Kwenye safu hii, toleo Na. 391, niliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari: “Rais Magufuli wasaidie wanyonge hawa”.

Nilichoandika kilihusu mateso yanayowafika maelfu ya Watanzania katika magereza nchini mwetu. Nilianza na kisa cha kweli cha mama mmoja niliyemkuta akitoka kumwangalia mwanae katika mahabusu ya Gereza la Kisongo, Arusha.

Mwanae, Gerald Silvanus Sambayuka (23) ni dereva wa bodaboda. Inadaiwa kuwa alikamatwa nje ya duka akimsubiri mteja wake. Baadaye akaambiwa kosa lake ni la unyang’anyi wa kutumia silaha! Anaumia rumande tangu mwaka 2017.

Kwenye makala hiyo niliandika haya: “Magereza na mahabusu zimejaa pomoni kwa kesi nyingi za kutungwa na wala watu hawana hofu ya Mungu. Tuna binadamu wenzetu wanaoteseka kwa sababu tu ya unyonge wao. Hakuna aliyependa azaliwe katika mazingira ya unyonge.

“Wapo Watanzania mamia kwa maelfu walionyimwa dhamana kwa makosa au tuhuma zinazostahili dhamana. Matokeo ya uamuzi huo ndiyo haya tunayoona leo ya kujaa kwa magereza na mahabusu zote nchini.

“Tukio la Tabora limewagusa wengi wenye ndugu magerezani na mahabusu. Hawa wangependa kuona wakitendewa haki kama mwenzao wa Tabora.

“Kama nilivyosema awali, kuiacha kazi hii kwa Rais Magufuli pekee ni jambo la kumwonea. Anaweza kupokea makontena ya malalamiko.

“Tunavyo vyombo vya kikatiba na kisheria vya kushughulikia mambo ya aina hii ili kuondoa uonevu katika taifa letu. Tuna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, tuna vyombo vingi vya kusimamia masilahi na haki za wananchi. Tunao viongozi, kuanzia kwa waziri wenye mamlaka ya kuchunguza malalamiko haya. Lakini tukiri kuwa, ama sheria zetu hazivipatii vyombo hivi nguvu zinazostahili, au wenye dhima hiyo wameamua kukaa kimya maana wanaoumia bila hatia si ndugu au jamaa zao. Bodi ya Parole sijui kama ina ubavu wa kukabiliana na hali hii kwa wafungwa.

“Kwa hali ilivyo, napendekeza kwa Rais Magufuli, kwa mamlaka aliyonayo kama kiongozi wetu mkuu wa nchi, aone uwezekano wa kuunda chombo maalumu chenye wataalamu wa sheria na haki za binadamu – kitakachopita katika mahabusu zote nchini kusikiliza malalamiko ya waliowekwa humo.

“Mahabusu wanaoamini kuwa wameonewa wapewe uhuru wa kuandika malalamiko yao. Yakusanywe. Yapitiwe na jopo la wanaounda chombo hicho. Wayapime na kutoka miongoni mwayo waone mangapi ‘yanayokaribiana na ukweli’. “Wayachukue, wawaite wahusika ili wajieleze mbele yao. Kwa kufanya hivyo ukweli utabainika. Tunaambiwa wapo hadi mahabusu ambao ni wagonjwa wa akili. Wako rumande kwa miaka sasa. Hao wapelekwe kunakostahili wakatibiwe.

“Chombo hicho kiwe na majaji wastaafu na wataalamu wengine wa masuala yanayoendana na kusudio la kuundwa kwake na kiwezeshwe kwa hali na mali kwa ajili ya kupata ukweli utakaosaidia kuwaokoa Watanzania na wasio Watanzania wanaoozea mahabusu kwa kuonewa.

“Zipo taarifa zisizotiliwa shaka kwamba kuna watuhumiwa walioko mahabusu kwa miaka minane au 10 kesi zao zikiwa ‘hazijulikani’. Watu wa aina hiyo ni rahisi kubainishwa na kusaidiwa.

“Naamini kwa dhati kabisa kuwa endapo tutakuwa na chombo cha aina hiyo kitaifa, mambo mengi mabaya ya uonevu dhidi ya binadamu wenzetu yataibuliwa na watu wengi wataokolewa. Jela au mahabusu si mahali pa mtu kupelekwa kwa uonevu.

“Tanzania ni nchi huru. Viongozi wetu wanaapa kulinda haki za watu na masilahi ya nchi. Katika hali hiyo hatuwezi kuendelea kukaa kimya ilhali wapo wenzetu wanaoteseka bila hatia yoyote.

“Matamko ya kukemea ubambikiaji kesi yanayotolewa na viongozi hayawezi kupunguza wala kumaliza tatizo hili. Lililo la msingi ni kwa chombo ninachopendekeza kuingia mahabusu zote kufukua vilio vya kweli vya wanadamu wanaoteseka kwa ghiliba na husuda za wenye madaraka.

“Kwa pamoja tuifanye Tanzania iwe mahali pazuri pa kila binadamu kuona fahari ya kuishi kwa uhuru na haki. Rais Magufuli ukilifanya hili utakuwa umewatendea haki maelfu ya wanyonge na kwa hakika utaandikwa kwenye historia njema ya taifa letu.” Mwisho wa kunukuu.

