Na Isri Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Afisa habari wa klabu ya Yanga, Ali Kamwe ametangaza kuwa Rais wa Yanga, Hersi Said pamoja na Kamati yake ya Utendaji wamekubaliana kuwa mechi yao dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini itakayochezwa Jumamosi ya Machi 30, 2024 itakuwa bure sehemu za mzunguko.

Mechi hiyo ya robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika, itachezwa saa 3 usiku, hivyo kulingana na muda huo uongozi wa Yanga umeamua kuwapunguzia gharama mashabiki wake.

“Viongozi wa Klabu yetu hawana tamaa ya fedha, ndio maana tumepunguza na kuondoa tiketi ya mzunguko kwa lengo la kuhakikisha mashabiki wengi waje Uwanjani, Tumeweka maslahi ya mpira wa Tanzania mbele, Mechi ya Mamelodi ni kubwa mno lakini kwa kuwa lengo sio fedha ni hamasa basi tunawasihi mashabiki kujitokeza kwa wingi.

“Kiasi cha fedha ambacho ungelipia tiketi ya mzunguko basi utatumia kama nauli ya usafiri wa kukufikisha uwanjani na baada ya mchezo wetu uweze kurudi nyumbani salama”

Aidha Ali Kamwe amesema atatangaza hivi karibuni kuwa ni mchezaji gani atapewa heshima ya mechi hiyo kama wanavyofanya siku zote katika mechi zao za kimataifa zinazochezwa nyumbani, huku akiwataka mashabiki wao kutoikatia timu tamaa mapema licha ya ukubwa na ubora wa kikosi cha Mamelod Sundowns.

“Mwananchi usisikilize uchambuzi wa mchambuzi yoyote Yule, Tusipotezwe kwenye dira yetu, Young Africans SC ikiamua jambo lake hatuwezi kufeli Nina uhakika kwa zaidi ya asilimia 100 kuwa tunakwenda kushinda mchezo ujao, Mtu akikwambia Mamelodi ina wachezaji wazuri mwambie hata sisi tuna wachezaji bora kuliko wao”

By Jamhuri