Serikali imezindua ndege mbili za Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) zinazotarajia kuanza kufanya safari zake katika mikoa mbalimbali nchini.

Ndege hizo aina ya Q400 zimetengenezwa na kampuni ya Bombardier iliyoko nchini Canada.

Baada ya jitihada za Serikali katika kuhakikisha ndege za Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) zinaruka, tunatarajia kuona mapinduzi makubwa katika usafiri wa anga hapa nchini pamoja na kuleta ushindani wenye tija kwa watumiaji.

Katika uzinduzi wa ndege hizo mbili uliofanywa na Rais John Magufuli, tumemsikia akiwahadharisha bodi ya kampuni hiyo  pamoja na menejimenti mpya, kutofanya kazi kwa mazoea, huku akisisitiza kila anayepanda ndege hizo lazima alipe.

JAMHURI tunaamini kwamba huo ni mwanzo mzuri kwa menejimenti ya kampuni hilo pamoja na bodi, kufanya kazi ya kuifufua kampuni hiyo na baadaye kuwa kampuni yenye kuleta tija kwa Taifa, maana kwa kipindi kirefu imekuwa ikitengeneza hasara.

Hatutarajii kuona kampuni hiyo ikirudia makosa yaliyowahi kufanywa huko nyuma, isipokuwa tunataraji kuona ubunifu zaidi utaoweza kuleta mazingira ya ushindani katika soko la usafiri wa anga, ambalo kwa sasa hapa nchini limeshikiliwa na mashirika ya ndege binafsi.

Tunaamini sifa zilizotolewa kuhusu ndege hizo, ni wazi kwamba menejimenti ya ATCL sasa ina kazi kubwa kuhakikisha kwamba walau wanarejesha matumaini yaliyokwisha potea, lengo ni kuona tunaanza na ndege mbili na baadaye kuongezeka na kusambaa nje ya anga letu.

JAMHURI tunaamini ya kuwa pamoja na changamoto za uendeshaji wa kampuni hiyo, hatutarajii kuona ATCL ikitoza gharama kubwa zaidi za usafiri kiasi cha kushindwa kumudu bei ya soko kwa safari za Mwanza, Kilimanjaro, Mbeya, Tabora, Kigoma, Bukoba pamoja na maeneo mengine ya nchi.

Sisi tunaamini kwamba, bado wapo Watanzania ambao watawaunga mkono, kwao ni fahari kusafiri na kampuni ya ndege ya Taifa, ni vyema kuanza na hao wachache na sifa za huduma zenu zisambae kila mahali.

Tunaamini kwa sasa bodi itakuwa inashughulikia mpango mkakati wa biashara utaopelekwa kwenye menejimenti kwa ajili ya utekelezaji, huku shauku ya Watanzania ikiwa juu, kuona ndege zilizonunuliwa kwa kodi zetu wenyewe zinaanza kuruka.

By Jamhuri