DODOMA

EDITHA MAJURA

Mwanafunzi wa Darasa la Nne, anayesoma shule iliyopo Kata ya Nzuguni, (majina yanahifadhiwa kimaadili) amekuwa akilawitiwa na mwendesha pikipiki, maarufu kama bodaboda tangu mwishoni mwa mwaka jana hadi mwaka huu, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Taarifa hizi zinaibuka ikiwa ni mwezi mmoja tangu JAMHURI liliripoti habari za mwanafunzi mwingine wa shule hiyo, kushindwa kuendelea na masomo ya Darasa la Tano, kwa kupewa mimba na baba yake mdogo.

Mwanafunzi huyo ameeleza kuwa amekuwa akilawitiwa na mtuhumiwa, lakini ameamua kusema baada ya kushindwa kustahimili maumivu makali, anayopata. Polisi wamepewa jina la mwanafunzi, shule na mwalimu wake.

Binti amemweleza walimu na wazazi wake kuwa kijana huyo amekuwa akimchukua kwa pikipiki mara kwa mara anapotoka shuleni na kumpeleka kwenye eneo lililo mwishoni mwa mtaa wa Nzuguni ‘B’ ndani ya mapagale (nyumba ambazo ujenzi wake haujakamilika, ambazo watu hawajaanza kuishi) na kumuingilia kinyumbe na maumbile.

Kwa nyakakati tofauti, JAMHURI limefanya mahojiano maalumu na baadhi ya walimu na wanafamilia ya binti husika, ambapo imeelezwa kuwa binti huyo amesema mtuhumiwa kila alipomfanyia tendo hilo alimpa pipi bomu (yenye kijiti cheupe) na Sh. 500.

Pamoja na zawadi hizo, alimuonya kutothubutu kumweleza mtu yeyote kuwa alikuwa akimfanyia vitendo hivyo kwasababu iwapo angesema, angemwua na kutokomea kusikojulikana.

Mwalimu Mkuu anayekamilisha taratibu za kustaafu, Lilian Lwiva, amekiri kumfahamu mwanafunzi huyo na kupokea taarifa za kutendewa ukatili huo ambazo amesema zimemshtua na kumsikitisha kwani binti ni mtaratibu, mpole na anatoka kwenye familia inayomcha Mungu.

“Hii tabia haikuwepo hapa shuleni ila mwaka juzi ndiyo tulianza kuona mabadiliko ya tabia kwa baadhi ya watoto, tukafanya mahojiano na kubaini mwanafunzi (wa kiume) ambaye sasa yupo darasa la sita, aliyehamia kutoka shule nyingine (jina linahifadhiwa) ya mjini Dodoma ndiye aliyefundisha wenzake,” ameeleza Mwalimu Lwiva.

Amesema jumla ya wanafunzi 6 waligundulika kulawitiana, kinara akiwa ni huyo aliyehamia na kwamba uongozi wa shule ulichukua hatua stahili, Mtendaji wa Mtaa akawapelekea kituo cha polisi NaneNane ambako waliadhibiwa na baadhi ya wanafunzi walihamishwa shule na wazazi wao.

Baada ya tukio hilo amesema hali ilikuwa shwari mpaka mwaka huu ambapo taarifa za baadhi ya wanaume kuwatendea ukatili wa kingono baadhi ya wanafunzi kuiibuka tena.

 

Ilivyogundulika

Mmoja wa walimu wa Darasa la Nne, amesema baada ya kutoridhishwa na mabadiliko ya kitabia ya binti huyo walianza kufatilia nyendo zake na kubaini alikuwa mara nyingi akichukuliwa na mmoja wa madereva wa bodaboda, anapotoka shuleni.

“Kwakuwa familia yake inafahamika (babu wa binti ni Mchungaji wa kanisa moja mjini hapa), tukawasiliana nao na kuwataka nao wafanye ufuatiliaji wa nyendo za binti yao. Tukawa tunapeana taarifa bila yeye kufahamu mpaka ilipofika hatua ya kuamua kumuhoji kwa nyakati tofauti,” ameeleza Mwalimu huyo.

