KUNDI la kigaidi la Al-Shabaab la nchini Somalia ko kwenye wakati mgumu kama Boko Haram la Nigeria ambalo taarifa za kuuawa kwa kiongozi wake, Abubakar Shekau.

Kutokana na hali hiyo, taarifa zinasema kwamba kumekuwa na mawasiliano baina ya makundi ya kigaidi kuunganisha nguvu za pamoja ili kukabiliana na hali ya kuzidiwa na wapinzani wao katika harakati zao.

Baadhi ya vyombo vya habari duniani vilitangaza taarifa za kuuawa kwa Shekeu- kiongozi wa kundi la wanamgambo wenye itikadi kali ya kiislamu la Boko Haram.

Mbali ya kuumua kiongozi huyo, Jeshi la Nigeria limesema kwamba limefanikiwa kuwakamata wanamgambo wa Boko Haram zaidi ya 260 eneo la Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa jeshi hilo kumekuwa na makundi kwa makundi wanajisalimisha, lakini hata hivyo taarifa ambazo wamezipata zinasema kwamba wale walioko mafichoni wameanza kupata nguvu mpya kutoka kwa Al-Shaabab kutoka Afrika Mashariki.

Rais Nigeria, Goodluck Jonathan ametaka ulimwengu kuchukua hatua za haraka kukabiliana na vitisho hivyo kwani serikali yake imepata taarifa kwamba magaidi hao wameunganisha nguvu.

“Lazima wasichana wale 200 waokolewe. Magaidi hawa wameungana na wenzao wa Al-Shaabab na Al-Qaida, tunaomba Afrika nzima tusaidiane, tunaomba dunia nzima tusaidiane,” alisema Jonathan.

Tayari Jeshi la Polisi lililoweza kumpata msichana mmoja aliyeachiwa huru wiki iliyopita. Boko Haram iliwachukua mateka wasichana hao kutoka shule yao eneo la Chibok karibu na mpaka baina ya Nigeria na Cameroon Aprili, mwaka huu.

Habari za kushitua zaidi kwa nchi za Afrika Mashariki ni siri iliyotolewa na Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa (UN), Augustine Mahiga aliyesema kwamba amepata kushuhudia vijana wa Kitanzania wakishirikiana na kundi la kigaidi la Al-Shabaab la nchini Somalia.

Mahiga, alitoa ushuhuda huo mjini Dodoma wiki iliyopita, wakati wa maadhimisho ya siku ya amani ya kimataifa na kuwataka vijana kutoshabikia machafuko, kwani vita ikianza hakuna tena utu.

Alisema amewashuhudia vijana hao wa kitanzania wakipigana Al-Shabaab nchini Somalia na wakati mwingine maiti zao zikiwa zimezagaa mitaani.

Alifafanua kuwa baadhi ya vijana hao aliopata kuzungumza nao, walimweleza kwamba wanajiunga na vikundi hivyo kwa ajili ya kutafuta fedha na kwamba sasa wengine wako nchini Yemen.

Balozi Mahiga ambaye ni msimamizi wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, alisema kwa sasa kundi hilo la kigaidi limebanwa na kwamba linahaha kutafuta msaada ambako sasa wanaupata kutoka kwa Boko Haram.

Balozi Mahiga alisema kwamba wanaojiunga na makundi hayo wanatafuta ajira na fedha, lakini akasisitiza kwamba kundi hilo sasa limefungiwa milango ya kupata fedha kutoka nje.

Pamoja na hayo Jeshi la polisi la Uganda limeonya Tanzania kuwa makini na makundi hayo kwani yamepanga kushambulia nchi zote za Afrika Mashariki baada ya kuteketeza maeneo mbalimbali nchini Kenya.

 

“Al-Shabaab ni hatari kwa nchi za Afrika Mashariki. Wanapanga kutekeleza mashambulizi Kampala na katika miji mingine, lakini tumezuia mashambulizi hayo,” alisema Mkuu wa jeshi la polisi nchini Uganda, Kale Kayihura.

By Jamhuri