Mengi mazuri yanayomhusu Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine, yamesemwa na yanaendelea kusemwa.

Kwa Mtanzania yeyote wa kweli, kamwe hatachoka kusikia mengi yaliyofanywa na Sokoine wakati wa uongozi wake.

Miaka 30 sasa tangu alipoaga dunia, shujaa huyu hajulikani kwa vijana wengi wa Tanzania. Safu hii ni fupi mno, kiasi kwamba haiwezi kumweleza japo kwa nukta mtu huyu hata akaeleweka kwa vijana wengi.

Itoshe tu kuwaasa vijana kuyasaka kwa udi na uvumba maandiko yanayomhusu shujaa huyu wa Tanzania, ambaye mfano wake kwenye nafasi ya Waziri Mkuu, haujapatikana.

Licha ya wengi kumzungumza Sokoine, hiyo haitoshi kutufanya nasi tusiweke neno wakati huu wa kumkumbuka.

Moringe alikuwa kipenzi cha Watanzania wengi, hasa makabwela. Alipendwa na watu wa jinsi, hali na rika zote. Hakuwa na makuu. Alikuwa mcha Mungu wa kweli. Hakuwa kiongozi wa kupayuka-payuka, bali alikuwa mpole, msikivu na mwenye kusimama katika ukweli na haki. Uwajibikaji na uadilifu ndiyo uliokuwa msingi mkuu wa Sokoine.

Kwa wasiomjua, wanaweza kudhani yanayosemwa juu yake yanatiwa chumvi, lakini ni ukweli ulio wazi kwamba mtu huyu alikuwa wa aina ya pekee, kiasi kwamba hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alimpenda na kumweka mbele.

Waliofanya kazi na Sokoine wanasema alipokuwa na jambo, alibeba faili mwenyewe na kwenda ofisini kwa Rais Mwalimu Nyerere akamsubiri aingie ofisini. Mwalimu alipoingia ofisini, alimkuta na hapo alijua kuna jambo lisilo la kawaida. Bado wapo wanaojiuliza muda ambao kiongozi huyu aliweza kuutumia kulala. Hawajapata majibu.

Sokoine alikuwa kiona mbali. Ndiye mwasisi wa usafiri wa daladala. Alimshauri Mwalimu kuwa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) pekee lisingeweza kukabiliana na adha ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam. Kwa mawazo yake, usafiri wa daladala ukaanzishwa Dar es Salaam na kuenea katika miji mingine nchini.

Sokoine alishiriki kwa kiwango kikubwa kuifanya Serikali iruhusu kuwapo kwa maduka ya watu binafsi ili kusaidia utoaji huduma muhimu kwa wananchi. Tunaweza kusema mengi, lakini kwa ufupi ni kwamba Moringe ndiye chachu ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji uchumi wa nchi yetu.

Tofauti na viongozi wengi wa sasa waliojaa ubabaishaji, ahadi za uongo, ulaghai, wizi na kujilimbikizia mali, Sokoine hakuwa mtu wa aina hiyo. Hilo linathibitishwa na ukwasi wake mdogo aliouacha baada ya kifo chake. Inaelezwa kwamba hata viatu hakuwa na jozi zilizozidi tatu!

Sokoine alikuwa tumaini kubwa la wanyonge na kwa hakika aliwafanya Watanzania waipende nchi yao kwa moyo wa dhati kabisa. Kila lililosemwa na Sokoine lilipokewa na wananchi kwa shangwe.

Vita dhidi ya wahujumu uchumi na walanguzi ilipotangazwa, mwitikio wake ulikuwa mkubwa mno. Sokoine alikuwa mtu wa watu.

Tunapomkumbuka Sokoine miaka 30 baada ya kifo chake, viongozi wa sasa wanapaswa waone aibu. Wajiulize, wana lipi walilojifunza kutoka kwa shujaa huyu? Kwa hakika Sokoine ataendelea kuwa alama ya aina ya kiongozi anayestahili kuliongoza Taifa hili. Watanzania wanamhitaji Sokoine mwingine 2015. Tunamuomba Mwenyezi Mungu ampe pumziko la amani, Amina.

2354 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!