Kwa upande wa familia, mmoja wa wanafamilia amelieleza JAMHURI kuwa kwa kubadilishana taarifa na walimu walifanikiwa kubaini kuwa binti yao alikuwa akichelewa kurejea nyumba.

“Walipokuwa wakitoka shuleni Saa 8:00 mchana baadhi ya siku alikuwa akifika nyumbani Saa 11:00 jioni na siku nyingine alikuwa akirudi kwa wakati unaotakiwa. Tukabaini alikuwa akitoroka shule; alipotoka darasani kwa ajili ya mapumziko hakurudi darasani wala kuja nyumbani,” ameeleza mmoja wa wazazi ndani ya familia hiyo.

Ndipo mwishoni mwa mwezi uliyopita pande hizo mbili ziliafikiana kumbana na binti aeleze kulikoni? Upande wa wazazi na shuleni, wote wanasema walipata wakati mgumu kumfanya azungumze, lakini hatimaye alieleza yote aliyokuwa akifanyiwa tangu mwishoni mwa mwaka jana.

“Walimu walishindwa kujizuia kutokwa machozi, wakati wakimsikiliza binti akieleza jinsi alivyoharibiwa yaani hatukutegemea kabisa kuwa naye angekuwa miongoni mwa watoto waliofanyiwa unyama huu,” ameeleza mmoja wa walimu waliomuhoji na kumchunguza.

Mtuhumiwa alivyokamatwa

Katikati ya mwezi uliyopita mmoja wa wanafamilia alifika kituo cha Bodaboda anakopaki mtuhumiwa na kumkodi ampeleke mahala kumbe alimpeleka nyumbani kwa babu yake na binti huyo ambapo baada ya kumfikisha, wanafamilia wa kiume walitoka na kumkamata.

“Tulizuia wananchi kuchukua sheria mkononi, tukamfikisha kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa ambaye alipiga simu polisi wakafika na kumchukua mpaka Kituo cha Polisi cha Kati,” amesema mwanafamilia huyo.

Amesema wakati wakiendelea na shughuli hizo, baba mzazi wa binti alikuwa amefungiwa chumbani chini ya uangalizi maalum, kwani baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa uongozi wa shule, hali yake kisaikolojia ilionekana kutokuwa nzuri na wanafamilia walihofia angeweza kufanya jambo baya dhidi ya mtuhumiwa.

Jumatano ya mwanzoni mwa mwezi huu, gwaride la utambuzi lilifanyika kwenye kituo cha polisi na taarifa za uhakika zimeeleza kuwa binti alimtambua mtuhumiwa kwanza kwa kutokea mgongoni na baadaye usoni.

Imeelezwa na wanafamilia kuwa wameelekezwa na afisa wa upelelezi anayeshughulikia kesi hiyo kwamba watulie nyumbani, watapigiwa simu kufahamishwa siku ambayo mtuhumiwa atapelekwa mahakamani.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alipoombwa kuzungumzia tukio hilo wiki iliyopita, amesema mpaka wakati huo alikuwa hajapewa taarifa ya tukio hilo na kuomba apewe muda afatilie, kabla hajalizungumzia.

Sheria ya kujamiiana

Mwaka 1998 Bunge lilitunga Sheria ya Makosa ya Kujamiiana na Sheria hii ilirekebisha baadhi ya makosa kwa kuyafafanua zaidi katika Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya Juzuu iliyofanyiwa marekebisho 2002 na kuongeza mengine.

Kwa mfano kosa la kubaka lilifafanuliwa zaidi na swala la ridhaa liliondolewa kabisa kama kosa la kubaka litafanyika dhidi ya mtoto aliye chini ya miaka 18.

Adhabu Katika Kosa la Kubaka
a. Kifungo cha maisha
b. Au kifungo cha miaka isiyopungua 30 pamoja na viboko au pasipo
viboko na faini.
c. Mkosaji atatakiwa kulipa fidia kwa mhanga wa kosa au mlalamikaji.
d. Kwa kosa la kubaka mtoto chini ya miaka kumi mtenda kosa lazima
ahukumiwe kifungo cha maisha.

Binti alazwa siku 3

Binti huyo alilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma katikati ya mwezi Februari, mwaka huu na sasa ameacha masomo yupo nyumbani.

2031 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!