Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilimanjaro

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imetoa maelekezo kwa watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo waliosimamia mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo na kusema kuwa kamati haijaridhishwa na usimamizi wa mradi huo na dalili zinaonesha waziwazi kuna ubadhirifu wa fedha.

Kauli hiyo imetolewa Machi 20, 2024 na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya LAAC, Ester Bulaya akiwa na wajumbe wa kamati baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa hospitali ya Wilaya ya Rombo na baadae kukagua mradi wa jengo la halmashauri.

Bulaya amesema lengo la kamati ya LAAC ni kuangalia matumizi ya fedha za umma na ubora wa kazi zilizofanyika katika halmashauri ambapo ameeleza kusikitishwa kwa miradi ya Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kwa kuchukua muda mrefu, kutokukamilika kwa wakati wakati Serikali ilishawapatia fedha za kutekeleza miradi hiyo.

Akieleza kuonekana kwa dalili za ubadhirifu wa fedha zilizotumika katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya amesema, maelekezo yalitolewa na Serikali na miongozo ya Ofisi ya TAMISEMI ni kuwa Sh milioni 800 zilitakiwa kujenga majengo manne na badala yake yamejengwa majengo mawili pamoja na Halmashauri kuongeza fedha kutoka mapato ya ndani zaidi ya milioni 170 lakini pia fedha hizo hazionekani matumizi yake.

“mnajiamulia wenyewe kufanya maamuzi yenu hakuna vibali vya kubadilisha matumizi kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuna hospitali zimepewa  Sh bilioni 3.1 majengo yote yamekamilika, nyie hamjakamilisha na mmetumia zaidi ya fedha hizo” amesema Bulaya

By Jamhuri