Agizo la Rais John Magufuli la kuwaondoa watumishi raia katika majeshi ya ulinzi na usalama, limeanza kutekelezwa, huku Wizara ya Utumishi wa Umma ikiendelea kupitia muundo.

Taarifa ambazo JAMHURI limezipata, zinasema kuwa tayari kazi hiyo imekamilika katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), huku Jeshi la Polisi likiwa tayari limeshafikisha orodha ya watumishi hao kwa mamlaka husika.

Akizungumza na JAMHURI, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi, Angela Kairuki, anasema tayari kazi hiyo imeshakamilishwa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, huku akikiri ofisi yake kupokea orodha ya wafanyakazi wengine kutoka kwa Inspekta Generali wa Polisi nchini, (IGP), Ernest Mangu.

“Tayari ofisi yangu imeshapokea majina kutoka ofisi ya IGP Mangu…lakini zoezi kama hilo limeshakamilika ndani ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Sasa tunaendelea kupitia muundo na kuangalia maeneo yenye mahitaji,” anasema Waziri Kairuki.

Waziri huyo anasema baada ya kupokea orodha hiyo, wameanza kufanya uchambuzi wa sifa za watumishi hao kabla ya kuanza kuwasambaza kwenye maeneo yeye mahitaji ndani ya idara na taasisi za Serikali, anasema orodha ya majina hayo ni zaidi ya watumishi 100.

“Tuliagizwa na Rais na sisi kazi yetu ni kutekeleza maagizo hayo…sasa tunachambua sifa za watumishi hao pamoja na kupitia muundo wa utumishi kabla ya kuwapangia maeneo mengine,” anasema Kairuki.

Akizungumza na JAMHURI, IGP Mangu anasema, hawezi kutoa taarifa zaidi za watumishi wasiokuwa askari ndani ya Jeshi la Polisi, badala yake akalitaka gazeti hili kuwasiliana na Wizara ya Utumishi.

“Kuhusu hao wafanyakazi raia ndani ya Jeshi la Polisi, naomba ziulizwe mamlaka za watumishi hao raia…tafadhali naomba muwatafuate watu wa Wizara ya Utumishi,” anasema IGP Mangu.

Julai, mwaka huu Rais Magufuli alipokuwa anawakamisheni Makamishna na Makamishna Wasaidizi wa Jeshi la Polisi, alitoa agizo la kuwaondoa watumishi raia katika majeshi.

Rais Magufuli alihoji sababu za kuwapo watumishi raia katika majeshi, ikiwa ni pamoja na Polisi na kuagiza watumishi watakaoajiriwa wawe ni askari, akilenga kupeleka nidhamu ya jeshi kwenye idara ya uhasibu.

“Hao watumishi ambao ni raia, muwapeleke Utumishi, kwani hakuna polisi ambao wamesomea uhasibu, uhandisi pamoja na masuala ya utawala? Matatizo ya wizi wizi pamoja na yale ya watumishi hewa, kama yanaletwa na raia, IGP kaorodheshe majina yao wote watoke,” alinukuliwa Rais Magufuli.

Baada ya kutoa agizo hilo, Jeshi la Polisi lilianza kuangalia njia za kutekeleza agizo hilo. Kada ya wahasibu ilionekana kulengwa zaidi kwani wao ni waajiriwa wa Hazina.

Habari kutoka ndani ya Jeshi hilo zinasema baada ya tafakuri, iliamuriwa wahasibu wote ambao ni raia wapelekewe kwenye mafunzo katika Chuo cha Polisi Moshi.

Wahusika wote walipewa taarifa wakitakiwa wajiandae kwenda kwenye mafunzo ya kijeshi. Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea, viongozi waandamizi wa polisi walipitia miongozo mbalimbali na kubaini kuwa na wahasibu ambao ni askari kungeleta mtanziko mkubwa kwenye kazi za kihasibu.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa wetu, kuajiriwa kwa wahasibu raia kulilenga kuwawezesha ‘kuwabishia’ viongozi wa polisi ambao wangeonekana kutumia zaidi amri badala ya kanuni na miongozo ya fedha.

“Mwongozo wa kwanza kabisa kwa askari ni utii, ukiwa na mhasibu askari, kama koplo, hawezi kukataa au kuhoji amri ya mkuu wake inayomtaka atoe fedha.

“Mhasibu askari anapokaidi maagizo au amri anaadhibiwa kijeshi, lakini kwa raia hiyo haiwezekani,” kimesema

Chanzo chetu.

Inaelezwa kuwa uamuzi wa kuwafanya wahasibu wawe waajiriwa Hazina ulifikiwa tangu uongozi wa awamu ya kwanza kwa lengo la kuleta nidhamu za kihasibu kwenye matumizi ya fedha.

“Wakubwa wetu (viongozi wa polisi) hili jambo linawasumbua sana, hawajui wamweleze nini mheshimiwa, lakini ukweli ndiyo huo kwamba wanaona uzito kuwa na wahasibu ambao ni askari.

“Wakati fulani uamuzi kama huu ulijaribiwa kwenye vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama na kwa kweli kulitokea matatizo makubwa sana kwenye matumizi ya fedha, ikaamuriwa utaratibu wa kuwatumia wahasibu ambao ni raia, uendelee,” kimesema chanzo chetu na kuongeza:

“Kwa uelewa wangu mdogo nadhani kuwekwa watumishi raia kwenye majeshi ilikuwa ni kuwadhibiti hawa wanaojiita afande hususani katika amri zao.

“Mfano RPC anamfuata mhasibu na kumwambia lipa haya malipo, na kanuni ya Jeshi ni tekeleza kwanza ndiyo uhoji baadaye.

“Watumishi raia walikuwa na nafasi ya kuhoji anachoona hakielewi, askari huwa hawana.”

3162 Total Views 1 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!