DODOMA

NA EDITHA MAJURA

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mwasiliano, Elias Kuandikwa, ametoa wito kwa wenye uwezo wa kujenga nyumba za kupangisha, kufanya hivyo mkoani Dodoma ili kusaidiana na serikali katika kuwapatia  makazi bora, wanaohamia kutokana na utekelezaji hatua ya serikali kuhamishia makao makuu yake mjini hapa.

Waziri Kuandikwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ushetu, mkoani Shinyanga, amesema licha ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kumiliki jumla ya nyumba 960 za kibiashara mkoani humo, hawajakidhi mahitaji ya nyumba yaliyopo kwa sasa.

“Namshukuru Rais, Dkt. John Magufuli, kuridhia nyumba 431 zilizokuwa chini ya CDA na nyingine 71 zilizokuwa chini ya TAMISEMI zilizopo Mpwapwa na Kodoa kuwa chini ya TBA lakini nimeambiwa pamoja na ongezeko hilo la nyumba bado mahitaji ni makubwa, hivyo ninatoa wito kwa watu binafsi kuwekeza katika eneo hili ili wasaidiane na serikali,” amesema Naibu Waziri.

Hata hivyo, Kaimu Meneja wa TBA wa Mkoa wa Dodoma, Steven Simba, amesema pamoja na changamoto nyingine, majengo wanayopangisha yamechakaa, hali inayosababisha washindwe kupangisha kwa gharama halisi ya soko na kwamba hata majengo yaliyokuwa ya CDA, yanahitaji ukarabati utakaogharimu jumla ya Sh. Bilioni 17.782.

Mpango wa kukabiliana na changamoto hiyo umeelezwa na Simba, kuwa ni kutumia makusanyo ya kodi kukarabati majengo hayo kuyaongezea thamani. Hata hivyo, amesema mpango huo unaweza usitekelezwe kutokana na wapangaji wengi kutolipa kwa wakati kodi ya pango.

“Pamoja na jitihada tunazofanya kukabiliana na changamoto hii, tunaomba mheshimiwa Naibu Waziri, ofisi yako itusaidie kuhimiza taasisi za serikali kulipa kwa wakati huduma zinazopata kutoka kwetu. Utekelezaji wa mpango mkakati wetu unakwama kwa kiasi kikubwa kutokana na tunaowahudumia kutolipa kwa wakati madeni tunayowadai,” amebainisha Simba.

Ametoa mfano kwa kutumia nyumba 458 ambazo tangu awali zilikuwa zikimilikiwa na TBA, kwamba ilitegemewa katika Mwaka wa Fedha 2017/2018 wakusanye jumla ya Sh. bilioni 1.109 (1,108,800,000.00) lakini mpaka sasa wamekusanya Sh. milioni 464.879 tu.

Amesema nyumba zinazotumiwa na viongozi, watumishi na taasisi za serikali zinadaiwa jumla ya Sh. bilioni 1.286.

Samba ameiomba serikali kuendelea kutenga fungu kwa ajili ya kukarabati nyumba za viongozi na kununua thamani, kwani kumekuwa na malalamiko kutoka kwa viongozi kwamba samani zilizo katika nyumba wanazoishi ni chakavu na hazibadilishwi kwa wakati.

Naibu Waziri asononeshwa

Baada ya kufanya ziara na kuona hali ya majengo yaliyo chini ya TBA ikiwemo makazi ya viongozi na watumishi yaliyopo Area D na Kisasa mjini Dodoma, Naibu Waziri Kuandikwa, amesema ipo haja ya kuona uwezekano wa kuchukua hata mkopo benki majengo yote yafanyiwe ukarabati na kuongezewa thamani hata kodi itakayotozwa iendane na bei ya soko.

Amesema pamoja na uchakavu wa majengo, hata hali ya usafi wa mazingira katika makazi mengi hairidhishi, hivyo akaagiza TBA kuangalia uwezekano wa kukokotoa gharama za usafi ziongezwe kwenye kodi inayolipwa na wapangaji wake, kusudi jukumu hilo walitekeleze wao badala ya kuliacha kwa mpangaji.

Ameahidi kushughulikia kwa haraka na ukamilifu, yote yaliyoelezwa na wakala huo, kupitia taarifa yake iliyowasilishwa kwake na Simba ambapo amesema anataka huduma zinazotolewa na TBA ziwe za kupigwa mfano kwa ubora wake.

Amesema pia ni muhimu kuweka utaratibu utakao wajibisha wapangaji ambao wanapotumia nyumba hizo ama kwa makazi au shughuli nyinginezo, wakafanya uharibifu; Ikiwezekana, mpangaji anapoomba nyumba atozwe fedha ambayo itafidia gharama za ukarabati wa jengo endapo wakati anahama itabainika amefanya uhalibifu.

Kudorola ujenzi wa jengo la NEC

Ujenzi wa jengo la kisasa la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), unaotekelezwa na Kikosi cha Ujenzi cha TBA kinachojulikana kama “Tanzania Building Contractor” uliotarajiwa kukamilika ifikapo Julai mwaka huu, umesimama kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza.

Msimamizi Mkuu wa Mradi huo, Mhandisi Yohana Mashausi, ametaja moja ya changamoto hizo kuwa ni kuadimika kwa baadhi ya vifaa ikiwamo kokoto na kuongezeka kwa bei ya nondo na saruji katika vipindi tofauti.

“Tunashauri watu wawekeza kwenye kuzalisha na kuuza vifaa vya ujenzi, hususan kokoto kwasababu zinahitajika sana. Tumefikia hatua ya kushauri uongozi uanzishe karakana yetu ya kuzalisha kokoto na wameishaanza kufanyia kazi kwani eneo limepatikana Nzuguni,” amebainisha Mhandisi Mashausi.

Naibu Waziri Kuandikwa, amesema hajafurahishwa na mradi huo kusimama akaagiza NEC na TBA (mkandarasi) kuharakisha kuondoa vikwazo vilivyojitokeza utekelezaji wa mradi huo uendelee kwakuwa ni jengo muhimu hasa kwa kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa viongozi unaotarajiwa kufanyika Mwaka 2020.

By Jamhuri