Kabrasha linaanza kufunguka juu ya nani anahusika na mauaji ya watoto mkoani Njombe huku ikithibitika kuwa ndumba, uchawi, ukimwi na ujinga vimekuwa nguzo ya mauaji hayo, JAMHURI limebaini.

Ni wiki mbili sasa tangu matukio ya mauaji ya watoto wasiopungua saba katika mazingira ya kutatanisha na kutikisa taifa yaanze kutokea mkoani Njombe na JAMHURI limebaini namna baadhi ya matukio hayo yalivyotekelezwa.

Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni. Mtuhumiwa mmoja katika mauaji ya watoto watatu wa familia moja ameamua kuzindika taarifa zisivuje kwa ‘kuzika’ Sh 15,000 katika kaburi la bibi yake akitekeleza masharti ya mganga wa kienyeji.

Tukio mojawapo katika matukio saba ya mauaji ya watoto hao ni lile la mauaji ya watoto watatu wa familia moja; Gaspar Nziku aliyeuawa na kukutwa na majeraha kichwani, Godwina Nziku aliyeuawa na kutelekezwa mtoni, na mwenzao, Gilbert Nziku. Matukio haya yamefanyika katika Kijiji cha Nundu.

Nyuma ya mauaji ya watoto hao watatu, uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika unabainisha kuwa mtuhumiwa mkuu katika mauaji ya watoto hao watatu ni baba mdogo wa watoto hao (jina linahifadhiwa), ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wenye ukwasi wa wastani mkoani hapa. Anamiliki mali kadhaa, likiwamo lori aina ya Fuso ambalo ndilo – uchunguzi unafichua kuwa lilitumika kuwachukua watoto hao na kuelekea kusikojulikana hadi ilipobainika wameuawa.

 

Nyuma ya pazia

Gazeti hili la JAMHURI limehakikishiwa kuwa mtuhumiwa huyo baada ya upelelezi wa kina wa vyombo vya dola, hasa Jeshi la Polisi lililokuwa chini ya Timu Maalumu iliyounganisha wataalamu kutoka Jeshi la Polisi Makao Makuu, mtuhumiwa huyo alihusisha matatizo yake ya kiafya (inadaiwa ni ugonjwa wa ukimwi) na kufanyiwa ushirikina (kulogwa).

Mganga wa mtuhumiwa huyo alimweleza kuwa mtu ‘mbaya’ anayemloga ni baba yake mdogo, na amekuwa akifanya ‘ubaya’ huo kupitia kwa mmoja wa watoto hao.

Katika kundi la watoto hao watatu, taarifa za kiuchunguzi zinabainisha kuwa mmojawapo alikuwa akimlaki kwa mapenzi makubwa baba yake huyo mdogo kila anapofika nyumbani kwa familia ya watoto hao, ikiwa ni pamoja na ‘kumkimbilia’ kila anapomwona kwa ajili ya kumsalimu (kumwamkia).

Kwa hiyo, taarifa zinafichua kuwa mganga huyo wa kienyeji alimweleza kuwa mtoto huyo ndiye mbaya na kila anapofika kwa ajili ya kumsalimu humshika kichwa kwa ajili ya kumwekea ‘jini’ na ndiyo maana afya yake imekuwa ikizorota, ingawa taarifa za kitabibu zinabainisha kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na matatizo ya afya – kwa mujibu wa vipimo vya kisayansi, yaani hospitalini.

Mipango ya mauaji

Taarifa zinafichua kuwa katika hatua za awali baada ya mganga kumshawishi mteja wake kuwa mtu ‘mbaya’ anayemwandama hadi kukabiliwa na matatizo ya kiafya ni baba yake mdogo, mtuhumiwa huyo alichukua sheria mkononi, akapanga kwenda kummaliza baba yake huyo mdogo, akiwa na gurudumu la gari akidhamiria kwenda kumvalisha mhusika na kumchoma moto. Hata hivyo, katika hekaheka za kukabiliana na tukio hilo kwa juhudi za watu kadhaa mlengwa alibaki salama.

Mtuhumiwa hakuridhika, na katika hatua mbaya zaidi alifanya mipango ya kuwaua watoto hao wasio na hatia, ingawa yalikuwa maelekezo ya mganga wake na hasa msisitizo ukiwa kwa mtoto aliyekuwa akimsalimia kwa ‘bashasha’ mtuhumiwa huyo kila alipokuwa akifika nyumbani kwao.

 “Alielezwa na mganga kwamba mmoja wa watoto hao ambaye hupenda ‘kumkimbilia’ kwa ajili ya kumsalimu kila anapofika nyumbani ndiye hatari, na kwa kila anapomfuata kwa ajili ya kumkimbilia ili amsalimie ndipo hapo humuingizia ‘jini’.

Kwa hiyo, katika kulenga mpango wake wa kuangamiza watoto hao, chanzo chetu cha habari kinaeleza: “Siku moja, baada ya mtuhumiwa kutoridhishwa na hali ya kushindikana kwa jaribio la kumwangamiza baba yake mdogo, ndipo akafanya uamuzi siku nyingine wa kuuawa watoto hao watatu. Huyu anamiliki gari aina ya Fuso. Hiyo siku alikwenda na Fuso lake hadi nyumbani kwa hao watoto (watatu) na aliwakuta wakicheza na watoto wenzao hapo nyumbani.

