Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar,

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeeleza dhamira yake ya kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya soka Zanzibar ili kuendeleza sekta ya michezo nchini.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), Dk. Patrice Motsepe na ujumbe alioongozana nao.

Dk. Mwinyi ameomba ushirikiano na CAF katika kuzikuza na kuziendeleza taasisi za michezo zikiwemo skuli za michezo nchini kwa nia ya kufuzu vyema mashindano ya “School Academic” kwa Zanzibar hasa ikiangaliwa kuwa Zanzibar ni mwanachama wa CAF tokea mwaka 2006.

Alisema, Serikali imejidhatiti kukabililiana na kuondosha changamoto zinazoikumba sekta ya michezo Zanzibar ili kufikia azma ya kufuzu mashindano ya kimataifa.

Amesema, Zanzibar inahitaji kushiriki na kufanya vizuri kwenye mashindano ya soka makubwa zaidi duniani na kueleza kwasasa inajivunia hatua ya sekta ya michezo ilivyofikiwa kwa kuimarika miundombinu ya kisasa na kuahidi Serikali kufanya makubwa zaidi kwenye kuimarisha miundombinu ya michezo nchini.

Pia Rais Dk. Mwinyi ameushukuru uongozi wa CAF kwa kuifanya Zanzibar kuwa mmoja wa waandaji wa Mashindano ya “African Academic Football Champion” kwa mwaka huu wa 2024.

Kuhusu mashindano ya AFCON, yanayaorafajiwa kuchezwa Afrika Mashariki mwaka 2027 ambayo wenyeji watakuwa Tanzania, Kenya na Uganda, Rais Dk. Mwinyi ameondoa shaka kwa Zanzibar kuwa na kipingamizi chohote cha kufanikisha mashindano hayo na kueleza Serikali ilivyojipanga na mashindano hayo.

Naye, Dk. Motsepe amesifu juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua ya kuinua sekta ya michezo na maendeleo makubwa yaliyofikiwa Zanzibar ikiweko kuwa na Uwanja mpya wa michezo “New Aman Coplex” wenye hadhi ya kimatafa na kukidhi viwango vyote vya FIFA.

Pamoja na hatua nzuri iliyopo ya ushirikiano baina ya TFF na ZFF, Motsepe pia amesifu juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa ZFF, Dkt. Suleiman Jabir kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuinua Soka, Zanzibar.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Damas Daniel Ndumbaro amesefu sekta ya Michezo inavyokua kwa Kasi Tanzania kutokana juhudi za kuimarika kwa miundombinu imara ya michezo nchini.

Amesema, kuelekea AFCON 2027, Tanzania inatarajiwa kuwa na Viwanja 11 vyenye kukidhi sifa zote za viwanja vya kimataifa baada ya kufanyiwa maboresho na matengenezo makubwa vikiwemo Zanzibar vitatu cha “Aman New Complex”, uwanja wa Gombani, Pemba na kiwanja kipya kujengwa, kwa Tanzania bara viwanja nane, ukiwemo uwanja mpya wa Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mororogoro, Mbeya, Mwanza, Songea na Tanga.

Akizungumzia fainali za Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika kwa skuli za CAF zilizoanza tangu Jumanne wiki hii ambapo kilele chake ni leo Uwanja wa “New Aman Coplex” Zanzibar, Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Tabia Mwita Maulid amesema, Serikali imetimiza wajibu wake kwa kuweka mazingira yote salama kwa fainali hizo na kuahidi kwa tayari kwa changamoto yoyote itakayojitokeza kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Fainali za Kombe la Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika za CAF zinafanyika chini ya udhamini mkubwa wa “Motsepe Foundation” ambazo zimewashirikisha wachezaji chini ya umri wa miaka 15 kutoka mataifa 11 ya Afrika miongoni mwao ni Tanzania, nchi ya Afrika ya Kusini, Benin, Genie, Kongo Brazaville, Morocco na Uganda, kwa timu za wasichana na wavulana ambazo zilianza kwa ngazi ya taifa, zone hadi bara na Tanzania imetoa timu zote mbili za wasichana na wavulana.
Mwisho

By Jamhuri