Na Moshy Kiyungi, Tabora

Imekuwa kawaida kuandika historia ya mtu pindi anapofariki. Katika makala hii namuangazia mwigizaji mkongwe wa Filamu na vichekesho Tanzania, Amri Athuman maarufu kama King Majuto. Mchekeshaji Amri Athuman ‘Mzee Majuto’ amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Saalam baada ya kuugua.

Ofisa Habari wa Chama Cha Waigizaji Mkoa wa Kinondoni, Masoud Kaftany alithibitisha taarifa kuhusu kuugua kwa msanii huyo mkongwe.

Alisema mwigizaji huyo alipelekwa hospitali hapo baada ya kuzidiwa.

“Ni kweli Mzee Majuto anaumwa na sasa hivi tupo naye hapa Muhimbili anaendelea na matibabu,” alisema Kaftany.

Afisa huyo amekiomba Chama cha Waigizaji, wadau wa filamu Tanzania na Watanzania wote kumuombea mwigizaji huyo aweze kupona haraka.

Hivi sasa amelazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili akisumbuliwa na ugonjwa wa ‘Tezi Dume’.

Hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli na mkewe, walimtembelea hospitalini humo kumjulia hali.

Kuna kipindi nguli huyo alizushiwa kifo baada ya taarifa ambazo zilikuwa zimesambaa kuwa amefariki dunia, lakini ikathibitishwa kuwa si za kweli.

Kabla ya kusambaa kwa uzushi huo,

Mchekeshaji King Majuto alikuwa amelazwa hospitali kwa muda wa siku tatu, ameruhusiwa na kurudi nyumbani kwake baada ya kufanyiwa upasuaji wa hernia (ngiri) mkoani Tanga.

Mke wa muigizaji huyo, Bi. Aisha Majuto alisema kwamba tatizo lililokuwa likimsumbua mumewe lilianza siku nyingi ingawa kwa wiki iliyopita hali ilibadilika na kuwa mbaya zaidi hadi kufikia kulazwa.

“Ni kweli tulikuwa tumelazwa, lakini mume wangu amesharuhusiwa na kurudi nyumbani. Tatizo ni hernia (Ngiri) na ameshafanyiwa upasuaji.”

Wasifu wa Amri Athuman’ King Majuto’ unaeleza kuwa alizaliwa mwaka 1948 mjini Tanga wakati huo.

Alipata elimu katika shule ya msingi Msambweni, kuanzia mwaka 1958.

King Majuto akiwa na umri mdogo wa miaka 9, alikuwa akiigiza katika majukwaa.

Anao uwezo mkubwa wa kuigiza mwenye mashabiki wengi kutokana na maonyesho mbalimbali, vichekesho vyake aliyoshiriki nchi mbalimbali.

Aidha King Majuto ni mtunzi na mwandishi wa miswada .

King Majuto ndiye mwigizaji wa kwanza kuandaa kazi zake katika mikanda na kuuza akiwa na Tanzania Film Company (TFC).

Licha ya umri kuonekana kuwa umemtupa mkono, mkongwe huyu wa sanaa ya Komedi, Amri Athuman ‘King Majuto’ anaendelea kutamba na yaelezwa kuwa bado hakuna wa kumpiku katika fani hiyo.

Siri pekee ya kusalia kwenye tasnia hiyo hadi leo ni uvumilivu, nidhamu na ubunifu awapo kazini, ndiyo vilivyompatia mafanikio niliyonayo kwenye Komedi.

Aliwahi kutamka kuwa anashukuru amevuna mambo mengi, vikiwamo ubunifu na msimamo kutoka kwa aliyekuwa gwiji mwenzie, marehemu Said Ngamba ‘Alwatan Small’ au maarufu kama ‘Mzee Small’ ambaye kwa mara ya kwanza alikutana naye mwaka 1973, Mtaa Moshi, Ilala, jijini Dar es Salaam.

Akielezea namna alivyolipata jina la ‘King Majuto’, alisema kuwa alipokuwa kwenye kundi la DDC Kibisa, aliigiza michezo mingi ambayo mwisho ilikuwa akimalizia kwa kujuta na watu wakaamua kumpachika jina hilo.

King Majuto alisema kuwa uzembe katika kazi ya sanaa pamoja na wasanii wavivu wenye kawaida ya kujivutavuta kufika ‘lokesheni’, ni kati ya kero kubwa kwa King Majuto anayevutiwa zaidi na waigizaji Jacob Stephen ‘JB’ na Brother K wa kipindi cha ‘Futuhi’.

“Faida niliyokwishaipata kwenye uigizaji ni kusomesha watoto wangu, kujenga nyumba tatu, kununua magari matano, kumiliki shamba na mifugo,” alisema King Majuto.

Mzee huyo anayo sifa anayojivunia ya kuwaibua wengi katika maigizo.

King Majuto anaitaja faida nyingine aliyoipata kutokana na uigizaji kuwa ni kuanzisha kundi lake binafsi liitwalo King’s Entertainment lenye wasanii 75, ambalo maskani yake yapo CCM Hall, jijini Tanga.

Kifamilia, King Majuto ni baba wa familia mwenye watoto 12 ambao wote ni waigizaji kama alivyo yeye isipokuwa mtoto wake wa kwanza aitwaye Athuman aliyeamua kuingia kwenye muziki akipiga gitaa.

Matarajio yake makubwa ni kuwa mkulima baada ya kusataafu kazi hiyo.

King Majuto amekuwa msanii huru tangu 1983, baada ya kupitia vikundi vya sanaa vya JKT, JWTZ, Zimamoto na Bandari.

“Ninachowausia wasanii wenzangu ni kujitahidi katika kuthubutu kwasababu ukiogopa kuthubutu kwenye kazi yako, utafeli,” alisema King Majuto ambaye hujisikia raha anapokutana na Brother K kwenye filamu.

Kama unadhani kuwa siku moja King Majuto atageukia uanasiasa umekosea, kwani anasema, atabaki mwigizaji kwa kuwa vitu hivyo haviingiliani.

Majuto ameweza kustawisha afya yake kwa kipindi kirefu kwa kutumia kula mbogamboga zinazomfaa kwa matumizi ya nyumbani.

Anamiliki shamba lililopo maeneo ya Kiruku limeanza kuleta faida, kutokana na mazao ya mananasi, machungwa, mihogo, minazi na maembe vinavyovunwa kwa wingi hivi sasa.

King Majuto anayependa kuimba akijisifu uwezo wa sauti anao ila anakwazwa na umri kumtupa mkono.

Wakati wa uongozi wa rais wa awamu ya nne ya Dk. Jakaya Kikwete, alitamka kuwa anaendelea kumuomba rais huyo amsaidie Trekta kwa ajili ya kilimo, ingawa ulipita mwaka wa tatu bila kujibiwa.

Talanta ya King Majuto ameweza kupatiwa matangazo lukuki ya biashara kutoka katika mashirika na kampuni mbalimbali yanayorushwa katika luninga mbali mbali nchini.

Wapenzi, mashabiki pamoja na Watanzania wote, tumuombee King Mjuto aweze kupona haraka.

By Jamhuri