekuwa chini ya utawala wa kisultani, lakini pia hakungekuwa na hayo Mapinduzi ya kuyabeza.

Wakati tukisherehekea miaka hii 56 ya Mapinduzi, ni wakati wa kutafakari kule tulikotoka, tukiangalia hapa tulipo kama njia ya kupima iwapo yale tuliyoyaazimia wakati wa Mapinduzi yametekelezeka.

Ni dhahiri kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa tangu Mapinduzi katika nyanja zote za maisha. Maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na katika nyanja nyingine ni dhahiri. Lakini hilo halipaswi kuwafanya Wazanzibari kubweteka, kwa sababu bado hawajafikia ngazi ya juu sana ya maendeleo.

Ukiangalia jinsi dunia inavyokwenda leo, utabaini kuwa Zanzibar na watu wake wanapaswa kufanya kazi kubwa sana ili kufikia malengo yaliyowekwa baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964. Watu wanaweza kudhani kuwa malengo hayo ni ya juu sana au yamepitwa na wakati, hasa ukiangalia dunia inavyokwenda leo hii.

Hata kama hilo ni kweli, sisi tunaamini kuwa bado misingi ya malengo yale bado inapaswa kufuatwa, kwa maana ya kutekelezwa ipasavyo ili kumweka Mzanzibari kuwa huru zaidi.

Tunaamini kuwa hilo linawezekana. Kama Mzanzibari na unyonge wake mwaka 1964 aliweza kufanya mapinduzi yaliyomwodoa sultani madarakani licha ya wao kuwa na kila aina ya silaha, nini kitamfanya Mzanzibari leo hii ashindwe kufanya mapinduzi mengine makubwa katika nyanja ya uchumi?

Kama njia ya kuyaenzi Mapinduzi ya mwaka 1964, Wazanzibari wainuke sasa na kufanya mapinduzi mengine makubwa kiuchumi.

By Jamhuri