“Akafanya ujanja wa kuwatawanya wale watoto wa majirani … akiwaambia wengine wanaitwa na wazazi wao. Wakabaki wale watoto wa ndugu yake, akawashawishi aondoke nao, akawachukua na kuondoka nao kwenye gari hilo. Kwa hiyo kutoka katika kundi la watoto waliokuwa wakicheza, akawachukua wale aliowataka kwa ajili ya kwenda kutekeleza nia yake.

“Katika kukiri kwake, alieleza kila alichokifanya, na hata kutimiza masharti ya mganga wake mara baada ya kufanya mauaji ya watoto hao. Sharti la mwisho la mganga lilikuwa kwamba aende kwenye kaburi la bibi yake kwenda kuhitimisha malipo ya kafara kwa kufukia shilingi 15,000 kwenye kaburi hilo, ili kitendo alichokifanya (cha mauaji ya watoto) kisimgeuke,” alisema mtoa habari wetu.

Hadi tunakwenda mitamboni kuchapishaji gazeti hili, taarifa zinaonyesha kuwa baada ya mtuhumiwa kukiri kuhusika [na mauaji] wiki iliyopita, wakati wowote atafikishwa mahakamani.

Matukio ya mauaji

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka, amebainisha mlolongo wa matukio saba ya mauaji ya watoto mkoani hapa.

Novemba 16, mwaka jana, mwili wa mtoto ulipatikana eneo la Sido Mjini, mwili huu haukutambuliwa na alizikwa na manispaa.

Desemba 8, mwaka jana, mwili wa mtoto aliyefahamika kwa jina la Oliva Ng’anda mwenye umri wa miaka sita ulikutwa ukiwa umenyongwa eneo la Mfeleke – Njombe Mjini, huu ulikuwa mwili wa kwanza kutambulika, wazazi walifika na kuuchukua kwa ajili ya maziko.

Januari 10, mwaka huu, mtoto aliyefahamika kwa jina la Goodluck Mfugale mwenye umri wa miaka mitano alikutwa akiwa ameuawa, mwili wake ulikutwa na majeraha kichwani. Mwili huo ulikutwa eneo la Shule ya Sekondari Njombe.

Januari 21, 2019, Gaspar Nziku aliuawa na mwili wake kukutwa na majeraha kichwani, mwili huo ulikutwa eneo la Nundu.

Januari 27, 2019, Godwina Mwenda Nziku mwenye umri wa miaka 10, aliuawa na kukutwa eneo la Mto Hagafilo.

Januari 27 (tena), 2019, Gilbert Nziku mwenye umri wa miaka mitano alikutwa ameuawa eneo la Kijiji cha Nundu.

Februari Mosi, 2019, Rechol Malekela, mwanafunzi wa darasa la pili, naye alikutwa ameuawa Kijiji cha Matembwe.

Kumekuwa na imani za kishirikina kuwa kitu chenye ncha kinachotumika kwa ajili ya mauaji kikiwa na damu ya marehemu hupelekwa kwa mganga wa kienyeji kwa ajili ya kukidhi imani za kishirikina kama kujipatia mali na mahitaji mengine.

 

Agizo la RC Sendeka

Itakumbukwa kuwa baada ya mauaji ya watoto hao kutokea na kuzua taharuki, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher ole Sendeka, aliapa kuwa wote waliohusika ni lazima mkono wa sheria uwaguse bila kujali nafasi zao katika jamii, na kundi mojawapo lililodhaniwa kuhusika na mauaji ya watoto hao ni baadhi ya wafanyabiashara mkoani Njombe.

Hata hivyo, baada ya kuwakamata na kuwashikilia baadhi ya wafanyabiashara maarufu takriban wanane huku uchunguzi wa Jeshi la Polisi ukiendelea, imebainika kuwa wafanyabiashara hao baadhi wakiwa maarufu wenye vitega uchumi vikubwa katika mji wa Makambako hawahusiki na matukio hayo.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Sendeka, akizungumzia agizo lake la awali la kuwakamata watuhumiwa wakiwamo baadhi ya wafanyabiashara amesema imebainika wafanyabiashara hao wanaendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria zote za nchi na hawahusiki na vitendo hivyo.

Ilivyokuwa wiki mbili nyuma

Baada ya matukio hayo kujitokeza mfululizo wiki kadhaa nyuma, kulizuka hali ya taharuki miongoni mwa wazazi katika mji wa Makambako kiasi cha Mbunge wa Makambako, Deo Sanga, amenukuliwa na gazeti moja la kila siku akisema: “Karibu wafanyabiashara 10 ambao wamewaajiri watu 200 wamekamatwa na hatujui kinachoendelea kufikia sasa.” Mbunge huyo alisisitiza kuwa hata shughuli za kiuchumi zilikwama kwa siku hizo za awali baada ya taarifa hizo kufichuka na kuzua taharuki.

Kamanda wa Polisi Njombe, Renata Mzinga, naye katika taarifa yake ya awali kuhusu mauaji hayo alinukuliwa akisema: “Tumevumbua mtandao wa watu waliohusika na mauaji hayo. Tunashirikiana na kitengo maalumu cha polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam kuhakikisha wote waliohusika na ukatili huo wanatiwa nguvuni.”

Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeliomba Bunge kuunda Kamati Maalumu kuchunguza mauaji hayo ya watoto Njombe.

Wizara ya Mambo ya Ndani imewahakikishia usalama wananchi wa Njombe na kusema serikali itahakikisha wote wanaohusika na mauaji hayo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

5685 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!