Wiki iliyopita Rais John Magufuli alifanya jambo kubwa mno. Alizuru Gereza la Butimba mkoani Mwanza. Humo ndani alipokea malalamiko ya mahabusu, wafungwa na askari magereza.

Siku mbili baadaye, akiwa Kongwa mkoani Dodoma, akaagiza Wizara ya Katiba na Sheria na vyombo vya ulinzi na usalama vinavyohusika na masuala ya mahakama kupita katika magereza yote nchini kuchambua na kuwaondoa mahabusu wasiostahili kuwamo magerezani.

Rais akasema: “Siwezi kutawala nchi ya machozi; machozi haya yataniumiza, siwezi kutawala nchi ya watu wanaosikitika – wapo kwenye unyonge na unyonge wao ni wa kuonewa.” Hii ni kauli nzito.

Takwimu za Jeshi la Magereza zinaonyesha kuwa hadi Aprili mosi, mwaka huu, idadi ya wafungwa katika magereza yote nchini ilikuwa ni 17,838; na mahabusu wa mahakama zote walikuwa 19,193. Jumla kuu kwa wafungwa na mahabusu wote nchini ni 38,668. Uwezo wa magereza yote ni kuhimili wafungwa na mahabusu 29,902; hii ikiwa na maana kwamba kuna watu 8,766 waliozidi uwezo wa magereza.

Nampongeza Rais Magufuli kwa hatua hii ya kiutu. Matarajio ya wengi ni kuona agizo lake la kuwatambua mahabusu na hata wafungwa walioonewa linatekelezwa haraka iwezekanavyo. Lakini pia aangazie mahabusu wanaoteseka magerezani kwa maelezo kwamba wako kwenye hali hiyo kutokana na maagizo yake rais.

Ni ukweli ulio wazi kwamba wapo watu wanaumizwa na wabaya wao kwa kisingizio kuwa wamepewa maagizo kutoka ‘juu’. Haya yapo na yanajulikana. Mtu wa kawaida anapoambiwa ndugu yake anashikiliwa kwa maagizo kutoka juu, hawezi kufurukuta kutafuta haki. Hili naomba litazamwe pia.

Tutakuwa tunajidanganya tukiamini kuwa tunaweza kuwa taifa la watu wenye furaha kama tutapuuza mateso yanayowapata ndugu zetu wasiokuwa na hatia waliowekwa katika mahabusu na magereza mbalimbali nchini.

Tutakuwa tukitenda dhambi kwa kuamini kuwa hao wanaoonewa wanastahili shida wanazopata ilhali umma ukiendelea kufumbia macho uonevu huo.

Lakini hali hii haitabadilika kama kwanza Jeshi la Polisi lenyewe halitafumuliwa na kuwa na muundo unaoendana na ulimwengu wa leo wa haki za binadamu na utawala bora.

Kuna swali limepata kuulizwa kwamba kama KAR ilifumuliwa na kuundwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kitu gani kinatufanya Tanzania tuendelee na Jeshi la Polisi ambalo bado mambo yake kadhaa ni ya mfumo uliowekwa na watawala wa kikoloni?

Wote wanaozungumzia msongamano wa kesi na mahabusu magerezani lawama ni kwa Jeshi la Polisi. Leo hii wapo polisi wanaopokea kesi za madai na kuzipa hadhi ya kesi za jinai. Watu wanadaiana nauli ya bodaboda na wanapofikishana polisi busara pekee ya askari wetu ni kwa mdaiwa kuwekwa rumande na baadaye kuhamishiwa gerezani!

Viji-kesi vidogo vidogo visivyokuwa na kichwa wala miguu ndivyo vinavyoongoza kuwatesa maelfu ya Watanzania wenzetu magerezani. Hili halina budi kutazamwa katika muktadha wa kuhakikisha Jeshi la Polisi linasukwa upya na kuwa jeshi lenye askari weledi waliopata mafunzo ya haki za binadamu.

Kabla ya kuhitimisha, nimpongeze kwa dhati kabisa Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, aliyeshauri tuhuma za makosa yote ziwe na dhamana; lakini pia kesi zinazopelekwa mahakamani upelelezi wake uwe umeshakamilika. Hii ni kauli inayopaswa kupokewa na kufanyiwa kazi. Ni kauli ya kiongozi mkuu wa mhimili wa utoaji haki.

Kauli ya Rais Magufuli na hii ya Jaji Mkuu Profesa Juma zikiwekwa pamoja naamini Watanzania wengi watafurahia matunda ya utoaji haki nchini. Kama alivyosema Rais Magufuli, sisi tulio nje ni wafungwa watarajiwa.

Tunapotunga sheria hatuna budi kulitambua hilo. Tunaponyamaza ilhali wenzetu maelfu kwa maelfu wakiumia magerezani tutambue kuwa nasi ipo siku tutakuwa upande huo. Na kwa kuwa tulisherehekea kwa kukaa kimya bila kuwasemea wenzetu, basi nasi tutastahili kutendewa vivyo hivyo.

By Jamhuri