Nimeamka nikiwa na afya njema kabisa leo. Nimeamka nikiwa nina akisi maisha halisi na yale ya baadhi ya watu ya kuigiza. Nimeamka nikiangalia maisha halisi ya kujitegemea kwa kilimo na ufugaji na maisha halisi ya kutegemea siasa. Nimeanza kuona uhalisia wa kile ambacho tulikuzwa nacho enzi za maazimio ya utendaji na siyo maazimio ya kisiasa.

Leo nimepata fahamu vizuri kwamba mimi siye wa leo ni wa kale kwa kuwa mambo mengi ninayofikiria ni yale ya kale. Nafikiria maendeleo ya jembe la mkono, ufugaji wa kienyeji, ujengaji hoja wa kizamani na biashara iliyopitwa na wakati. Ninafikiria mawasiliano ya kizamani sana, hii ndio taabu ya kuwa wa kizamani.

Naandika barua hii nikiwa najua fika kwamba mimi ni mtu wa kizazi cha zamani, ambaye nimeshindwa kwenda na wakati, ambaye nimeshindwa kukubaliana na dhana halisi ya sasa ya kimaendeleo. Najaribu kufananisha mambo halisi na ya kuiga, bado nashindwa kushabihiana na ukweli wa maisha yetu ya leo.

Najua kuwa maisha yanasonga na maendeleo yapo, ninagubikwa na wimbi zito la maendeleo ya kidhahania zaidi kuliko maendeleo halisi na yanayoshikika. Najaribu kwa ujinga wangu kuangalia maendeleo ya watu wengine na utimilifu wa kweli katika maendeleo.

Miaka ile tukipata uhuru, nchi nyingi duniani zilikuwa maskini kama sisi, na zipo ambazo zilikuwa masikini zaidi yetu. Nakumbuka jambo kubwa sana ambalo linaniumiza kichwa sana leo jinsi ambavyo Hayati Mwalimu Julius alipokwenda China kuomba msaada wa kujengewa reli ya TAZARA na akaishia kusema nilikuja kwenu nikiamini ni matajiri, nilikuja kuomba msaada wa kujengewa reli, lakini kwakuwa nimezunguka hapa China na kuona jinsi ambavyo mnapambana na maendeleo kama kwetu sina haja ya kuwaomba msaada wenu. Akasema tena nimegundua kwamba msaada ninaoomba ni robo ya bajeti yenu ya taifa.

Cha ajabu Wachina wale kwa urafiki wao na Tanzania na kuelewa maana ya maendeleo waliamua kutoa robo ya bajeti yao kwa manufaa ya maendeleo ya taifa letu na Zambia. Ulikuwa ni uamuzi mgumu kwa taifa masikini linalohitaji kufikia maendeleo kwa ajili ya wananchi wake.

Leo baada ya nusu karne tayari wenzetu wale waliotukopesha robo ya bajeti yao ni matajiri wanawaowakopesha walioendelea miaka ya nyuma ya nusu karne, sisi tuliokopeshwa wakati ule bado ni taifa mojawapo ya mataifa masikini duniani. Afya yangu niliyoamka nayo inanisuta na kusema hapana kuna mahali tumekosea na tuna usugu wa maradhi ambayo kamwe hatutapona na umasikini huu.

Tanzania ni nchi kama nchi nyingine, tunahitaji kubadilika ili tuweze kufika katika maendeleo yanayosemwa na mataifa mengine. Tunahitaji kwenda na kasi kama ya mataifa mengine. Maendeleo siyo kuyaonyesha kwa maneno ya siasa bali ni kwa matendo ya umiliki wa vitu vinavyoshikika. Maendeleo ni pamoja na watu na siyo mali.

Nimewaza mambo mengi sana, juu ya maendeleo ya majukwaani, maendeleo ya katika semina mbalimbali, maendeleo ya kuiga na maendeleo ya mbali ambayo hatujayafikia yanayoakisi kurukwa kwa maendeleo ya kipindi na wakati maalumu.

Maendeleo ya tekinolojia yameshika kasi kuliko mataifa yaliyoendelea. Sasa Watanzania tunafikiria kwenda mwezini kwa maneno badala ya vitendo, tunapanda majukwaani na kunadi siasa za kwenda mwezini badala ya kufungua viwanda vya mbolea, viatu, zana za kilimo nakadhalika.

Watanzania tumefika mahali ambapo tunadhani kwamba maendeleo yatapatikana kwa kufanya siasa na kutokuwa wazalendo kwa taifa letu. Tunadhani kwamba maendeleo yatapatikana kwa kubishana badala ya kufanya kazi, tunadhani kwamba maendeleo yapatikana kwa kujifananisha na walioendelea kuliko sisi.

Nadhani turudi katika misingi ya kufanya kazi badala ya kuwa na njozi, turudishe maazimio ya kazi badala ya maazimio ya kisiasa. Tuamue kuwa katika mchakato wa maendeleo au kuwa masikini na kuamini ni matajiri kwa kuangalia matajiri.

Nazidi kuakisi maisha ya siku zijazo, maisha ya haraka na kusahau mara moja jambo muhimu, nayaona maisha ya mpito yasiyo ya asili na kuyaona maisha ya kudumu ya kuigiza. Ni njozi zangu ambazo nimeamka nazo leo, maisha ya kubahatisha na siyo ya kuhakikisha. Maisha ya kubambikiwa na siyo maisha yetu na mwisho nikaona niandike waraka huu kwenu kizazi cha mpito.

1764 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!