Kumekuwapo mikutano ya siri inayowahusisha viongozi waandamizi wa Chama cha ACT-Wazalendo na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao hawana hakika kama watatendewa haki wakati wa kupitishwa kwa majina ya wagombea urais.
Mazungumzo hayo yamelenga kufungua njia kwa wana CCM hao kujiunga na chama cha ACT endapo watafanyiwa mizengwe ndani ya CCM.


Habari kutoka kambi mbalimbali za wawania urais kupitia CCM zinasema mipango inaendelea kusukwa kwa umakini na usiri mkubwa.
Walio mstari wa mbele kufanikisha mpango huo ni wapambe wa watu wanaoutaka urais ambao wanasema hakuna sababu ya kuendelea kubaki ndani ya CCM kama mizengwe itapewa nafasi kumpata mgombea atakayekiwakilisha chama hicho.


“Mtaji wa ushindi ni wananchi. Endapo mahitaji ya wananchi yatapuuzwa, hakuna sababu ya kuendelea na CCM. Baba wa Taifa alishasema CCM si mama yake; kama mwasisi mwenyewe alisema hivyo, sisi ni nani hata tushindwe kuwashawishi tunaowataka ili waupate urais kupitia vyama vingine.
“Juzi tumeona namna Mzee Obasanjo (Rais mstaafu Oluseguni Obasanjo wa Nigeria) alivyochana kadi ya chama chake hadharani. Kitendo kile bila shaka yoyote kimechangia kuwafanya wapinzani washinde. Tunataka hayo yatokee hapa kwetu,” amesema mmoja wa wapambe wa wagombea urais.
Kikao cha karibuni kilifanyika katikati ya wiki iliyopita katika moja ya nyumba za watu wanaotajwa kuwania urais kupitia CCM iliyopo Mbezi jijini Dar es Salaam.


Kuna habari kwamba tayari viongozi waandamizi wa CCM, akiwamoa Mwenyekiti Rais Jakaya Kikwete wamedokezwa taarifa hizo za kishushushu, na sasa wanatafuta njia sahihi ya kuhakikisha CCM inaendelea kuwa moja hata baada ya vikao vya mchujo.
Duru za uchunguzi kutoka vyanzo mbalimbali ndani ya CCM na ACT zinasema CCM imeingiwa hofu kubwa kwamba huenda uamuzi wa wanachama hao wa kuhamia kwenye chama cha upinzani ikaweka rehani ushundi wa chama hicho kikongwe katika Uchaguzi Mkuu.


“Unadhani ni kwanini hadi leo CCM wanasita kutangaza tarehe ya wanachama kuchukua na kurejesha fomu? Kuchelewesha huku ni mkakati wao wa kuona mambo mengi yanafanywa kwa muda mfupi ili kuwanyima fursa wanachama watakaotaka kuhamia kwenye upinzani, hasa ACT,” kimesema chanzo chetu kingine.
Inaelezwa kwamba baadhi ya wanachama wa CCM walio chini ya uangalizi kwa madai ya kuanza kampeni kabla ya muda wamekuwa na mazungumzo ya kuwawezesha kuunganisha nguvu pamoja endapo uongozi wa juu utaendelea kuwabana au kuwafanyia hila.
Wana CCM walio chini ya uangalizi ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira; Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Januari Makamba; na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.


Matokeo ya uchaguzi nchini Nigeria yaliyokipa ushindi chama cha upinzani cha All Progressives Congress (APC) cha Rais mteule Muhammadu Buhari, yanatajwa kuwa changamoto kubwa kwa CCM.
Buhari na Rais Goodluck Jonathan, kwa pamoja walipata kushiriki harakati za kurejesha demokrasia nchini Nigeria kabla ya yeye na kundi kubwa la wanachama kujiengua na kuanzisha APC.


Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amenukuliwa akitamba kuwa kuna kundi kubwa la wabunge na watu wengine maarufu kutoka vyama vya siasa walio njiani kujiunga na chama chake.
Ameweka wazi kuwa wapo watu waliokata tamaa na siasa za kibabe ndani ya chama tawala na vyama vya upinzani, ambao kwa sasa wanajiandaa kujiunga na ACT.


Bila kuwataja majina, Zitto amesema wabunge zaidi ya 50 tayari wanakamilisha mipango ya kujiunga ACT-Wazalendo.
Viongozi maarufu wanaotajwa tajwa kumfuata Zitto ni wale wanaoona kuwa fursa ya wao kutendewa haki ndani ya CCM ni ndogo.
Kwa upande wake, Zitto amesema, “Subirini, mtaona tu.”

By Jamhuri